“Uhuru
wa tume utaanzia tangu kwenye jina la tume yenyewe…; Kubadilishwa kwa jina na
kuweka neno ‘Huru’ kunaweza kubadili fikra za wadau juu ya Tume ya
Uchaguzi,”alisema Lubuva. Jaji Mstaafu, Joseph
Warioba ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba akizungumza na
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damiani Lubuva (kulia)
jijini, Dar es Salaam jana. Picha na Juliana Malondo.
MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Mstaafu
Damian Lubuva ametoa maoni mbele ya Tume ya Katiba akipendekeza kuwa Katiba
Mpya iunde Tume Huru ya Uchaguzi na kwamba itambulike kwa jina la Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi.
Jaji Lubuva aliyekuwa akitoa maoni hayo kwa niaba ya Tume ya
Taifa ya Uchaguzi, alisema kuwa tume huru ni inayokubalika na wadau wote wa
uchaguzi na wananchi kwa jumla, ambayo katika utekelezaji wa majukumu yake,
itafanya kazi zake bila kuingiliwa.
“Uhuru wa tume utaanzia tangu kwenye jina la tume yenyewe…;
Kubadilishwa kwa jina na kuweka neno ‘Huru’ kunaweza kubadili fikra za wadau
juu ya Tume ya Uchaguzi,”alisema Lubuva.
Lubuva alifafanua kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, inapaswa
kuanzishwa chini ya sheria mama ya nchi ambayo ni Katiba, kama ilivyo kwa nchi
nyingine za Afrika.
Alizitaja baadhi ya nchi hizo zilizo na tume huru za uchaguzi
kuwa ni pamoja na Afrika Kusini, Kenya, Ghana, Zimbabwe na Botswana.
Alipendekeza pia uteuzi wa wajumbe wa Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi ufanywe na wadau mbalimbali na kuteuliwa na rais kabla ya
kuthibitishwa na Bunge.
“Na kwa kuboresha mazingira ya upatikanaji wa wajumbe
wa tume hiyo na viongzi wengine tumependekeza pia Katiba Mpya itamke kwamba
wadau mbalimbali watashiriki kupendekeza majina, ambayo mwisho wake Rais
atashiriki kuteua majina, lakini siyo rais ateue moja kwa moja,” alisema Jaji
Lubuva.
Mbali na hayo, Jaji Lubuva pia alipendekeza Katiba Mpya itambue
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini akataka isiunganishwe na Tume Huru
ya Taifa ya Uchaguzi katika utendaji wake wa kazi.
“Pia tunapendekeza Katiba iipe Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
mamlaka ya kugawa kata katika maeneo ya uchaguzi wa madiwani,” alisema.
Alisema kuwa mamlaka hiyo hivi sasa iko chini ya Wizara ya
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi), jambo alilosema lina athari
kipindi cha uchaguzi, kwa kuwa huathiri uchaguzi wa madiwani, ambao hufanywa na
Tume.
Ofisi ya Msajili wa Vyama
Akizungumzia utendaji kazi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa pamoja na NEC, Mwenyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi alisema:
“Tumependekeza kwamba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itambulike kikatiba.
Tumetaka pia kazi za ofisi hiyo zifanyike kwa kujitegemea na zisichanganywe na
NEC.”
Tangu mwaka 1995 ulipofanyika Uchaguzi Mkuu wa kwanza chini ya
mfumo wa vyama vingi uliorejeshwa mwaka 1992, NEC imekuwa ikilaumiwa kuwa siyo
huru na kwamba inaegemea chama tawala.
0 comments:
Post a Comment