BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

Mbowe ataka matukio ya kikatili yadhibitiwe

Waombolezaji wakiweka kaburini Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Diwani wa kata ya Namwawala wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Godfrey Luena wakati wa mazishi yaliofanyika jana.Godfrey alizikwa katika kijiji cha Namwawala. Picha na Juma Mtanda.

Na Juma Mtanda, Morogoro.
Kilombero. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema Tanzania haitakuwa salama kama haki haitatendeka kwa Serikali kutafuta ufumbuzi na kudhibiti matukio ya watu kuuawa kikatili.

Akizungumza jana wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Diwani wa Namwawala wilayani Kilombero, Godfrey Luena aliyeuawa Februari 22 kwa kukatwa mapanga, Mbowe alisema Watanzania wasikubali kuingia katika uadui wa kisiasa.

Mbowe alisema matukio yanayotokea sasa ya mauaji yanatia shaka na Serikali isipoyadhibiti itasababisha wananchi wanaopotelewa na ndugu kukaa na manung’uniko.

Alimuomba Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunyo aliyehudhuria mazishi hayo kuwatuliza vijana wenye jazba kuhusu matukio yanayoendelea nchini. 


Mkuu wa Wilaya, Ihunyo aliposimama kuzungumza alisema wameshaunda timu maalumu kuwasaka waliohusika na tukio hilo.

Awali, Mbowe alisema matukio ya mauaji ya kikatili dhidi ya viongozi wa Chadema hayatairudisha nyuma badala yake wataendelea kuimarika.

Alisema kwa kuwa Polisi imetoa tamko kuwa kushambuliwa Luena kunatokana na kisasi, hivyo inawajua watuhumiwa, ana imani watakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya dola.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema ndani ya mwezi mmoja chama hicho kimepoteza viongozi wawili katika matukio yanayofanana.

Alimtaja mwingine kuwa ni Katibu wa Chadema Kata ya Hananasif jijini Dar es Salaam, Daniel John ambaye mwili wake uliokotwa katika ufukwe wa Coco. 


Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na wabunge wa Kilombero Peter Lijuakali, Susan Kiwanga wa Mlimba, Mbunge wa jimbo la Mikumi, Joseph Haule (Prof Jay) na Devotha Minja wa Viti Maalumu.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: