BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WATUMISHI 9,932 WALIOFUTWA KAZI NA SERIKALI KWA KUGHUSHI VYETI, KUSHITAKIWA MAHAKAMANI

Rais John Magufuli akionesha kabrasha lenye Taarifa za Uhakiki wa Vyeti kwa Watumishi wa Umma baada ya kukabidhiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki (kulia) katika hafla iliyoenda sambamba na uzinduzi wa Sherehe za Kutimiza Miaka Kumi ya Kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), mjini Dodoma jana. Kushoto kwake ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan. (Picha na Mohamed Mambo).

RAIS John Magufuli amewafuta kazi watumishi 9,932 wa serikali waliobainika kuwa na vyeti feki na kuagiza kusitishwa mara moja mishahara yao, huku akiwataka waondoke kazini mara moja na watakaokaidi agizo hilo watashitakiwa mahakamani.


Pia ameagiza majina ya watumishi hao yatangazwe kwenye magazeti ili watu waone na wajifunze kuwa waliiibia serikali fedha kwa kukaa kwenye nafasi ambazo si zao. Kwa mujibu wa sheria, mtumishi aliyeghushi cheti anakabiliwa na kifungo cha miaka saba gerezani.

Rais Magufuli alisema hayo jana mjini hapa baada ya kupokea taarifa ya uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma sambamba na uzinduzi wa sherehe za miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Rais Magufuli alisema ni lazima watumishi hao waondoke kwenye utumishi wa umma mara moja kutokana na kuisababishia serikali hasara kubwa. “Tena naagiza mshahara wao wa mwezi huu ukatwe na waondoke kwenye utumishi wa umma, watakaokaidi watapelekwa mahakamani kwa mujibu wa sheria na nafasi hizo 9,932 zitangazwe ili wasomi waweze kuziomba.

Hao ni majambazi na wezi kama walivyo wezi wengine, hatukusema mtu kuwa na sifa ya kuajiriwa mpaka uwe na digrii lakini haiwezekani kushikilia nafasi ambayo si yako, kama umeshindwa kufikia sehemu fulani usiruke nenda kwenye elimu ya kujiendeleza utafika lakini usidanganye.

Hili ni fundisho kwa watu waliozoea kughushi, mkafute majina yao yote kwenye kompyuta, orodha ninayo waondoke wenyewe kwa hiyari kabla ya kupelekwa mahakamani.”

Aliwataka wakatafute kazi ambazo zinalingana na elimu zao. Alisema mpaka Mei 15, mwaka huu watumishi wote walioghushi vyeti wawe wameondoka kwenye utumishi wa umma na wasipoondoka vyombo vya dola wawachukulie hatua, wapelekwe mahakamani wakajibu vyeti vyao wamechapisha wapi.

Aidha alitaka watumishi 1,538 ambao vyeti vyao vina utata mpaka Mei 15, mwaka huu, hatma yao ijulikane na kama wanajijua kuwa si wahusika wa vyeti hivyo waondoke mapema.

“Hapo tutakuwa tumetengeneza ajira 12,000, si haba kwa wasomi, “ alisema. Pia alitaka waliowasilisha vyeti vya utaalamu bila kuwa na vyeti vingine wafuatiliwe. “Kuna wengine wamejiendeleza hatua kwa hatua si lazima wafike kidato cha sita, watumishi hao 11,566 waendelee kulipwa mishahara yao ila uchunguzi ufanyike,” alisema.

Alisema tayari serikali imetangaza nafasi za ajira 52,456 ukiongeza na nafasi 12,000 za watumishi wenye vyeti bandia na vyenye utata, Watanzania wengi wenye sifa wataajiriwa serikalini.

“Hatua nyingi tunazochukua si za kumkomoa mtu, kila mmoja analalamika, tunataka kuipeleka Tanzania mahali fulani tunaomba ‘sapoti’ ya Watanzania, tunafanya yale yenye manufaa kwa Watanzania.

Hatutaki kulaumu watu waliopita ila tukumbuke dhambi walizofanya tusiporekebisha tutaendelea na mfumo huo huo. Kwani hawakuwepo mawaziri, wakurugenzi ila makosa waliyofanya sisi tuone wana nafasi ya kurekebisha,” alisema.

Rais Magufuli alisema serikali imejipanga kufanya kazi hasa kwa ajili ya Watanzania wanyonge na taifa hili ni tajiri. Alisema mapato ya serikali yanayokusanywa yameongezeka ambapo awali makusanyo ya mwezi yalikuwa ni Sh bilioni 800 ambayo sasa yamefikia Sh bilioni 850 na fedha za kulipa mishahara zilikuwa ni Sh bilioni 700.

“Huwezi kuendesha nchi kwa Sh bilioni 100 na kumbe fedha nyingi zilikuwa zikienda kulipa watumishi hewa, sasa tunavuna Sh trilioni 1.3 na hatujafanikiwa sana, bado kuna maeneo mengi fedha zinaibwa,” alisema.

Rais Magufuli alisema serikali ilifanikiwa kuwaondoa watumishi hewa serikalini 19,706 ambao walikuwa wakilipwa Sh bilioni 19.8 kwa mwezi na kwa mwaka walikuwa wakilipwa Sh bilioni 238. Alisema serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwenye elimu kuanzia ya msingi hadi vyuo vikuu.

Alisema jumla ya Sh bilioni 483 zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu 124,711 kutoka wanafunzi 98,320 waliokuwa wakipata mikopo mwaka jana. Kwa upande wake Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema wenye vyeti visivyo halali lazima waondoke kwenye utumishi wa umma kwani wanapoteza nafasi za watu ambao wana sifa za kuajiriwa kwenye nafasi hizo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki alisema; “ Uhakiki huu haujafanyika kwa viongozi wa kisiasa ambao wako serikalini kama vile Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao mamlaka ya uteuzi ndio wanajua ufanisi wa kazi zao na pia katika siasa suala ni kujua kusoma na kuandika.” Waziri alisema watumishi wa umma wataajiriwa kulingana na sifa zilizoainishwa kwenye miongozo mbalimbali.

Alisema uhakiki wa vyeti uliofanyika ni wa kidato cha nne na sita na vyeti vya ualimu na diploma. Alisema uhakiki huo ulifanyika kwa watumishi wa serikali za mitaa, mashirika ya umma, wakala wa serikali, serikali kuu, wizara na idara zinazojitegemea.

Alisema kati ya vyeti 1,114 vilivyowasilishwa Baraza la Mitihani kwa uhakiki, vyeti 344 vilikuwa vikifanana na watumishi hao walichukuliwa hatua kwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Alisema matokeo ya uhakiki kundi la kwanza watumishi 376,969 sawa na asilimia 94.3 walikuwa na vyeti halali na Baraza la Mitihani limejiridhisha magamba ya vyeti yaliyohakikiwa yalitolewa na baraza hilo.

Alisema watumishi 9,932 sawa na asilimia 2.4 walibainika kuwa na vyeti vya kughushi kutokana na miundo ya vyeti vyao kutofanana na vyeti husika. Pia watumishi wenye vyeti vyenye utata vilivyohakikiwa ni 1,538 sawa na asilimia 0.3.

Waziri huyo alisema watumishi 11,566 sawa na asilimia 2.8 waliwasilisha vyeti vya utaalamu peke yake bila cheti cha kidato cha nne au cha sita na wanafuatilia kwa makini ili kujua mwisho wake. “Suala la kughushi ni kosa la jinai na hatua zitachukuliwa kwa mawakala wanaotengeneza vyeti vya kughushi.”

Alisema katika sheria za nchi adhabu za mtu anayeghushi cheti ni kifungo cha miaka mitano gerezani. Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema kumekuwa na changamoto kubwa ya kughushi vyeti vya taaluma au kutumia vyeti vya watu wengine.

Alisema mwaka 2008 ulianzishwa utaratibu wa kuweka picha kwenye vyeti na kuliongezeka maficho yanayowekwa kwenye vyeti vinavyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: