Umoja wa Mataifa washambuliwa Nigeria
Kikundi cha waislamu wenye msimamo mkali nchini Nigeria - Boko Haram - kimedai kuhusika na shambulio dhidi ya makao makuu ya Umoja wa mataifa katika jiji la Abuja.
Msemaji wa kundi hilo alitoa madai hayo alipoongea kwa simu na afisi za BBC nchini Nigeria.
Kikundi hicho kilifanya mashambulio kama hayo dhidi ya makao makuu ya polisi mjini Abuja mwezi Juni mwaka huu.
Mkuu wa polisi wa Abuja Mike Zuokumor aliwaambia waandishi wa habari kwamba mshambuliaji aliyejitoa mhanga alifariki dunia papo hapo kwani mlipuko huo ulimkata vipande vipande.
Umoja wa Mataifa umesema kumekuwa na shambulio la bomu katika jengo la Umoja wa Mataifa nchini katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja.
Abuja
Mlipuko mjini Abuja
Mwandishi wa BBC Bashir Sa'ad Abdullahi ambaye yupo katika eneo la mlipuko amesema ghorofa ya chini ya jengo hilo imeharibika sana.
Huduma za dharura zinaondoa miili ya watu kutoka katika jengo hilo huku majeruhi wengine wakipelekwa hospitali, anasema mwandishi wetu.
Makundi ya wanamgambo wa Kiislam wamekuwa wakifanya mashambulio katika jiji hilo katika siku za hivi karibuni.
Magaidi
Bomu la kutegwa ndani ya gari lililipuka katika kituo cha polisi mwezi Juni na kulaimiwa kundi la Boko Haram, kundi ambalo linataka Nigeria kuanzisha matumizi ya sheria za Kiislam, Sharia.
Kwa mujibu wa walioshuhudia shambulio hilo- gari moja lilivamia eneo la kuingilia la ua wa makao hayo ya umoja wa mataifa likivunja mageti mawili tofauti huku walinzi wakijaribu kulisimamisha.
Walisema dereva wa gari hilo aliliendesha hadi sehemu ya mapokezi kabla ya kulilipua na kusababisha uharibifu mkubwa kila mahali.
Madirisha ya jengo la Umoja wa mataifa yalivunjwa na vipande vya vioo vilitawanyika kila mahali.
Kulikuwa na matone ya damu katika sehemu za kupitia watu na pia katika bustani na wanasema waliona miili ya watu iliotawanyika kila mahali.
Moshi
Shambulio la siku ya Ijumaa limefanyika takriban saa 5 asubuhi saa za Nigeria, katika eneo la kibalozi, katikati ya jiji la Lagos, karibu na ubalozi wa Marekani.
Kulikuwa na mlipuko mkubwa na moshi kutanda ukitoka ndani ya jengo.
"Niliona miili imetapakaa," Michael Ofilaje, mfanyakazi wa Unicef anayefanya kazi katika jengo hilo amesema, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.
"Watu wengi wamekufa."
Amesema alihisi kama "mlipuko huo umetokea chini ya jengo na kutikisa jengo zima".
Polisi wamefunga eneo hilo la tukio.
"Tumepeleka polisi wetu na kundi la wataalam wa mabomu. Hatuwezi kusema watu wangapi wamekufa," amesema msemaji wa polisi wa Abuja, kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press.
0 comments:
Post a Comment