MZOZO wa kisiasa nchini Misri unaonekana kuzidi kupanuka, baada ya
kikundi muhimu cha upinzani kuitisha maandamano makubwa kupinga kura ya
maoni juu ya mswada wa katiba, ambayo inatarajiwa kupigwa tarehe 15
Desemba.
Hayo yanajiri licha ya hatua ya rais Mohammed Mursi kuondoa sheria
aliyokuwa amepitisha kujilimbikizia madaraka.
Katika tangazo
lililotolewa kwa vyombo vya habari na kikundi kikubwa cha upinzani
nchini Misri, National Salvation Front, kikundi hicho kimesema
kinaipinga kura ya maoni juu ya mswada wa katiba, kwa sababu kinaamini
kwamba itasababisha mgawanyiko na migogoro zaidi.
Kikundi hicho kimeitisha maandamano makubwa kesho Jumanne katika miji
yote ya nchi hiyo, kuupinga mswada huo ambao kwa kiwango kikubwa
uliandikwa na tume inayodhibitiwa na wanasiasa wa kiislamu.
Mohamed ElBaradei, kiongozi wa kikundi kilichoitisha maandamano mapya
Uamuzi wa pupa
''Kuitisha kura ya maoni wakati nchi ikikumbwa na mivutano,
kunadhihirisha jinsi serikali inavyofanya mambo kwa pupa'', kilidai
kikundi hicho cha upinzani.
Kikundi hicho kinaongozwa na mwanasiasa
maarufu Mohammed el-Baradei, ambaye kupitia mtandao wa kijamii wa
Twitter, amesema, ''Tutaiangusha katiba ambayo haitilii maanani haki
zetu na uhuru wetu''.
Upinzani unasisitiza kwamba katiba hiyo inapuuza haki za msingi na uhuru
wa wanawake. Ikiwa wananchi wa Misri wataikataa katiba hiyo katika kura
ya maoni ya tarehe 15 Desemba, Rais Mohammed Mursi ataitisha uchaguzi
katika kipindi cha miezi mitatu, kuchagua baraza jipya la wawakilishi.
Maandamano mkabala
Rais wa Misri Mohammed Mursi
Kikundi cha Udugu wa Kiislamu ambacho ndicho anachotoka rais Mursi
kimeunga mkono uamuzi wake, na kuwataka wapinzani kuepuka kile
kilichokiita matatizo yasio na msingi. Msemaji wa kikundi hicho Mahmoud
Ghuzlan amesema raia wote wa Misri wanapaswa kuupigia kura mswada wa
katiba, na kuongeza kuwa kura hiyo inapaswa kupigwa kwa tarehe
iliyopangwa, bila mabadiliko wala kucheleweshwa.
Misri imekumbwa na maandamano makubwa mnamo wiki mbili zilizopita.
Watu saba walipoteza maisha yao Jumatano wiki iliyopita, katika
maandamano mengine yaliyowakutanisha watu wanaounga mkono kambi tofauti
za kisiasa.
Muungano wa vyama vya kiislamu umesema utafanya maandamano makubwa kesho
Jumanne kumuunga mkono rais Mursi, hii ikiwa ni kwa mujibu wa tovuti ya
gazeti linalomilikiwa na serikali.
Hakuna dalili ya suluhu
Watu kutoka kambi zinazokinzana kisiasa walipiga kambi nje ya Ikulu ya
rais mjini Cairo kwa siku tatu mfululizo, na waandamanaji zaidi
walijiunga nao Jumapili.
Wiki iliyopita, eneo hilo lilishuhudia
makabiliano yenye ghasia baina ya waandamanaji wanaompinga rais na wale
wanaomuunga mkono.
Misri imekumbwa na maandamano makali mnamo wiki mbili zilizopita,
kumshinikiza rais Mohammed kubatilisha uamuzi alioutangaza tarehe 22
Novemba, kupanua madaraka yake na kuahirisha kura kuhusu katiba.
Huo
ndio mzozo mkubwa zaidi kuikumba nchi hiyo tangu kuchaguliwa kwa rais
Mursi mwezi June mwaka huu.
Ingawa Mursi aliiondoa shereia hiyo mwishoni
mwa juma, waandamanaji wa upinzani tayari wameanza kumtaka aondoke
kabisa madarakani.
0 comments:
Post a Comment