BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAISLAMU WA TANZANIA WAMPATA MTUME, ANAJULIKANA KWA JINA LA NABII ILYASA


Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zubeir

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limewataka Waislamu kujiepusha na mtu anayejiita mtume na kufundisha mambo yanayopingana na Imani ya Kiislamu eneo la Kibaha Misugusugu mkoani Pwani.

Akizungumza kwa niaba ya Mufti Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Mufti, Shehe Khamis Mataka alisema Hamza Issa ndiye anayedai kushukiwa na roho ya Nabii Illyasa na kuwaaminisha watu kwenye mafundisho yake kuwa yeye ndiye Nabii Ilyasa.

“Maelekezo na mafundisho ya Uislamu yako wazi kabisa kwa kila Muislamu wa kada yeyote kwamba hakuna Mtume tena katika Uislamu baada ya Mtume Muhammad (S.A.W), na kwa hivyo upatikanaji wa mtu ndani ya Uislamu kudai kuwa yeye ni mtume ni kuamsha hisia kali za Waislamu hapa nchini,” alisema Shehe Mataka.

“Dhana ya ‘reincarnation’, yaani mtu baada ya kufa roho yake inamwingia mtu mwingine haikubaliki ndani ya Uislam. Uislam unaamini katika Ahela, kiama, kuhesabiwa na kulipwa lakini siyo roho ya mtu aliyekufa kumuingia mtu mwingine,” aliongeza Shehe Mataka.

Alisema baada ya kupokea maazimio ya Baraza la Mashehe wa Mkoa wa Pwani kuhusu taarifa za Hamza Issa kujiita mtume, Mufti Zubeir alikaa na Baraza lake la Ulamaa na kupitisha maazimio mbalimbali ikiwemo kuwaonya Waislamu kuwa yeyote atakayemfuata Hamza Issa, atakuwa ametoka ndani ya Uislamu.

Shehe Mataka alitaja maazimio mengine yaliyopitishwa na Baraza la Ulamaa ni pamoja na kuwataka mashehe wa mikoa, wilaya na maimamu, kutompa nafasi Hamza Issa ya kuzungumza misikitini wala kusikiliza CD zake ili kutoruhusu upotoshaji wake kuenea katika jamii.

Msemaji huyo wa Mufti alieleza kuwa Baraza la Ulamaa ni chombo cha kuchunga nidhamu ya dini katika Uislamu na kuongeza kuwa mafundisho yanayotolewa na Hamza Issa kuhusu kuingiwa na roho ilyomfanya kuwa mtume ni mara ya kwanza kusikika duniani kwa mujibu wa Imani ya Kiislamu.

Shehe Mataka alieleza kuwa Baraza la Ulamaa linaviomba vyombo vya dola kumkamata mtu huyo kwani akiachwa anaweza kusababisha uvunjifu wa amani kwa kuwa Uislamu haukubaliani na mafundisho yake.Habarileo
Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment