UTAKATISHAJI FEDHA DOLA ZA MAREKANI 22.1 MIL WAMHENYESHA RUGEMALIRA SETHI, WAONGEZEWA MASHATKA SITA
Wafanyabiashara wawili, Harbinder Sethi na James Rugemalira wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa mara ya pili na kusomewa mashitaka mapya sita likiwamo la utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Kimarekani milioni 22.1 na Sh bilioni 309.4.
Na Fransisca Emmanuel.
WAFANYABIASHARA wawili, Harbinder Sethi na James Rugemalira wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa mara ya pili na kusomewa mashitaka mapya sita likiwamo la utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Kimarekani milioni 22.1 na Sh bilioni 309.4.
Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering na mmiliki mwenza wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) na Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Power African Power (T) Limited (PAP), walisomewa mashitaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Huruma Shaidi, yakifanya sasa wakabiliwe na mashitaka 12 baada ya awali kupandishwa kizimbani Juni 19, mwaka huu, ambako walikabiliwa na mashitaka sita.
Akiwasomea mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro alidai washitakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kuisababishia serikali hasara na kutakatisha fedha. Kimaro alidai kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam, walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.
Alidai katika mashitaka ya pili kati ya Oktoba 8, 2011 na Machi 19,2014 jijini Dar es Salaam, wakiwa siyo watumishi wa umma walishirikiana na watumishi wa umma kutekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.
Katika mashitaka ya tatu yanayomkabili Sethi, inadaiwa kuwa Oktoba 10, 2011 katika Mtaa wa Ohio Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai, alighushi fomu namba 14 A ya usajili wa kampuni na kuonesha kuwa yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau, Masaki wakati akijua sio kweli.
Pia Sethi anadaiwa alitoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14 A ya usajili wa kampuni kwa Ofisa Msajili wa Kampuni, Seka Kasera kwa njia ya kuonesha kwamba yeye ni Mtanzania na Mkazi wa Mtaa wa Mrikau, Masaki Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Aidha, Kimaro alidai katika mashitaka ya kujipatia fedha kwamba kati ya Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23,2014 katika Makao Makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni na Benki ya Mkombozi, Tawi la Mtakatifu Joseph, kwa ulaghai washitakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Dola za Marekani 22,198,544.60 na Shilingi za Tanzania 309, 461,300,158.27.
Pia washitakiwa wote wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ambapo inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic, Tawi la Kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198, 544.60 na Sh 309,461,300,158.27.
Kimaro alidai kati ya Novemba 29,2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam, kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni dola za Marekani milioni 22.1 na Sh bilioni 309.4 wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.
Katika mashitaka ya nane, Kimaro alidai kuwa Novemba 29, 2013 katika Tawi la Benki ya Stanbic Tanzania, Wilaya ya Kinondoni, Sethi alitakatisha fedha kwa kuchukua kutoka BOT dola za Marekani milioni 22.1 wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.
Aidha, Sethi anadaiwa kuwa kati ya Novemba 29, 2013 na Machi 14,2014 katika Tawi la Benki ya Stanbic Kinondoni, Dar es Salaam alitakatisha fedha Sh bilioni 309.4 kutoka Benki Kuu ya Tanzania wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao uhalifu.
Katika mashitaka ya 10, inadaiwa Januari 23, 2014 katika Benki ya Mkombozi, Tawi la St Joseph Cathedral, Rugemalira alitakatisha fedha ambazo ni Sh bilioni 73.5 kutoka kwa Sethi wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.
Pia inadaiwa Januari 23, 2014 katika tawi hilo la Benki ya Mkombozi, Rugemalira alitakatisha fedha ambazo ni dola za Marekani milioni 22 kutoka kwa Sethi wakati akijua fedha hizo ni zao la uhalifu.
Kimaro pia alidai Sethi anadaiwa kuwa Januari 28, 2014 katika Tawi la Benki ya Stanbic, Kinondoni alihamisha Rand za Afrika Kusini 1,305,800 kwenda kwenye akaunti namba 022655123 katika Benki ya Standard Land Rover Sandton ya Afrika Kusini wakati akijua katika kipindi anahamisha fedha hizo zimetokana na zao la kujihusha na genge la uhalifu.
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Hata hivyo, upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na washitakiwa wamerudishwa rumande hadi Julai 14, mwaka huu kwa kuwa mashitaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili washtakiwa hao hayana dhamana.Hbarileo
0 comments:
Post a Comment