TIMU za Simba na Toto African zimeendelea kunga'ra kileleni katika Ligi Kuu, huku mabingwa watetezi Yanga wakiendelea kuchechemea katika ligi hiyo.Simba ilipaa hadi kileleni baada ya kupata ushindi wa bao1-0 dhidi ya Coastal Union, bao lililofungwa na Patrick Mafisango, Toto nao wameendelea kung'ang'ania kileleni baada ya kuibwaga JKT Ruvu kwa bao 1-0.
Hali imeendelea kuwa tete kwa mabingwa Yanga baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Moro United timu iliyopanda daraja msimu huu.Baada ya matokeo hayo basi lililowabeba wachezaji wa Yanga lililazimika kuondolewa uwanjani hapo kwa kusindikizwa na magari ya polisi.
Yanga walilazimika kusubiri hadi kipindi cha pili kupata bao la kuongoza katika dakika ya 68 kupitia kwa Niyonzima aliyeunganisha vizuri krosi ya Shadrack Nsajigwa.
Shangwe za mashabiki wa Yanga zilizimika katika dakika ya 87, baada ya Jerome Lambele kufunga bao la kusawazisha kwa Moro United akiunganisha krosi ya Bakario Mpakala aliyeingia kuchukua nafasi ya Benedict Ngasa.
Yanga ilianza mchezo huo kwa kasi na kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Moro United, lakini ngome ya Moro ilikuwa imara kuokoa hatari zote.
Kiungo Nurdin Bakari alikosa bao la wazi katika dakika ya 15, baada ya kupokea pasi ya Hamisi Kiiza, lakini alipiga shuti hafifu lililodakwa na kipa wa Moro United, Lucheke Mussa.Katika dakika ya 20, Kiiza alikosa bao akiwa ndani ya eneo la hatari baada ya kupata pasi kutoka kwa Haruna Niyonzima, lakini shuti lake lilipaa juu.
Kocha Sam Timbe akizungumza baada ya mechi hiyo alisema hivi sasa Yanga inakazi kubwa kufikia mafanikio yake kwa sababu wachezaji wengi wameshindwa kucheza kwa kiwango chao tangu walipofungwa na Simba na JKT Ruvu.
Naye Hassan Banyai wa Moro United alisema mchezo ulikuwa mgumu kwao, lakini amefarijika kwa matokeo hayo ya sare na sasa anawaza mechi yake ijayo dhidi ya Toto.
Tanga: Simba iliendeleza rekodi yake ya ushindi katika mechi ya pili katika ligi baada ya Mafisango kufunga bao la kuongoza katika dakika ya 24 kwa shuti la mguu wa kushoto akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Amir Maftah.
Katika mchezo huo uliojaa mashabiki wengi kwenye Uwanja wa Mkwakwani ulishuhudia Simba ikiendeleza ubabe wake dhidi ya Coastal Union yenye pointi moja.
Mwanzoni mwa mchezo huo mshambuliaji wa Simba, Gervais Kago aliifungia Simba bao katika dakika ya 5, lakini mwamuzi Thomas Mkomboza alilikataa bao hilo kwa madai mchezaji mwingine wa Simba, Mafisango alikuwa ameotea.
Kipindi cha pili Coastal waliamka kujaribu kutafuta bao la kusawazisha na katika dakika ya 65, Mbwana Hamis alikosa bao baada ya mpira wake wa adhabu kupaa kidogo nje ya goli. Tukio hilo lilitokea baada ya Maftah kumchezea vibaya Mandawa Rashid nje kidogo ya eneo la penalti.
Dodoma: Polisi Dodoma walijikuta wakipata taabu baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na JKT Ruvu kwenye uwanja wa Jamhuri.
Ruvu ilipata bao la kuongoza dakika ya 7, kupitia kwa Rajab Chau, lakini Polisi walisawazisha kupitia Hamad Kambangwa dakika ya 15 na kupata bao la kuongoza kupitia Bryton Mponzi katika dakika ya 37.
JKT Ruvu walianza vizuri kipindi cha pili kwa kishindo na kusawazisha bao kupitia Jimmy Shoji.
Mwanza: Wenyeji Toto Afrika waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting bao lililofungwa na Emmanuel Swita kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 63 kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Kagera Sugar ikiwa kwenye uwanja wake wa Kaitaba ilishindwa kutamba baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Villa Squad.
Wenyeji Kagera walipata bao la kuongoza katika dakika ya 35 kupitia kwa Temmy Felix, kabla ya Villa Squad kusawazisha bao hilo katika dakika ya 90 kupitia kwa Zubery Daby, pia katika mechi hiyo Sunday Frank wa Kagera alionyeshwa kadi nyekundu kwa mchezo mbaya.
Arusha; Oljoro JKT walijirekebisha baada ya kipigo cha kwanza kutoka kwa Simba na kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0, bao lililofungwa na Rashid Joshua.Timu ya Oljoro ilikuwa ikishangiliwa kwa nguvu na wanajeshi wenzao waliojitokeza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Imeandaliwa na Burhani Yakubu (Tanga), Juma Mtanda (Morogoro), Mussa Juma (Arusha) William Paul (Kagera) Masoud Masasi (Dodoma).
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment