BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MWANASHERIA AFRIKA YA MASHARIKI KUFUATILIA ISHU YA TUNDU LISSU KUSHIKILIWA NA JESHI LA POLISI

 
Wakati wenzao wakisema makosa manne ndiyo yanayoweza kumlazimu mtuhumiwa kupimwa mkojo, Jumuiya ya Afrika Mashariki imesema inafuatilia sakata la mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi.

Lissu, ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alikamatwa Alhamisi akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakati akisubiri kwenda Kigali, Rwanda kuhudhuria mkutano wa jumuiya hiyo.

Wanasheria wa Lissu wamesema waliambiwa na polisi kuwa amekamatwa kwa tuhuma za uchochezi, lakini alitakiwa kutoa kipimo cha mkojo, jambo ambalo limezua maswali.

“Tutafanya mipango ya kufuatilia kesi ya Wakili Tundu pamoja na mchakato mwingine wowote wa mahakama ambao umeshafikishwa mahakamani au unaweza kufikishwa mahakamani, kwa niaba yake kuthibitisha haki za Mtanzania kama zilivyoelezwa na sheria ya kimataifa,” inasema taarifa ya Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS) iliyosainiwa na rais wake, Richard Mugisha.

Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa EALS inachukulia kukamatwa kwa Lissu kama ishara nyingine ya kuendelea kuzorota kwa uhusiano baina ya Serikali na TLS, hali iliyoanza wakati wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.

“Ni kitu kilicho wazi kuwa uhusiano huo umekuwa ukiharibika tangu kipindi cha kuelekea na baada ya matokeo ya Mkutano Mkuu wa mwaka wa TLS ambao Wakili Lissu alichaguliwa na wanasheria wenzake kuongoza TLS kwa mwaka mmoja,” anasema Mugisha.

Wakati EALS ikitoa msimamo huo, wanasheria nchini bado wanahoji sababu za Lissu kuchukuliwa kipimo cha mkojo wakati akituhumiwa kwa makosa ya uchochezi.

Kwa mujibu wa wanasheria hao, makosa yanayoweza kusababisha mtuhumiwa achukuliwe kipimo hicho ni ya usalama barabarani, matumizi ya dawa za kulevya, ubakaji na mashauri ya ndoa na watoto ambayo hulazimu mkemia kupima sampuli hizo.

Hata hivyo, katika hali iliyoibua maswali chekwa, Lissu aliyekamatwa kwa makosa ya uchochezi, juzi alipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, kwa ajili ya kupimwa mkojo.

“Watu wanaotumia dawa za kulevya wanalazimishwa na sheria kupimwa mkojo ili kuondoa shaka, lakini mtuhumiwa wa uchochezi halazimishwi kupimwa mkojo,” alisema mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse aliyeulizwa kuhusu tuhuma zinazoweza kusababisha kuchukuliwa kwa kipimo hicho.

“Mtuhumiwa anaweza kukataa kupimwa mkojo kwa amri. Polisi nao hawaruhusiwi kutumia nguvu. Wanachoweza kufanya ni kutafuta amri ya mahakama ili kumlazimisha mtuhumiwa kukubali kupima au akabiliane na kifungo kwa kukaidi amri ya mahakama.”

Maoni ya Dk Jesse yanalingana na mwanasheria mwingine, Hudson Ndusyepo ambaye alisema Sheria ya Vinasaba vya Binadamu ya mwaka 2009 imebainisha watu au mamlaka zinazoweza kutaka sampuli kutoka kwa mtuhumiwa kwa masuala ya undugu, usalama barabarani au matumizi ya mihadarati.

“Wananchi wana haki ya kukataa vipimo ambavyo vinakinzana na sheria za nchi. Ikitokea (polisi) wakatumia nguvu badala ya utaalamu, basi sheria itawaweka kwenye matatizo zaidi,” alisema Ndusyapo, “Lissu alikamatwa kwa tuhuma za uchochezi ambazo hazina uhusiano wowote na kupima mkojo kama polisi walivyotaka. Kwa hiyo, Lissu alikuwa sahihi kukataa kupima mkojo.”

Mwanasheria mwingine, Benedict Isahabakaki alisema kitaalamu, polisi walitakiwa kumweleza mtuhumiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili na kifungu cha sheria ambacho wanadhani amekivunja.

“Vipimo vya mkojo havina uhusiano wowote na makosa ya uchochezi. Tatizo ni kwamba polisi wamekuwa wakifanya kazi zao kienyeji, ndiyo maana wanawakamata watuhumiwa wengi Ijumaa wakidhani kwamba hawawezi kutoa dhamana siku za wikiendi, kitu ambacho ni makosa. Polisi wanatakiwa kufanya kazi hata wikendi,” alisema mwanasheria huyo.

Lakini Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alisema uchunguzi wa polisi hauna mipaka na kwamba jeshi hilo halifanyi kazi kwa mihemko ya watu, bali kwa kuzingatia weledi.

Alisema kitendo cha watu kuhoji suala la Lissu kupimwa mkojo ni kuingilia uchunguzi. Alisema uchunguzi ni suala pana, hivyo kuwataka wasubiri mtuhumiwa huyo atakapofikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yake.

“Kwenye suala la ku-suspect (kutuhumu), polisi anaweza ku-suspect anything (kitu chochote) kutoka kwa mtu yeyote. 


Siwezi kuelezea mikakati na mbinu za kiuchunguzi, lakini mtambue kwamba uchunguzi is too general (ni mpana), unaweza kuchunguzwa kwa mambo mengi,” alisema Mwakalukwa.Mwananchi
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: