UJERUMANI inakamilisha mhula wake wa miaka 2 kama mwanachama asiye wa
kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa uliogubikwa na mzozo wa
Libya na Mashariki ya kati
Miaka miwili ya Ujerumani kuwa mwanachama wa zamu wa baraza la Usalama
la Umoja wa mataifa inamalizika baadaye hii leo na matokeo yake
yamepokelewa kwa aina tofauti.Msemaji wa tume ya mambo ya nchi za nje ya wabunge wa chama kikuu cha upinzani nchini Ujerumani cha Social Democratic, SPD, Rolf Mützenich, anahisi Ujerumani imejitahidi ikiwa kama mwanachama asiye wa kudumu wa baraza la usalama, kuhakikisha zinajadiliwa pia mada ambazo kwa jumla hazijadiliwi sana na hasa kuhusiana na watoto katika vita.
Anasema balozi wa Ujerumani katika Umoja wa mataifa, Peter Wittzig, na waziri wa mambo ya nchi za nje, Guido Westerwelle, wameyaleta pia katika meza ya mazungumzo masuala yanayohusiana na mabadiliko ya tabia nchi na sera ya aina mpya kuelekea Afghanistan.
Maamuzi mawili makuu yameugubika mhula wa miaka miwili ya Ujerumani katika baraza la usalama. Wa kwanza ilikuwa Machi 17 mwaka 2011 pale baraza la usalama lilipopiga kura kuhusu Libya.
Azimio hilo lililengwa kuharakisha kung'atuka madarakani aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi.
Katika wakati ambapo washirika wa magharibi waliunga mkono mashambulio ya angani, Ujerumani ilijizuwia sawa na Urusi, China, Brazil na India. Uamuzi huo wa Ujerumani ulikosolewa na baadhi ya wanasiasa humu nchini.
Jukumu la Ujerumani kuelekea Israel
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (kushoto) na kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Na wiki chache zilizopita walimwengu waliikodolea macho hadhara kuu ya Umoja wa mataifa.
Wakati ule lilihusika suala kama Palestina itakubaliwa nafasi ya mwangalizi, bila ya kuwa mwanachama wa Umoja wa mataifa.
Ujerumani ilijizuwia kupiga kura katika suala hilo muhimu katika mzozo wa mashariki ya kati na uamuzi huo wa Ujerumani ukasifiwa na wengi miongoni mwa wadadisi.
Mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa kutoka Münster, Profesa Sven Bernhard Gareis, anasema, "Kuelekea Israel, imebainishwa tuna jukumu maalumu, tuna urafiki wa dhati pamoja na taifa la Israel na wananchi wa Israel.
Lakini imedhihirishwa pia kwamba sera za ujenzi wa makaazi ya wahamiaji, zinazoendelezwa na waziri mkuu Benjamin Netanyahu, zinaangaliwa na serikali kuu ya Ujerumani kama kizingiti katika kupatikana ufumbuzi wa madola mawili."
Mageuzi ya baraza la Usalama
Kikao cha baraza la usalama la Umoja wa mataifa
Kuanzia Januari mosi Ujerumani inarejea kukikalia kiti chake kama mwanachama wa kawaida wa Umoja wa mataifa. Juhudi za kulifanyia mageuzi baraza la usalama hadi sasa bado hazijaleta tija.
Mbali na wingi wa thuluthi mbili ya kura kutoka hadhara kuu ya Umoja wa mataifa, wanachama wote watano wa kudumu wa baraza la usalama wanabidi waunge mkono mwongozo mpya.
Mmoja tu akipinga, utaratibu mzima utashindwa kutekelezwa.
0 comments:
Post a Comment