KWA UFUPI
Baadhi ya maeneo ambayo wanasiasa hao walivamia mikutano ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kusababisha ivunjike ni Shehia za Magomeni na Mpendae Mkoa wa Mjini Magharibi.Hii ni mara ya kwanza ghasia kuzuka katika mikutano ya kukusanya maoni ya Katiba Mpya visiwani humo.
Mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba Jaji warioba.
MIKUTANO ya kukusanya maoni ya upatikanaji wa Katiba Mpya Visiwani Zanzibar, imeingia dosari baada kuzuka ghasia na baadhi ya watu kujeruhiwa kwa kuchomwa visu.
Vurugu hizo ambazo chanzo chake ni siasa, zilitokana na wafuasi wa baadhi ya vyama vya siasa, kuvamia mikutano iliyokuwa ikifanyika Unguja na kusababisha hofu za kiusalama.
Baadhi ya maeneo ambayo wanasiasa hao walivamia mikutano ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kusababisha ivunjike ni Shehia za Magomeni na Mpendae Mkoa wa Mjini Magharibi.
Hii ni mara ya kwanza ghasia kuzuka katika mikutano ya kukusanya maoni ya Katiba Mpya visiwani humo.
Tukio la kuchomana visu, lilitokea katika Shehia ya Mpendae baada ya vurugu zilizosababishwa na vijana kuvamia mkutano uliokuwa ufanyike jana mchana.
Vijana hao walianzisha ghasia hizo baada ya kutaka kuvunja utaratibu uliokuwa umewekwa. Walitaka wakae mbele ya wengine waliokuwa wametangulia katika mkutano huo.
Hatua hiyo ilipingwa na kuibua ghasia ziliozababisha watu kadhaa kujeruhiwa kwa visu.
Tukio jingine lililovuruga mkutano huo ni lile lililotokea katika Shehia ya Magomeni, Jumatatu wiki hii baada ya kuibuka kwa mvutano baina ya makundi mawili yenye misimamo tofauti juu ya mfumo wa Muungano;
kuna wanaopinga na wanaoukubali.
Misimamo hiyo imeelezwa kujikita katika misingi na sera za vyama vyao vya kisiasa.
Katika misimamo hiyo, CUF kinaamini katika Serikali ya Zanzibar na Tanganyika kila moja kuwa na mamlaka kamili na Muungano uwe wa mkataba wakati, CCM kinasimamia kwenye Serikali mbili; Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Shehia ya Magomeni
Saa mbili kabla mkutano kuanza, watu wengi walifika Uwanja wa Mzalendo ambako mkutano ulitakiwa kufanyika. Walijipanga kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Tume ambao ni aliyewahi kufika ndiye anayetangulia kutoa maoni.
Hali hiyo ilisababisha wakazi wa Shehia hiyo waliokuwa wenyeji wa mkutano, kukosa nafasi ambayo ingewawezesha kutoa maoni kwa mazungumzo ya ana kwa ana.
Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni, Salmin Awadh Salmin, alisema hawakuwa tayari kuwa wenyeji wa mkutano ambao hawatashiriki akisema waliokuwa wamejipanga wote walifikishwa kituoni hapo kwa magari kwa lengo maalumu la kuwakosesha wenyeji kutoa maoni yao, kwa kuwa inafahamika kuwa wengi wao ni wana CCM.
Hoja hizo alizitoa kwa wajumbe wa Tume ambao pia hawakuridhishwa na hali ya usalama katika eneo hilo kutokana na vurugu zilizokuwa zikifanywa na wafuasi wa CCM na CUF.
“Kwa hali ilivyo, hatuwezi kupata utulivu utakaowezesha tufanye kazi kwa ufanisi na kumaliza mkutano kwa amani bila fujo. Natangaza rasmi kuwa leo hakuna mkutano,” Mwenyekiti wa Timu ya Tume hiyo inayokusanya maoni visiwani hapa, Profesa Mwesiga Baregu.
Akizungumza baada ya kuvunjika kwa mkutano huo, Salmin alisema waliokuwa wamefika kutoa maoni walikuwa wakitaka kunadi misimamo ya vyama vyao akisema hiyo ni hali ya kihistoria inayowakabili wakazi visiwani humo.
0 comments:
Post a Comment