Balozi Christopher Stevens.
MAAFISA wa Libya wanasema Balozi wa Marekani nchini Libya, Christopher Stevens, na wafanyakazi wengine wa ubalozi wameuawa baada ya kundi la watu kuvamia ubalozi mdogo katika mji wa Benghazi Jumanne usiku.
Vifo hivyo vimetokea baada ya waandamanaji waliokasirishwa na sinema iliyotengenezwa Marekani ikimkashifu Mtume Muhammad kufyatulia risasi na kuchoma moto sehemu za ubalozi huo mjini Benghazi.
Balozi J. Christopher Stevens, mwanadiplomasia wa siku nyingi na mmoja wa mabalozi wenye uzoefu mkubwa katika eneo hilo, alikuwa nchini humo chini ya miezi minne tu baada ya kuchukua wadhifa huo mjini Tripoli mwezi Mei.
Waziri mdogo wa mambo ya ndani wa Libya Wanis al-Sharif alisema balozi huyo aliuawa "pamoja na maafisa wengine watatu," akithibitisha kuwa Stevens alikuwepo ndani ya ubalozi huo uvamizi ulipotokea.
Sharif aliwaambia waandishi kuwa kundi la watu wenye silaha walishambulia ubalozi huo katika hali ya "kujitoa mhanga." Alisema ubalozi wa Marekani "una makosa" kwa kutochukua hatua za kutosha.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani haijatoa tamko lolote kuhusiana na habari hiyo.
Maandamano yalivyokuwa Lebanon.
WAKATI HUO HUO Mchezaji sinema mwanamke aliyetokea katika filamu iliyozusha maandamano ya waislamu sehemu kadha duniani amefungua mashitaka dhidi ya mtengenezaji filamu hiyo kwa udanganyifu.
Katika madai hayo, yaliyofunguliwa mjini Los Angeles, muigizaji Cindy Lee Garcia anadai kuwa mtengenezaji filamu hiyo The Innocence of Muslims, Nakoula Basseley Nakoula, alimhadaa kwa kumwambia kuwa anatokea katika filamu inayoonyesha maisha ya zamani Misri.
Lakini maneno waliyotumia wakati wa kupiga filamu hiyo yalibadilishwa na maneno ya kumkashifu Mtume Muhammad.
Garcia anasema amepata vitisho kadha vya kuuawa tangu toleo fupi la filamu hiyo litolewa katika mtandao wa Internet na anashindwa kuonana na familia yake kwa hofu kwamba wanaweza kudhuriwa.
0 comments:
Post a Comment