RAIS wa Misri Mohamed Mursi ametia saini rasimu ya katiba kuwa sheria
akisema hatua hiyo itasaidia katika kuumaliza mvutano wa kisiasa na
kumruhusu kuangazia hatua ya kuirekebisha hali tete ya kiuchumi.
Matokeo juu ya kura ya maoni kuhusu katiba yaliyotangazwa Jumanne yameonyesha kwamba asilimia 63.8 ya wamisri wameiridhia katiba hiyo kwa kupiga kura ya ndio na kufungua njia ya kufanyika uchaguzi wa bunge katika kipindi cha takriban miezi 2 ijayo.
Asilimia 63.8 wapitisha katiba mpya.
Ushindi huo unamaanisha kundi la udugu wa kiislamu limepata ushindi wa tatu tangu alipoondolewa kwa nguvu madarakani kiongozi wa zamani Hosni Mubarak mwaka 2011 baada ya huko nyuma kushinda uchaguzi wa bunge na rais.
Ofisi ya rais Mursi imetangaza kwamba Jumanne usiku kiongozi huyo aliamua kutia saini kuwa sheria rasimu hiyo ya katiba ya tangazo rasmi la matokeo ya kura ya maoni yaliyoonyesha kwamba asilimia kubwa ya wamisri wameikubali katiba hiyo ambayo ni ya kwanza tangu kutimuliwa madarakani Hosni Mubarak.
Hata hivyo pamoja na kutajwa kwamba wengi wameiridhia katiba hiyo,kumejitokeza mgawanyiko mkubwa katika nchi hiyo ya kiarabu hali ambayo imekuwa ikizusha maandamano ya ghasia mara kwa mara katika mitaa ya mji mkuu Cairo.
Makundi ya upinzani yanailaani katiba hiyo yakisema kwamba imezingatia zaidi misingi ya itikadi kali na haifuati misingi ya kidemokrasia.
Wapinzani wanalalamika kwamba katiba hiyo inatoa nafasi kwa viongozi wa kidini kuingilia kati hatua za kuunda sehria na kuyaacha kando makundi ya waliowachache bila ulinzi wa kisheria.
Hata hivyo rais Mursi aliyesaidiwa na kuungwa mkono kuingia madarakani na washirika wake katika kundi la udugu wa kiislamu anaamini kupitishwa katiba hiyo ni hatua muhimu kabisa ya kumaliza kipindi cha mvutano na hali ya wasiwasi wa kiuchumi ambayo imelikumba taifa hilo.
Ametilia mkazo kwamba katiba hiyo mpya inatoa ulinzi kwa kila mwananchi wa Misri bila ya kujali makundi yao akisema kwamba wamisri wamechoshwa na maandamano ya mitaani ambayo yamesababisha kuzuia hali ya kawaida kurejea pamoja na kuizuia serikali kutoangazia suala la uchumi.
Uchumi wayumbayumba.
Serikali ya rais Mursi inadai kwamba wapinzani wanauharibu uchumi wa nchi kwa kurefusha mvutano wa kisiasa.Hata hivyo kinachoshuhudiwa kwa sasa katika mitaa ya mjini Cairo kitovu cha maandamano ni utulivu huku yakionekana makundi ya watu wachache tu wanaoandamana na kuchoma matairi wakati wa usiku.
Aidha Mursi na serikali yake wameahidi kuanzisha hatua isiyopendwa na wengi ya kuongeza kiwango cha kodi pamoja na kupunguza bajeti ya matumizi ya nchi ili kupata mkopo kutoka shirika la fedha la kimataifa IMF.
Rais huyo pia anatarajiwa kwenda Ujerumani Januari 29 kuomba msaada wa kuujenga upya uchumi wa taifa lake.
0 comments:
Post a Comment