BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TANZANIA YAANZA KASI YA KIMAENDELEO, KUWA NA TRENI YENYE KASI YA KILOMETA 160 KWA SAA.

Tokeo la picha la photos of treni za umemeTreni ya umeme inayotarajiwa kuanza kazi baada ya miezi 30 nchini itakuwa ya pili Afrika itakayosafiri kwa mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa, baada ya ile ya nchini Morocco.

Hakika treni hii inaiweka nchi ya Tanzania katika historia ya usafiri wa haraka na wa maendeleo, baada ya kumalizika kwa ujenzi wa reli hiyo mpya ya kisasa awamu ya kwanza kati ya Dar es Salaam mpaka Morogoro utakaogharimu kiasi cha Sh2.7 trilioni.

Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO) imetiliana saini mkataba wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na kampuni za ujenzi kutoka nchi za Uturuki na Ureno.

Reli hiyo itakayokuwa na urefu wa kilomita 205 za njia kuu na 95 za kupishania treni inatarajiwa kujengwa na kampuni za Yapi Merkenzi Instant Ve Sanayi A.S ya Uturuki na Mota-Engil, Engenharia E and Construcao S.A ya Ureno, ujenzi utakaochukua miezi 30.

Pia, ujenzi huo utahusisha ujenzi wa uzio na vivuko vya watembea kwa miguu ili kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na treni itakayokuwa ikitumika itakuwa ya umeme.

Rais John Magufuli anasema kukamilika kutaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuwa na treni inayokwenda kasi (kilomita 160 kwa saa) na inayobeba uzito mkubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na ya pili barani Afrika kwa treni zinazokwenda kasi baada ya ile ya Morocco ambayo inakimbia kwa kilomita 200 kwa saa.

Katika miaka ya karibuni Kenya na Ethiopia walizindua treni zinazokwenda kasi ya kilomita 120 kwa saa lakini treni ya Kenya inatumia mafuta na ile ya Ethiopia inatumia umeme.

Rais Magufuli amesema mwendo kasi wa kilomita 160 kwa saa ni wazi kuwa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro treni hiyo itakuwa ikitumia chini ya saa 1:30 ambapo kwa basi kwa sasa ni zaidi ya saa 4:00. Kwa mtu anayesafiri kwenda Dodoma sasa atalazimika kutumia saa 2:30 kufika makao makuu hayo ya nchi kutoka muda wa sasa wa saa nane hadi tisa kwa basi.

Amesema reli hii ya kisasa itakuwa na uwezo wa kubeba tani 35 na kwa mwaka itaweza kusafirisha mzigo wa uzito wa tani milioni 17 ikiwa ni ongezeko la karibu mara mbili na nusu ya uzani wa awali.

Anasema kukamilika kwa reli hiyo hadi Mwanza na Kigoma itakuwa daraja muhimu katika uchumi wa nchi kwa kuiunganisha Tanzania na nchi za jirani ambazo hazina bandari.

Umoja wa Mataifa umetupa jukumu la kuwapa njia ya kwenda bandarini na kutoka huko na hivyo tunawajibika kwao kwa kuwezesha kufanikisha matakwa ya usafiri wa watu na mizigo kwa nchi hizo.

Hata hivyo, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa anasema Serikali imeamua kufanya ujenzi wa reli hiyo kwa kasi na itapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uzalishaji na kuimarisha biashara ndani ya bara la Afrika .

Kukubalika zabuni
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Profesa Norman Sigalla, anasema kuanza kwa ujenzi wa reli hiyo ni kutimiza ndoto za Rais John Magufuli za kuona Tanzania inakamilisha ujenzi wa reli ya kiwango cha kisasa.

‘‘Pamoja na kuwa inaonekana kwa wengi tumechelewa lakini kuchelewa huku ni kuzuri kwa sababu tumepiga ndege wengi kwa jiwe moja kwa kupata treni inayokwenda kasi na ya umeme na kuwashinda wenzetu wa Kenya na Ethiopia’’ alisema Sigalla.

Jambo linalotia faraja zaidi ni kauli ya Waziri Mbarawa aliyoitoa wakati wa utilianaji saini mkataba huo kuwa tayari Serikali imetangaza zabuni ya ujenzi wa reli hiyo kuanzia Morogoro hadi Makutupora kilometa 336, Makutupora hadi Tabora kilometa 294, Tabora hadi Isaka kilometa 133 na Isaka hadi Mwanza kilometa 248.

Ni faraja kwa hatua hii kufikiwa kwani inadhihirisha nia ya dhati ya Serikali iliyopo madarakani chini ya Rais Magufuli kuleta mabadiliko ya kweli na kuimarisha kiwango cha maisha ya Watanzania walio wengi.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Hawa Ghasia anasema kama mtu alikuwa anasafiri kwa saa 17 kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam kwa basi leo amepunguziwa saa 10 utaona ni kwa kiasi gani ameongeza muda wa kufanya kazi.

Moja ya mambo ambayo anayaona kuwa yamekuwa yakikwamisha maendeleo katika sekta nyingi nchini ni kuwapo kwa watendaji wanaozihujumu sekta hizo, hivyo anasisitiza kuundwa utawala madhubuti kuhakikisha reli hiyo si tu inajiendesha kibiashara bali inadumu kwa muda mrefu.

Anasema kuwa na bandari ni faida kiulinganifu, lakini haitakuwa na faida kama hakuna miundombinu itakayoifanya kushindana na nchi nyingine zenye bandari na miundombinu mizuri na gharama nafuu za usafirishaji. 


“Sasa ili tufaidike na hiyo bandari ni lazima tujenge reli na kuweka miundombinu mizuri ili kutoka kwenye ‘comparative advantage’ na kuwa ‘competitive advantage’ (faida za kiushindani) ili tupate faida ya kuwapo kwa bandari na tayari naona mwelekeo wa kufika huko. Kwa hili Serikali inapaswa kupewa pongezi na kuungwa mkono,” anasema Ghasia.Mwananchi
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: