BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

Mbunge mwingine CCM afikishwa mahakamani


Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla,

MBUNGE wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla, amekamatwa na kuswekwa rumande kisha kufikishwa mahakamani jana kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko usiokuwa halali.

Habari zimeeleza kuwa mbunge huyo alikamatwa juzi jioni na kuwekwa mahabusu ya polisi katika Kituo cha Nzega ambako alilala hadi jana asubuhi alipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Nzega kujibu tuhuma hizo.

Alikamatwa pamoja na watu wengine watatu, Mrisho Hamisi, Mathew Dotto na Mwanja Mwandu, wote wakiwa wakazi wa kata ya Nata ambao ni wachimbaji wadogo, waliodaiwa kushiriki vurugu zilizotokea juzi katika kijiji cha Mwabangu.

Wakisomewa mashtaka yao jana mbele ya hakimu Ajali Mlanzi waendesha mashtaka wa polisi, Merito Ukingoji na Joseph Mbwana, walisema kwa pamoja watuhumiwa hao wanashtakiwa kwa kufanya mkusanyiko usio halali Oktoba 23 mwaka huu, katika mgodi mdogo wa wachimbaji wadogo uliopo kijijini hapo.

Waendesha mashtaka hao waliieleza mahakama kuwa mbali na kufanya mkusanyiko usiokuwa wa halali, watuhumiwa hao pia, waliingia katika mgodi huo mdogo unaomilikiwa na wawekezaji bila idhini ya wamiliki na kuvamia Kituo cha Polisi cha Nzega.

Waendesha mashitaka hao, walisema washtakiwa hao pia wanatuhumiwa kufanya njama katika ofisi ya wilaya ya CCM na kufanya maandamano kisha kuvamia kituo cha polisi.

Dk Kigwangalla na Mwandu pia wanakabiliwa na shitaka la kupiga na kujeruhi. Waendesha mashtaka hao waliwataja waliopigwa katika tukio hilo kuwa ni Moses Kichambi na Ferdinald Yusuph.

Hata hivyo watuhumiwa wote wanne walikana shtaka na wako nje kwa dhamana baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa bado unahitaji muda kuendelea na upepelezi wa tukio hilo.

Mbali na hakimu Mlanzi kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 18 mwaka huu, amemzuia mbunge huyo kufika katika eneo la mgodi huo ili kuondoa uwekezakano wa kutokea kwa machafuko mapya.

"Mahakama inatambua kuwa ni wewe (Kigwangalla) ni mbunge wa jimbo na unapaswa kutembelea wananchi wako lakini kwa sababu suala hilo sasa liko mahakamani, hutakiwi kufika kwenye eneo la mgodi huo," alisema hakimu Mlanzi.

Adai rumande imemdhalilisha

Dk Kigwangalla aliliambia gazeti hili nje ya mahakama kuwa hakujua kama angehusishwa kwenye kesi hiyo na kuswekwa rumande kwani alifika kituoni hapo kwa nia ya kuwadhamini wenzake.

Dk Kigwangalla alisema kuwa baada ya kuwatuliza wananchi ambao walikuwa wakielekea kwenye Kituo cha Polisi Nzega Mjini, aliwaweka kchini katika ofisi ya CCM wilaya na kuwataka wamsubiri aende kuwawekea dhamana wenzake waliokamatwa.

"Tulipokuwa tunaelekea kituoni, askari wakawa wanazungumza kwa jazba na kusema mimi ndiye niliyeanzisha vurugu na nilipofika kituoni ghafla nikaambiwa nivue viatu na kuelezwa nitalala rumande," alisema Dk Kigwangalla.

"Leo (jana) wamenitoa rumande na kunipeleka mahakamani nikiwa nimefungwa pingu na watu wengine niliokuwa nimeenda kuwadhamini," alisema Dk Kigwangalla.

"Nilikataa kutoa maelezo nilipokuwa kituoni lakini (leo) jana nilipelekwa Mahakamani na kufunguliwa mashtaka kama nane hivi, moja likiwa kujeruhi na mengine ya jinai," alisema Dk Kigwangalla.

Dk Kigwangalla alilalamika "Nimedhalilishwa sana na hawa polisi kwa kuninyima hata nafasi ya kupiga simu kwa mtu yeyote kabla sijawekwa rumande."

"Nimeshangazwa na polisi hasa OCD, kunibambikia makosa ambayo hayana ukweli na kunidhalilisha kwa kunipiga vibao kama mtoto mdogo na dhihaka mbalimbali kwa wananchi wangu ambao walikuwa wakidai haki yao ya msingi. Hii si haki, sikutendewa haki katika hili ni uonevu mtupu!’’alilalamika Dk Kigwangalla.

Kilufi naye afikishwa tena kortini

Wakati huohuo Brandy Nelson anaripoti kutoka Mbeya kuwa
mashahidi watatu katika kesi inayomkabili Mbunge wa Mbarali kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Modestus Dickson Kilufi jana walianza kutoa ushahidi katika kesi hiyo ya kutishia kuua kwa maneno.

Kesi hiyo inayoendeshwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, jana ilianza kusikilizwa kwa shahidi wa kwanza Jordan Masweve, ambaye ndiye mlalakaji kumwambia Hakimu Mkazi Michael Mteite kuwa, Machi 16 mwaka huu, aliongozana na diwani wa kata yake, Alex Paulo kwenda katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.

Alieleza kuwa akiwa katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, ofisi tatu tofauti na alipomaliza shida zake alirejea kwenye gari tayari kwa kurejea nyumbani, alipofika kwenye gari, alikuta simu ya Diwani Paulo ikiita wakati mwenyewe akiwa mbali. Alisema wakati huo diwani huyo alikuwa akizungumza na Mbunge Kilufi.

”Nilichukua simu hiyo kwa lengo la kumpelekea diwani kabla sijafika katika eneo walilokuwepo Mbunge Kilufi alinipa tahadhari kuwa nisifike kwenye eneo hilo na kunitaka niende nikajisalimishe kwake ndani ya wiki mbili,”alisema na kuongeza:

“ Huku akijisifu kuwa nisipojisalimisha atanionyesha kwa kuwa ana marafiki wengi ambao ni watu wakubwa serikalini akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria.”

Alisema baada ya kuambiwa hivyo aliamua kuondoka, lakini Kilufi alianza kumrushia matusi kwa kumwambia kuwa yeye (Jordan) ni mpumbavu na kwamba baada ya kitendo hicho aliamua kwenda katika kituo cha Polisi kwa ajili ya kufungua jalada kwa kitendo hicho alichofanyiwa na Mbunge huyo.

Shahidi wa pili, Alex Paulo ambaye ni diwani wa Kata ya Rwiwa aliiambia mahakama kuwa wakati wakiendelea na maongezi na Mbunge Kilufi, alisikia mbunge huyo akijibizana na Masweve, akimtaka aondoe kesi mahakamani na kama asipofanya hivyo atamtoa roho.

Alisema baada ya kutolewa vitisho hivyo, aliongozana na Masweve kwenda kumweleza Mkurugenzi wa Wilaya, George Kagomba, ambaye aliwashauri kwenda kuripoti suala hilo polisi.

Baada ya upande wa mashahidi kumaliza kutoa ushahidi wao, Hakimu Mteite alimtaka Mbunge Kilufi aanze kujitetea, lakini mawakili wa Serikali walipinga kwa madai kuwa walikuwa hawajajiandaa kwa ajili ya kusikiliza upande wa utetezi.

Hakimu Mteite aliamua kuiahirisha kesi hiyo hadi leo siku ambapo Kilufi ataanza kujitetea.

Wabunge wengine walioonja rumande

Mzimu wa kulala rumande umewaandama wabunge kadhaa wa bunge la sasa katika siku za karibuni kutokana na visa na mikasa mbalimbali.

Waliofikwa na balaa hilo ni Mbunge wa Hai ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na mwenzake wa Moshi Mjini Philemoni Ndesamburo waliosekwa rumande mwishoni mwaka jana kutokana na kasheshe la uchaguzi wa udiwani Arusha. Mwingine aliyefikwa na balaa hilo, ni Mbunge wa Chadema, Arusha Godbless Lema.

Wengine ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) kwenye vurugu za Tarime, Mbunge wa CUF Viti Maalumu Mkoa wa Tabora , Magdalena Sakaya naye alijikuta akilala mahabusu kwenye sakata la wafugaji Tabora .

Susan Kiwanga Viti Maalumu Chadema na Sylivester Kasulumbai (Chadema- Maswa Mashariki) hawa walionja rumande kwenye sakata la uchaguzi wa Igunga uliomalizika hivi karibuni
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: