BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

INZI WAHARIBIFU WA MATUNDA KUAWA


Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe

WATAFITI wa mazao ya kilimo hususani mazao ya matunda wamebuni njia mbadala itakayotumika kwa ajili ya kuwaua inzi waharibifu wa matunda yakiwamo maembe, machungwa, mapera, ndizi na maparachichi kwa kutumia nafasi zao za mapenzi.

Hayo yalifahamika jana ndani ya Ukumbi wa Bunge ambapo Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe alisema kuwa katika mtego huo, wataalamu wamegundua kemikali itakayotolewa na inzi jike kwa ajili ya kuvutia madume ili yaweze kushiriki tendo la kuzaliana.

Waziri alisema kuwa katika mtego huo ambapo utawekwa ulimbo wa kuwanasa madume ya inzi kutakuwa na vivutio vya kikemikali ambapo vitasaidia kupunguza mazalia ya wadudu hao na kupungua kwa uharibifu wa matunda katika maeneo mbalimbali.

Alikuwa akijibu swali la Riziki Omar Juma (Viti Maalum-CUF) aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani madhubuti wa kupambana na inzi waharibifu wa matunda ikiwa ni pamoja na kuanzisha maabara ya kutafiti kwa kina juu ya namna bora ya kupambana na wadudu hao.

Waziri alisema katika mwaka wa fedha 2010/11 jumla ya lita 260 za kemikali ya dawa hiyo ilisambazwa na kuanza kutumika ambapo zilionyesha mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya wadudu hao.

Mbinu nyingine ni pamoja na utafiti uliogundua kuwa wadudu aina ya nyigu ambao ni adui mkubwa wa inzi anafaa kwa kazi hiyo pia na hivyo wataalamu kulazimika kuwaleta manyigu 30,000 kutoka Shirika la utafiti la ICIPE ili wazaliane kwa wingi na kusambazwa kote nchini kwa ajili ya kuwadhibiti wadudu waharibifu wa matunda ambapo majaribio ya awali yalifanywa katika Wilaya ya Mkuranga na kuonyesha mafanikio makubwa.

Juhudi nyingine ni kutolewa kwa mafunzo ya namna ya kudhibiti wadudu hao ambapo wataalamu wa kilimo 116 wakiwamo maofisa 88, wakaguzi wa mazao 22 na maofisa wa maabara sita walipatiwa mafunzo hayo na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Chakula (FAO) ambalo tayari limechapisha na kusambaza vipeperushi 6,000, mabango 3,000 na nakala 100 za kijitabu chenye maelezo ya kuwatambua na kuwadhibiti wadudu hao.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: