MMOJA WA NG'OMBE ANAYEDAIWA KUPIGWA RISASI NA ASKARI WA HIFADHI YA TAIFA YA MIKUMI MKOA WA MOROGORO KATIKA KIJIJI CHA NGAITE-LUHOZA TARAFA YA MASANZA KATIKA MPAKA WA MTO MIHOMBO UNAOTENGENISHA HIFADHI NA KIJIJI HICHO WILAYANI KILOSA JUNI 27 MWAKA HUU MKOANI HAPA.
SERIKALI imeahidi kutoa majibu ya tuhuma zinazotolewa na wafugaji wafugaji wa jamii ya kimasai wa kijiji cha Ngaite-Luhoza kuwatuhumu askari wa hifadhi ya taifa ya Mikumi kwa kuwaua kwa kuwapiga risasi mifugo yao zaidi ya 200 na kusababisha hasara ya zaidi ya 219Mil pindi wanapoingia ndani ya hifadhi hiyo katika vipindi vya kati ya mwaka 2010/2012
Naibu waziri wa maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kwa simu na kudai kuwa serikali inajipanga kwaajili ya kuitisha kikao maalumu baina ya pande hizo mbili za wafugaji na viongozi wa hifadhi hiyo ili kupata majibu muhimu yatakayosaidia kuimarisha ushirikiano baina ya pande hizo.
Kauli hiyo ya naibu waziri imekujaa baada ya wafugaji hao wa vijiji vya Ngaite-Luhoza na Kiduhi vilivyopo ndani ya tarafa ya Masanza wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro kutoa malalamiko kupitia vyombo vya habari ikiwemo gazeti hili kwa madai kuwa askari wa wanyama pori wa hifadhi hiyo katika nyakati tofauti wamewauwa mifugo hiyo kwa kuipiga risasi baada ya kuigia katika hifadhi hiyo.
Akizungumza njia ya simu Nyarandu alisema kuwa tayari wizara yake imepata malalamiko ya kuwepo kwa tuhuma hizo zinazodaiwa kufanywa na baadhi ya askari wa hifadhi ya taifa ya Mikumi ya kuwapiga risasi mifugo mara wanapoingia ndani ya hifadhi hiyo baada ya kukutana na wawakilishi wa jamii ya wafugaji hao mapema wiki iliyopita katika viwanja vya Bunge Mkoani Dodoma.
Akielezea juu ya tuhumu hizo Nyarandu alisema kweli ameonana na wawakilishi wa wafugaji wa vijiji hivyo na baada ya kukabidhi vielelezo vyao ameahidi kulifanyia kazi kwa kuwakutanisha viongozi wa hifadhi na wafugaji hao ili kuweza kutatua tatizo hilo.
“Nimepata malalamiko juu ya askari wa hifadhi ya taifa ya Mikumi wakituhumiwa kuwapiga risasi mifugo zaidi ya 200 kati ya mwaka 2010 na 2012 hivyo baada ya kukutana na wawakilishi wa wafugaji hao nimemuagiza katibu mkuu kuniandalia mkutano baina ya viongozi wa hifadhi ya Mikumi na wafugaji wa vijiji vya Ngaite-Luhoza na Kiduhi ili niweze kukaa nao na kutatua tatizo hilo” alisema Nyarandu.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoipata toka kwa wafugaji hao vikiwemo vielelezo vyao,tatizo kubwa ni mpaka ambao unatenganisha hifadhi na vijijini ambapo kuna mto Mihombo.
Alisema kuwa wafugaji hao wamelalamika wakati mifugo yao ikienda kunywa maji katika mto huo unaotenganisha hifadhi na makazi ya raia ipo ile inayovuka na kuingia katika sehemu ya hifadhi hivyo askari hao wamekuwa wakiwapiga risasi huku ukijua hakuna mto mwingine unaoweza kutumiwa na wafugaji hao kunywesha mifugo ya maji baada ya machungo
Nyarandu alisema kuwa serikali haiungi mkono vitendo hivyo vinavyofanywa na askari hao na kubainisha kuwa katika njia za kuleta usuluhishi na kuepusha migogoro hiyo wizara yake itaangalia uwezekano wa kuwachimbia visima wafugaji hao ikiwa ni sehemu ya kuweka mshikamano baina ya pande hizo amabazo kwa kiwango kikubwa imeanza kupoteza mashiko baada ya askari hao kutuhumiwa kuuwa mifugo ya wafugaji wa jamii ya kimasai na kuwaletea hasara kubwa.
Alibainisha kuwa mara baada ya uchunguzi kufanyika na kubaini kuwepo kwa matukio hayo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya askari wanaodaiwa kufanya matukio hayo.
Naye mkuu wa msafara wa wafugaji wa vijiji hivyo vya Ngaite-Luhoza na Kiduhi tarafa ya Masanza wilaya ya Kilosa Ibrahim Oloishuro alisema kuwa wamechukua hatua ya kuonana na waziri baada ya kukidhiri kwa matukio ya mifugo ya kupigwa risasi na askari wa hifadhi ya taifa ya Mikumi huku idadi hiyo ikipanda mwaka hadi mwaka.
Oloishuro alisema kwa takwimu ambazo wamemkabidhi naibu waziri ni pamoja na idadi ya mifugo 204 tangu mwaka 2010 hadi 2012 vikiwemo na vielelezo vingine vinavyohusiana na mikapa.
Kwa mujibu wa Oloishuro alisema kuwa mwaka 2010 jumla ya mifugo 169 walikufa kwa kupigwa risasi wakiwemo ng’ombe 149 na mbuzi 20 wakati mwaka 2012 ng’ombe 55 walikufa kwa kupigwa risasi ambapo mifugo hiyo ilipigwa kwa nyakati tofauti tofauti.
“kwa sasa kuna hasara ya zaidi ya sh200Mil tuliyopata wafugaji kwa ng’ombe na mbuzi kufa kutokana na kupigwa risasi ambapo matukio hayo yameanzia kuanzia mwaka 2010 na mwaka 2012 na mwaka pekee ambao sisi wafugaji hatupoteza mifugo ni mwaka 2011 pekee na waolengwa zaidi ni madume yanayozalisha” alisema Oloishuro.
Hatua hiyo ya wafugaji wa kijiji cha Ngaite-Luhoza na Kiduhi imekuja baada ya kuwepo vitendo vilivyokidhiri vya kupigwa risasi kwa mifugo ya wafugaji wa jamii ya kimasai ikiwemo mifugo 17 walipigwa risasi ambapo watano kati yao walikufa lililotokea juni 27, 2012.
0 comments:
Post a Comment