BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

Mbinu za ‘kishamba’ zitampa Lwandamina ushindi wa kwanza vs Simba

 

Na Baraka Mbolembole
KUSHINDA mechi ni jambo zuri kwa timu, lakini kushinda mechi huku ukiimarisha falsafa ya kushinda mechi kwa mbinu sahihi, ni jambo la kupendeza zaidi kwa kocha ye yote yule.

Namtazama kocha wa Yanga SC, Mzambia, George Lwandamina, kisha nafikiria ni mbinu gani hasa zinaweza kumuongoza kuishinda Simba SC kwa mara ya kwanza tangu alipochukua nafasi ya Mholland, Hans van der Pluijm, Disemba, 2016.

Lwandamina ameiongoza Yanga kushinda ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara 2016/16, lakini bado nashindwa kupima uwezo wa kocha huyo aliyeifikisha Zesco United ya Zambia katika nusu fainali ya ligi ya mabingwa Afrika msimu wa 2016 kwa kutazama kiwango cha Yanga katika baadhi ya michezo muhimu na mikubwa katika miezi yake Sita ya mwanzo klabuni hapo.

Suluhu vs Simba SC katika nusu fainali ya Mapinduzi Cup mapema Mwezi Januari huko Visiwani Zanzibar, kushindwa kuwafunga ZANACO ya Zambia katika mchezo wa kwanza kuwania kufuzu kwa makundi ligi ya mabingwa Machi mwaka huu jijini, Dar Es Salaam, kipigo cha 2-1 kutoka kwa Simba katika mchezo wa marejeano ligi kuu Bara, Machi mwaka huu.

Kufungwa 1-0 na kuondolewa katika nusu fainali ya michuano ya FA Cup vs Mbao FC na kipigo kingine kama hicho kutoka kwa Mbao katika mchezo muhimu wa mwisho katika ligi kuu na aina ya mbinu anazoendelea kutumia hivi sasa, hakika Lwandamina bado anahitaji ‘msaada’ ili kupata matokeo katika michezo mikubwa japo katika ligi kila mchezo huchukuliwa kwa uzito sawa.

Majeraha yalimuathiri wakati anaingia Yanga?

Kwanza Simba wamekuwa na bahati nzuri kwa kutokutana na mchezaji ‘mkali’ Mzimbabwe, Donald Ngoma katika michezo miwili iliyopita ya ‘Dar-Pacha’. Lwandamina anaweza kujitetea kuwa alishindwa kuifunga Simba katika mchezo wa Mapinduzi kwa sababu kikosi chake hakikuwa na Ngoma na wachezaji wengine wane muhimu katika kikosi chake cha kwanza.

Pia anaweza kuchukulia sababu hiyo na kuitumia kama Ngao ya kujinga katika mlolongo wa matokeo mabaya katika michezo muhimu niliyoitaja.

Aliipokea Yanga ikiwa na matatizo ‘lukuki’, wachezaji kufanya migomo baridi kwa kile ambacho kilisemwa kutofurahishwa na uamuzi wa klabu kumuondoa mwalimu Hans. Matatizo ya mishahara ya wachezaji, na majeraha ya wachezaji wake muhimu yaliisumbua sana Yanga kati ya mwezi Januari hadi Mei mwaka huu.

Kama mambo hayo muhimu yanakuwa sivyo ndivyo klabuni ni rahisi kuvuruga mbinu za kocha na utimamu wa mwili na akili kwa wachezaji . Haya yote ni sababu tu ambazo zinaweza kuendelea kumlinda Lwandamina lakini bado sikupendezwa na mbinu zake kiuchezaji ambazo zilitegemea uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na si timu kucheza na kupata matokeo kama timu.

Sasa…

Lwandamina anakwenda kucheza kwa mara ya tatu vs Simba na wakati huu ana washambuliaji wake wote mahiri. Mrundi, Amis Tambwe,Ngoma, Mzambia, Obrey Chirwa huku kuondoka kwa Saimon Msuva aliyefunga magoli 14 kukimkaribisha kikosini Ibrahim Ajib aliyeifungia Simba magoli yasiyopungua sita msimu uliopita.

Kuondoka kwa Mnyarwanda Haruna Niyonzima kunaweza kuwa nafasi kwa sajili mpya za Pius Buswita na Rafael Daud kuchukua nafasi ya kuichezesha timu wakati katikati ya uwanja wakitaraji huduma ya ‘nahodha asiyevaa beji’ Mzimbabwe, Thaban Kamusoko na kiungo mpya raia wa DR Congo, Papy Tshishimbi ambaye alionesha kiwango kizuri jana Jumapili katika mchezo wa kirafiki vs Jamhuri ya Pemba.

Lwandamina amepata nyongeza na mlinzi mwenye nguvu na uwezo wa kuzuia zaidi Gadiel Michael katika beki ya kushoto, huku Juma Abdul na Hassan Kessy wote wakiwa timamu kimwili na kiakili katika beki ya kulia na ni hivyo pia kwa wazoefu, Kelvin Yondan na nahodha wa kikosi Nadir Haroub katika beki ya kati.

Kwa namna hali ilivyo kuelekea mchezo wa Jumatano hii ni wazi, Lwandamina ataingia kuwakabiri Simba kwa mara ya tatu lakini safari hii akiwa na kikosi kisicho na majeraha, migomo huku kila mchezaji akionekana kuwa timamu kimwili na kiakili katika kila idara.

Atumie mbinu za ‘kijinga’ atawapiga Simba kwa mara ya kwanza

Kwanza anapaswa kumtambua mchezaji wake wa hatari katika mashambulizi na ‘kumkabidhi mechi’ Wakati Simba ikiwa na Abdi Banda na Novaty Lufunga katika ngome, Ngoma alipasua vizuri. Na mipango ya Hans wakati ule ilikwenda sahihi kwa sababu alimkabidhi mechi ya ‘Dar-Pacha’ Ngoma kwa kutambua mchezaji huyo ni mwenye nguvu, kasi, uwezo wa kumiliki mpira na kukimbia nao, kupiga chenga na mbinu binafsi za kusaka mikwaju ya faulo.

Lwandamina hapaswi kuwa muoga tena vs Simba. Ngoma aliweza kutumia kasi ndogo ya Banda na Lufunga kuisaidia Yanga kila alipocheza vs Simba na baada ya kukosekana katika michezo miwili iliyopita namuona Mzimbabwe huyu akimgeuza SalimMbonde kuwa ‘uchochoro’ kama tu Lwandamina atawapanga washambuliaji wake watatu wa kulipwa kuanza mchezo.

Chirwa ni mjanja sana, wakati Fulani asipokuwa na mpira huonekana mchezaji asiye na kasi, lakini ukweli mchezaji huyo wa Zamabia anaweza kusababisha mikwaju ya penalty, kupiga pasi nzuri na mwisho na kufunga yeye mwenyewe akitokea upande wa kulia. Ili kuimaliza Simba ni lazima kwanza Yanga iendelee kutumia safu yake ya mashambulizi kama mbinu ya kwanza katika kujilinda.

Na kuwapanga, Chirwa akishambulia kutokea upande wa kulia, Ngoma upande wa kushoto, na Tambwe akicheza kama mshambulizi wa kati itakuwa mbinu nzuri sana kwa Yanga nah ii itawasaidia wachezaji wao wa kati kuzunguka kwa umakini wakizuia njia za viungo wa Simba ambao kwa namna inavyoonekana kocha wao Joseph Omog atapanga kikosi ambacho hakitakuwa na balansi nzuri katika kushambulia na kuzuia nah ii itawapa wakati mgumu walinzi wa Simba ambao watatu kati ya wane hawana kasi.

Kuwatumia washambuliaji watatu katika mbinu ya kuzuia na kushambulia inaweza kuonekana ‘mbinu ya kijinga’ lakini wakati mwingine hutoa matunda bora. 


Lwandamina anaweza kubebwa na wachezaji wake sita wa kigeni ambao kwa hakina wanastahili kuanza vs Simba Jumatano hii, lakini kushinda mechi itategemea na ujasiri wa mwalimu huyo anayependelea kuichezesha timu yake kwa kujilinda zaidi.

Li kushinda katika falsafa yako ni lazima wakati mwingine kocha kutumia ‘ushamba wa kiufundi’ dhidi ya mpinzani wako ndiyo maana tumeshuhudia Totenham ikichapwa isivyotarajiwa na Chelsea jana Jumapili katika ligi kuu England hii ni kwa sababu kocha Antonio Conte alitumia ‘ufundi wa kishamba’ kuishinda timu iliyokuwa timamu kimwili na kiakili zaidi yao.Chanzo/shaffihdauda.co.tz
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: