wa ufupi
Mshambuliaji wa Stars, Mrisho Ngassa alifunga bao pekee kwenye mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wikiendi iliyomalizika.Kikosi cha baadhi ya wachezaji wa zambia kikishangilia.
KIPIGO cha bao 1-0 walichokipata mabingwa wa Afrika, Chipolopolo
ya Zambia kutoka kwa Taifa Stars ya Tanzania, kimemshtua Kocha Herve
Renard na sasa ameamua kuwatoa kwenye kikosi wachezaji wa kikosi hicho
wanaocheza ligi ya ndani nchini humo.
Mshambuliaji wa Stars, Mrisho Ngassa alifunga bao
pekee kwenye mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam wikiendi iliyomalizika.
Akizungumza na gazeti la Times of Zambia muda
mfupi baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kenneth
Kaunda akitokea Tanzania, Renard alisema wachezaji wa ndani wanapaswa
kuthibitisha ubora wao kwenye michezo ya kirafiki ili waweze kuingia
kwenye kikosi cha Chipolopolo.
“Wachezaji wa ndani wanahitaji kuonyesha uwezo wao kabla ya kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa,” alisema Renard.
“Kila tunaposafiri na wachezaji wa ndani tunapata
matatizo, hiyo ni ishara kwamba wanatakiwa kufanya kazi ya ziada, lakini
wengi wao wamekuwa ni mzigo kwa timu,” alisema.
Renard ambaye ametwaa tuzo ya Kocha Bora Afrika wa
mwaka 2012, alisema wachezaji kama Mukuka Mulenga na Saulani Phiri
pamoja na kipa Joshua Titima walionyesha kiwango kizuri.
Hiyo ndiyo sababu tosha ya kuwaita kwenye kikosi
chake cha wachezaji 23, atakachokitangaza siku 10 kabla ya kuanza kwa
michuano ya Afrika.
Renard alisema Wazambia hawapaswi kuwa na hofu kwa
matokeo dhidi ya Tanzania kwa sababu ni sehemu ya maandalizi yao, pia
mechi hiyo aliwakosa wachezaji wake 12 atakaokwenda nao Afrika Kusini.
Pia, kocha huyo alionyesha shaka na viwango vya
wachezaji wake, lakini ameahidi kulifanyia kazi suala hilo katika
kipindi cha wiki tatu zilizobaki kabla ya fainali hizo, ambapo Zambia
ipo Kundi C pamoja na Ethiopia, Burkina Faso na Nigeria.
Nahodha wa Chipolopolo, Chris Katongo, Isaac
Chansa, na James Chamanga (wanacheza China) pamoja na nyota wa TP
Mazembe, Rainford Kalaba, Nathan Sinkala, Hichani Himoonde na Stopila
Sunzu walicheza mechi ya Tanzania.
Wakati huohuo, Stars itaingia kambini Januari 6
kujiandaa na mechi za kufuzu kucheza fainali za mataifa ya Afrika kwa
wachezaji wa ndani mwaka 2014.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Boniface Wambura alisema jana Stars ilivunja kambi mara baada ya mechi
na sasa wanajipanga ili timu iende kuweka kambi Afrika Kusini.
0 comments:
Post a Comment