BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

Mbunge afariki dunia:Vilio, simanzi nzito bungeni


Waandishi Wetu
VILIO na simanzi vilitawala bungeni jana mara baada ya Spika, Anne Makinda kutangaza kifo cha Mbunge, Mussa Khamis Silima, (Baraza la Wawakilishi - CCM, ambaye alikuwa amelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), baada ya kupata ajali juzi nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma.

Spika Makinda aliwatangazia wabunge kuhusu tukio hilo la kuhuzunisha akisema, Silima alifariki jana mchana hivyo kutumia kanuni ya 149 kuahirisha Bunge hadi leo saa 3:00 asubuhi.

“Waheshimiwa Wabunge, jana asubuhi niliwatangazia kuwa, Mheshimiwa Silima alipata ajali na mkewe aitwaye Mwanaheri, kwa bahati mbaya mkewe akafariki dunia kutokana na ajali hiyo. Silima na dereva wake waliumia wakapelekwa Muhimbili kwa matibabu zaidi na leo asubuhi niliongea naye akasema anaendelea vizuri," alisema Makinda na kuongeza:

"Lakini, nasikitika kuwaambia kuwa muda mfupi uliopita nilipata taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwamba Mheshimiwa Silima amefariki dunia. Kwa maana hiyo, kwa kutumia Kanuni ya 149 naahirisha kikao cha Bunge hadi kesho asubuhi."

Nje ya ukumbi wa Bunge, wabunge walikuwa wamekusanyika katika vikundi mazungumzo makubwa yakiwa juu ya msiba huo.

Spika kuongoza ujumbe wa watu 60

Jana, jioni Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alitoa ratiba ya mazishi ya mbunge huyo na kusema Bunge litawakilishwa na ujumbe wa watu 60 watakaoongozwa na Spika Makinda.

Joel alisema katika ujumbe huo, watakuwamo wenyeviti wote wa kamati, wajumbe wa Tume ya Bunge, wajumbe kutoka Kamati ya Nishati na Madini ambayo marehemu alikuwa ni mjumbe wake na kwamba mazishi hayo yanatarajiwa kufanyika leo saa 7:00 mchana.

Alisema ujumbe huo unatarajiwa kuondoka leo saa 4:00 kwa ndege kuelekea Zanzibar kwa ajili ya mazishi hayo.

Watoto wa marehemu wazungumza

Akizungumzia msiba huo, mtoto wa kwanza wa marehemu, Thani Mussa Hamis alisema hakuonana na baba yake hadi mauti yalipomkuta ingawa alizungumza naye kwa simu na kumtaka amletee vitu kadhaa.

“Sikupata muda wa kuzungumza naye, lakini asubuhi ya saa 12 leo (jana) nilizungumza naye kwa simu na alinieleza kuwa hali yake ni nzuri huku akinitaka nimletee vitu vyake kadhaa (hakuvitaja) nilivitafuta na nilipovipata nikaja navyo hospitalini lakini hata hivyo, nilikuta hali yake ikiwa imebadilika.”

“Sikujua ilikuwa kimetokea nini kwani nilipofika na kutaka kumuona baba walinitaka nisubiri kwanza na nilipokuwa nasubiri niliwaona madaktari wakiwa wanahangaika huku na kule na mara alikuwa akilalamika kukosa hewa hivyo wakamvalisha mipira ya hewa na kumhamishia chumba cha wagonjwa mahututi,’’ alisema.

Thani alisema baada ya muda daktari alitoka na kumweleza kuwa amefariki.

“Inauma sana... juzi nililia sana kwa ajili ya kifo cha mama yangu, leo tena baba pia nalia lakini hakuna namna ni mipango ya Mungu hivyo tumuombee ampumzishe kwa amani huko alipo,’’ alisema Thani

Mtoto wa nne wa marehemu, Mussa Hamis Suleiman alisema kifo hicho kimewaacha katika masikitiko makubwa kwa kuwa walikuwa wanamtegemea kwa ushauri na mambo mengine.

Marehemu ameacha watoto watano, wawili wa kike na wengine wa kiume.

Wabunge wamlilia
Baadhi ya wabunge walizungumzia kifo hicho cha ghafla wakisema watakosa hekima na busara zake katika masuala mbalimbali ya uendeshaji wa Bunge, huku Kamati ya Nishati na Madini ambako alikuwa mjumbe wakisema kuwa "Tumepoteza mzazi katika kamati yetu."

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, January Makamba alisema Silima alikuwa mtu aliyewaunganisha wabunge hata pale palipotokea tofauti za mawazo na kusigana miongoni mwao.

"Alikuwa mpatanishi, mara nyingi mimi nilikuwa nampa nafasi ya mwisho wakati wa kuchangia maana hakuwa na utamaduni wa kuzungumza sana na mara zote nilipompa nafasi alitoa kauli ya hitimisho ambayo ilikuwa mwafaka kwa wabunge wote," alisema January na kuongeza:

"Yeye na Mheshimiwa Mariam Kisangi tuliwaona kama wazazi wetu, yeye (Silima) tulimwita baba wa kamati na Kisangi tunamwita mama wa Kamati kwa maana kwamba ni watu wazima kiumri kuliko wengi wetu kwenye kamati yetu lakini pia walitushauri mambo mengi."

Kauli ya January aliungwa mkono na Kisangi pamoja na Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage ambao walisema kwa nyakati tofauti kwamba mbunge huyo alikuwa mpatanishi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema Baraza la Wawakilishi, Bunge na Watanzania kwa ujumla wamepoteza mzalendo ambaye alikuwa muhimu sana kwa taifa.

"Alikuwa hana bias (upande), ulikuwa ukipata ushauri wake unauchukua asilimia 100 kwa sababu hakuwa na ushabiki wa aina yoyote, kwa msimamo wake wa wazi na umri wake, amekuwa msaada sana kwa chama chetu (CCM), kwa wabunge wa Zanzibar lakini pia kwa Bunge letu," alisema Lukuvi.

Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed alisema wananchi wa Uzini alikokuwa Mwakilishi wamepata pigo kubwa na amewaachia wabunge wa Zanzibar pengo kubwa.

"Ni msiba mkubwa, naweza kusema Mheshimiwa Silima alikuwa na uhusiano mwema na kila mmoja wetu, busara zake zilitufaa sana na alikuwa mtu wa watu, kweli tumepata pigo kubwa lakini hiyo ndiyo njia yetu sote," alisema Hamad.

Mbunge wa Busanda (CCM) Lolencia Bukwimba alisema atamkumbuka kama kiongozi mwema:
“Mara nyingi pia nilimwona akiwa kiunganishi cha wabunge wa Zanzibar, wengi walikuwa wakimfuata kuzungumza naye," alisema Bukwimba.

Ajali ilivyotokea

Silima na mkewe, Mwanaheri walipata ajali juzi katika eneo la Nzuguni nje kidogo ya Mji wa Dodoma walipokuwa wakirejea kutoka Zanzibar ambako walikwenda kuhudhuria msiba wa kaka wa mkewe.

Mwili wa Mwanaheri ulisafirishwa kwenda Zanzibar na kuzikwa juzi, huku Silima na dereva wake, Chizali Sembonga walisafirishwa kwa ndege ya kukodi kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam ambako walilazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa ajili ya matibabu.
Dereva huyo anaelezwa kwamba anaendelea vyema na amelazwa katika wodi maalumu Mwaisela.

Historia yake
Hadi alipofariki dunia, Silima alikuwa Mbunge akiwakilisha Baraza la Wawakilishi, Mwakilishi wa Jimbo la Uzini na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM (Tanzania Visiwani), nafasi alizozipata mwaka jana.

Alisoma katika Shule ya Msingi Mkwajuni Zanzibar (1961- 1968) na baadaye kujiunga na elimu ya sekondari katika Shule ya Uzini (1969 - 1970) kabla ya kuhamia katika Shule ya Sekondari ya Karume ambako alisoma 1971 - 1972.

Baadaye Silima alipata mafunzo ya ualimu wa ngazi ya stashahada katika Chuo cha Ualimu cha Nkurumah (1981- 1983) na baadaye kufundisha katika shule mbalimbali visiwani Zanzibar akiwa mwalimu wa kawaida (1973 - 1988) na baadaye mkuu katika shule mbalimbali (1988 - 1996).

Kabla ya kuingia kwenye siasa, Silima aliwahi kufanya kazi katika Ofisi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (2001 - 2010), Mratibu wa Masuala ya Wanafunzi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (1996 - 2001).

Bunge kuendelea

Kuhusu ratiba ya Bunge, Joel alisema ratiba itabaki kama ilivyo lakini akaongeza kwamba semina ya wabunge kuhusu Muswada wa Sheria ya Kuundwa kwa Katiba mpya ambayo ilikuwa ifanyike Jumamosi, haitafanyika kwani Bunge litaahirishwa Ijumaa jioni kwa hotuba ya Waziri Mkuu.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, leo mjadala wa hotuba ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji itaendelea na kumalizika jioni wakati keshokutwa Alhamisi itawasilishwa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Fedha na Uchumi ambayo itahitimishwa Ijumaa mchana kabla ya Waziri Mkuu kuahirisha Bunge jioni.

HABARI HII IMEANDALIWA KWA PAMOJA NA WAANDISHI WA GAZETI LA MWANANCHI NEVILLE MEENA, DODOMA NA BONIFACE MEENA, FESTO POLEA NA AIDAM MHANDO DAR ES SALAAM.

Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: