BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KIMOSA ABEBA MBUZI MNYAMA KIULAINI MASHINDANO YA DRAFTI YA MATESSA CUP MORO


Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Milikiel Manswet wa pili kutoka kushoto na Diwani wa kata ya Uwanja wa Taifa, Rashidi Matessa wa pili kutoka kulia wakiwa kwenye picha ya pamoja na bingwa wa drafti kata hiyo, Kimosa Rashid (aliyeshika mbuzi), Juma Seleman nafasi ya pili (aliyeshika kuku) na Ally Mohamed aliyeshika mfuko wenye mchele kilo tano baada ya kushika nafasi ya tatu. Picha na Juma Mtanda.

Juma Mtanda, Morogoro
Kimosa Rashidi ameibuka bingwa katika mashindano ya drafti ya Matessa Cup 2017 na kutwaa zawadi ya mbuzi mnyama baada ya kumsambaratisha mpinzani, Juma Seleman kwa kumtandika bao 1-0 katika mchezo mkali wa fainali uliopigwa kwenye klabu ya drafti ya Mawenzi Manispaaa ya Morogoro.

Akizungumza mara baada ya kutwaa ubingwa huo, Kimosa alisema kuwa haikuwa kazi rahisi kwa yeye kuibuka kidedea kutokana na ushindani aliokumbana nao kutoka kwa wapinzani wake.

Kimosa alisema kuwa alipata upinzani mkali katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Ally Mohamed (Dogo Ally) aliyemshinda kwa bao 1-0 na kutinga fainali iliyomwezesha kutwaa ubingwa baada ya kumkung’uta Juma Seleman kwa bao 1-0.

Ally Mohamed alikabidhiwa mchele kilo 5 kwa kuibuka mshindi wa tatu huku Juma Seleman alitwaa jogoo kwa kushika nafasi ya pili.

Akikabidhi zawadi kwa washindi, Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Milikiel Manswet alisema kuwa michezo imekuwa sehemu ya kukutanisha vijana wengi na wanaweza kujadiliana njia mbalimbali za kujikwamua na maisha ikiwemo kuweka mipango ya kuanzisha vikundi vya ujasiliamali.

Milikiel alisema kuwa halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kila mwaka imekuwa ikitenga fedha asilimia 5% kwa ajili ya kuwakopesha vijana kupitia kwenye vikundi vilivyosajiliwa pamoja na wanake ndani ya kata zao.

“Nimependa haya mashindano ya Matessa Cup kwani yanaweza kutumika kama sehemu ya kuweka mikakati kwa vijana kutengeneza wazo la kuanzisha vikundi ili viweze kunufaika na mikopo nafuu inayotolewa na Manispaa yetu ili kupunguza wimbi kubwa la vijana kutokuwa na ajira.”alisema Milikiel.

Kwa upande wa Diwani wa kata ya Uwanja wa Taifa, Rashidi Matessa alisema kuwa mashindano hayo yamefungua njia kwa vijana si katika kushindana tu na kugombea zawadi bali yametoa mwanga wa kuanzisha vikundi vya wajasiliamali.

Matessa alisema kuwa baada ya kumalizika kwa mashindano hayo sasa yataandaliwa mashindano mengine makubwa kwa kushirikisha wacheza wa klabu za drafti za kata mbalimbali lengo kukutanisha vijana ili kujadili fursa za kimaendeleo.

“Mashindano hayo yametupa funzo sisi kama viongozi za kuweza kuwasaidia vijana katika kukabiliana na changamoto za kimaisha ikiwemo kuwawekea mikakati ya kuwashawishi kuunda vikundi ili iwe rahisi kupata mikopo yenye riba nafuu na kujikwamua kiuchumi.”alisema Matessa

Msimamizi wa mashindano hayo, Omari Kizaba alisema kuwa mashindano hayo yalikuwa na msisimuko na ushindano wa hali hali ya juu hasa katika hatua ya 16 bora hadi kufikia fainali ikiwa imeshirikisha jumla ya wachezaji 42.

Kizaba alisema kuwa katika mchezo wa nusu fainali Kimosa Rashid alimtoa Ally Mohamed kwa bao 1-0 huku Juma Seleman alipenya kwa njia ya kurusha shilingi na kutinga fainali dhidi ya Said Mwarabu baada ya sare ya bao 2-2 kufuatia kutoshana nguvu katika michezo 10 wakati mshindi wa tatu Ally Mohamed (Dogo Ally) alimshinda Said Mwarabu bao 2-1.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: