Mrisho Ngassa akiwa anashangilia goli kwa mashabiki wa Yanga baada ya kufunga
goli la pili huku la kwanza likiwa limefungwa na John Bocco nyuma yake katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya AS VITA ya Congo DRC ambapo Azam FC waliibuka na ushindi wa bao 2-1.
MRISHO Khalfan Ngassa ameuzwa Simba kwa dau la Sh 25Mil mchana wa leo, Azam imethibitisha.
Habari za ndani kutoka Azam, ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka klabu hiyo, zimesema kwamba Simba wamelipa fedha hizo na wamesainiwa fomu za uhamisho na sasa Mrisho anafuata nyayo za baba yake Khalfan Ngassa, ambaye aliichezea Simba SC 1991/1992.
Azam ilifikia uamuzi wa kumuuza Ngassa, baada ya mchezaji huyo iliyemsajili kutoka Yanga miaka miwili iliyopita, kubusu jezi ya Yanga baada ya kufunga bao la pili katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Na uamuzi huo, ni wa mzee Said Salim Bakhresa mwenyewe, ambaye alikerwa na kitendo hicho akawaagiza wanawe, Wakurugenzi wa bodi ya timu wamuuze mchezaji huyo popote, haraka iwezekanavyo.
Ngassa alikuwa amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake aliosaini na Azam FC, akitokea Yanga miaka miwili iliyoipita kwa dau la Sh.
Milioni
55, lakini wasiwasi unakuja kwamba, Ngassa ana mapenzi na Yanga na kwa
Simba kumsajili, kuna hatari yaliyotokea akiwa Azam, yatajirudia hata
akiwa kwa Wekundu wa Msimbazi.
Mapema leo mchana, Stewart Hall, kocha Muingereza wa Azam FC jana alifukuzwa katika klabu hiyo kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Habari ambazo BIN ZUBEIRY ilizipata kutoka ndani ya Azam, zilisema kwamba kikao cha jana cha pamoja baina ya Bodi ya Ukurugenzi ya Azam FC, Mwanasheria wa kampuni na kocha Stewart kimeafiki kuvunja ndoa hiyo na sasa Azam FC itakuwa chini ya kocha kutoka India, Vivek Nagul ambaye alikuwa anafundisha timu ya vijana.
Habari zinasema kwamba, mapema baada ya mechi ya Nusu Fainali ya Kagame, kati ya Azam na AS Vita ya DRC, Stewart aliitwa na kuambiwa asimtumie tena Ngassa kwa kitendo cha mchezaji huyo kwenda kuibusu na kuivaa jezi ya Yanga, baada ya kufunga bao la ushindi.
Lakini Stewart katika kikao hicho, kwanza alimtetea Ngassa kutokana na kufunga bao la ushindi na kumuelezea kama mchezaji muhimu kwake, lakini msimamo wa bodi ulikuwa ni asipangwe tena.
Katika fainali, Stewart alimvalisha jezi Ngassa akamuanzishia benchi, lakini kama ilivyokuwa kwenye Nusu Fainali alimuingiza kipindi cha pili timu ikiwa nyuma kwa 1-0 na mwisho wa mchezo ikashinda 2-1 yeye akifunga la pili, dhidi ya Yanga pia alimuingiza timu ikiwa nyuma kwa 1-0.
Lakini Ngassa alishindwa kurudia kile alichofanya kwenye mechi na AS Vita na Yanga ikashinda 2-0.
Mbali na Ngassa, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ pia yuko katika wakati mgumu na jana inadaiwa alionekana akilia wakati anazungumza na kiongozi mmoja wa Azam, akiuliza ni lipi kosa lake.
Sure Boy, ambaye ni mtoto wa kocha wa timu ya vijana ya Yanga, Abubakar Salum ‘Sure Boy’ jana hajafanya mazoezi na leo pia, naye pia akituhumiwa kucheza kinazi katika mechi dhidi ya Yanga.
Stewart anakuwa kocha wa nne ndani ya miaka minne kufukuzwa Azam, tangu Neider dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin, Mbrazil mwingine.
Lakini ni Stewart angalau anaacha kumbukumbu ya taji na Medali Azam,
baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika nafasi ya
pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la
Urafiki na Kagame mwezi uliopita.
Habari kwa hisani ya Mahmoud Zubeiry BLOG
0 comments:
Post a Comment