BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAHAKAMA ILIVYOJIRUDI KISHERIA KATIKA RUFAA YA GODBLESS LEMA.


KWA UFUPI
Jopo la Majaji wa Rufaa, Bernard Luanda, Salum Massati na Nathalia Kimaro lilitengua hukumu ya Mahakama Kuu baada ya kuridhika kuwa hakukuwa na uthibitisho wowote kuwa wadai watatu katika shauri ya msingi ambao walikuwa wajibu rufaa, walikuwa wapigakura katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema akizungumza na wafuasi wa chama hicho makao Makuu ya Chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam jana baada ya Mahakama ya rufani kumrudishia ubunge wake jana.Picha na Fidelis Felix.




MAHAKAMA ya Rufaa Tanzania imemrejeshea Ubunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema kwa kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iliyomvua ubunge huo Aprili 5, mwaka huu.
Lema alivuliwa ubunge na Jaji, Gabriel Rwakibarila baada ya kuridhika na ushahidi wa walalamikaji; Mussa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo pamoja na mashahidi wao kuwa alitumia lugha za kashfa na matusi dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Batilda Burian.
Jopo la Majaji wa Rufaa, Bernard Luanda, Salum Massati na Nathalia Kimaro lilitengua hukumu ya Mahakama Kuu baada ya kuridhika kuwa hakukuwa na uthibitisho wowote kuwa wadai watatu katika shauri ya msingi ambao walikuwa wajibu rufaa, walikuwa wapigakura katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
Mengi yamezungumzwa kuhusu hukumu ya Jaji Rwakibarila na pengine yatazungumzwa kuhusu hukumu ya jana ya Jopo la Majaji wa Rufaa. Wapo wanaofurahi na waliochukizwa na hukumu zote mbili.
Hoja tatu zimezua mjadala baada ya hukumu ya Mahakama Kuu na pengine zitaendelea kujadiliwa hata baada ya hukumu ya jana. Kimsingi, hukumu iliyomrejesha Lema bungeni ambayo kwa njia moja au nyingine, imejibu maswali yaliyotawala katika medani ya sheria.
Hoja ya msingi iliyojibiwa na Mahakama ya Rufaa ni kuhusu haki ya wadai, Mkanga, Agnes na Kivuyo iwapo walikuwa na uhalali na haki ya kufungua madai mahakamani kulalamikia mambo ambayo hayakuathiri haki yao kama wapigakura.
Pili, ni Je, Jaji Rwakibarila alikuwa sahihi kukubali hoja za wadai na mashahidi wao ambao ni wanaCCM na kuyatumia kutengua ushindi wa Lema, lakini akatupilia mbali ushahidi wa utetezi kwa sababu mashahidi wote walikuwa ni wanachama na viongozi wa Chadema, hivyo walikuwa na masilahi kwa upande mwingine.
Wakati mdai wa pili, Mollel ni Mwenyekiti wa Mtaa kupitia tiketi ya CCM, yule wa tatu, Happy Kivuyo alikuwa Katibu Mwenezi wa CCM Kata ya Sokon I, jijini Arusha wakati mdai wa kwanza, Mussa Mkanga aliwahi kuwa Diwani wa Kata ya Sombetini kwa zaidi ya miaka 15 kwa tiketi ya CCM.
Tatu, ilikuwa sahihi kisheria Mahakama kumvua Lema ubunge kwa ushahidi wa mdomo usio na nyaraka za kuthibitisha madai dhidi yake?
Mahakama ya Rufani
Katika uamuzi wa jana, Jopo la Majaji wa Rufaa walizingatia hoja moja tu ya wadai kutokuwa na haki kisheria kufungua malalamiko kwa mambo ambayo hayakuathiri haki zao za kupiga kura.
Katika uamuzi wao uliosomwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Elizabeth Mkwizu, Jopo hilo lilienda mbali kwa kusema hakukuwa na kumbukumbu zozote katika nyaraka za Mahakama zanazoonyesha kama kweli wadai hao ni wapigakura waliosajiliwa kwenye daftari la kudumu la wapigakura.
Tangu hatua za awali za usikilizwaji wa shauri hili, Wakili wa Lema, Method Kimomogolo na Wakili Mkuu wa Serikali, Timon Vitalis aliyekuwa akimwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali walipinga uhalali wa wadai ya kufungua kesi kulalamikia masuala ambayo hayakuathiri haki yao ya kupiga kura.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: