MKUU WA MKOA WA MOROGORO JOEL BENDERA NAFUNGA MASHINDANO YA KAMANDA CHIALO CUP 2011.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro Joel Bendera (mwenye kipaza sauti) akifafanua jambo wakati wa kufunga mashindano ya Kamanda Chialo Cup 2011 mara baada ya kumalizika mchezo wa fainali kati ya Polisi Morogoro SC na Maskani FC kwenye uwanja wa Shujaa mkoani hapa ambapo Maskani ilishinda kwa bao 2-1, kulia ni Kamanda wa Polisi mkoa huo wa Morogoro Adolfina Chialo na kushoto ni Mkuu wa kitengo cha Polisi Jamii mkoa huo (ASP) Iddi Ibrahim.
KIUNGO mshambuliaji wa timu ya soka ya Maskani FC Isdory Katula, amesema hataweza kusahau ushindi walioupata dhidi ya Polisi Morogoro SC ambao umewawezesha kutwaa ubingwa wa mashindano ya Kamanda Chialo Cup 2011 kwenye mchezo mkali na kusisimua wa fainali ambao ulifanyika hivi karibuni kwenye uwanja wa Shujaa kwa kuitandika bao 2-1 mkoani hapa.
Mashindano hayo ambayo yalianza kutimua vumbi agosti mosi mwaka huu yalishirikisha timu 24 zinazoshiriki ligi daraja la tatu mkoa ngazi ya taifa pamoja na timu za vijana chini ya umri wa miaka 23 ambapo yaliandaliwa kwa pamoja na taasisi ya kuendeleza na kuibua vipaji vya michezo ya Nyati Sports Promotion Morogoro na jeshi la polisi mkoa wa Morogoro yakiwa na ujumbe wa ulinzi shirikishi polisi jamii lengo likiwa kushirikiana na wananchi katika kuwafichua waharifu kuanzia ngazi ya kaya.
Katula ambaye ni nahodha wa timu hiyo ya Maskani FC alisema kuwa rufaha aliyopata kwa kuifunga Polisi Morogoro SC katika mchezo wa fainali kamwe hawezi kusahau kwani hiyo kwake na timu kwa ujumla imekuwa histori kubwa kutokana na kucheza na timu inayoshiriki ligi daraja la kwanza ikiwa na wachezaji wenye kiwango kikubwa cha soka wakiwemo washambuliaji hatari wa Polisi Morogoro SC Mokili Lambo, Ally Moshi, Nicolaus Kabipe na mlinda mlango mahili wa timu hiyo Salum Kondo.
Dalili za ushindi kwa timu ya Maskani FC zilianza mapema baada ya kufanikiwa kudhibiti eneo la kiungo la Polisi Morogoro SC na kuwafanya washambuliaji wa timu hiyo kushindwa kuleta madhala katika lango lao na kumaliza kipindi cha kwanza bila kufungana jambo ambalo lilikuwa faraja kwao kutokna na kucheza na timu hiyo yenye uwezo mkubwa katika mashindano hayo.
Maskani FC walianza kipindi cha pili kwa mchezo kwa kasi na kufanya shambulizi la haraka haraka na katika dakika ya 46 walifanikiwa kupata bao lililofungwa kiufundi na mshambuliaji Jamal Simba baada ya kupokea pasi ya Issa Ahmad kabla ya kuwazidi ujanja na kumtungua mlinda mlango wao wa Polisi Morogoro SC, Salum Kondo na kuandika bao la kuongoza.
Polisi Morogoro SC baada ya kufungwa bao hilo walitulia na kupanga mashambulizi na katika dakika ya 67 mshambuliaji Nicolaus Kabipe aliisawazishia timu yake bao na kuongeza mashambulizi kwenye lango la wapinzani wao mara kwa mara kwa lengo la kusaka bao la ushindi.
Mabeki wa Maskani FC walifanikiwa kuzuia mashambulizi ya washambuliaji wa Polisi Morogoro SC na katika dakika 70 hadi 78 walifanikiwa kuwadhibiti washambuliaji hao huku nao wakishambulia kwa kustukiza na katika dakika ya 78 mshambuliaji wao tegemeo, Jamal Simba alipachika bao kwa kichwa kufuatia krosi ya Godfrey Mweli na kuandika bao la pili na ushindi uliowafanya kuibuka mabingwa wa mashindano ya Kamanda Chialo Cup 2011 kutwaa zawadi ya ushindi wa kwanza sh 400,000 huku mshindi wa pili Polisi Morogoro SC ikipata zawadi y ash 300,000 na mashindi wa tatu timu ya Terminal FC ikiambulia sh 200,000.
0 comments:
Post a Comment