KWA UFUPI
Taarifa zinaeleza kuwa askari hao ambao hawakuwa kazini siku hiyo, walikwenda huko na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja na vipande saba vya pembe za ndovu.
IGP SAIDI MWEMA.
JUZI katika gazeti hili tulichapisha habari iliyokuwa ikieleza kifo cha askari wawili waliouawa na wananchi wilayani Karagwe, mkoani Kagera wakituhumiwa kujihusisha na ujangili.
Habari hiyo ilieleza kuwa askari hao waliokuwa katika gari binafsi aina ya Toyota Noah waliuawa na wananchi katika Kijiji cha Kashenye, Kata ya Rugu, wilayani Karagwe baada ya kukutwa na vipande saba vya meno ya tembo.
Askari hao ambao walikuwa wakifanya kazi katika Kituo kidogo cha Polisi, Benacco wilayani Ngara, wanadaiwa kwenda wilayani Karagwe kwa lengo la kutafuta ‘ulaji’ baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasiri wao kuwa kulikuwa na mfanyabiashara ambaye alikuwa akitafuta mteja wa kununua meno ya tembo.
Taarifa zinaeleza kuwa askari hao ambao hawakuwa kazini siku hiyo, walikwenda huko na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja na vipande saba vya pembe za ndovu.
Wakati wakiondoka kurejea Benacco, mmoja wa wananchi anadaiwa kupiga simu kwa wanakijiji wenzake akiwataarifu kuwa askari hao walikuwa majambazi ambao tayari walipora nyumbani kwake.
Tukio hilo limekuja ikiwa ni siku chache baada ya askari wawili pia wa mkoani Kagera, ambao ni maofisa wa upelelezi kukamatwa wilayani Serengeti, mkoani Mara wakiwa na vipande 17 vya meno ya tembo.
Tunachukua nafasi hii kutoa masikitiko yetu kwa hatua waliyoichukua wananchi ya kujichukulia sheria mkononi kuwaua askari hao.
Tunaamini kuwa hakuna mtu ambaye ana haki ya kumtoa mwenzake uhai, hata kama akiwa jambazi. Sehemu pekee ambayo mhalifu anatakiwa kufikishwa ni kwenye vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake.
Huu ni msimamo wetu na msimamo wa nchi kwamba utawala wa sheria lazima uheshimiwe.
Hata hivyo, tunachukua nafasi hii pia kuonyesha masikitiko yetu kwa Jeshi la Polisi kutokana na matukio mengi ya hivi karibuni ya askari wake kujihusisha katika vitendo vya uhalifu ikiwamo ujagili.
Tunalaani vitendo hivyo kwa sababu, polisi ambao wajibu wake ni kulinda raia na mali zao tunaposikia wanajihusisha na uhalifu, inatutisha. Lazima tueleweke kwamba hatusemi kwamba askari wote nchini ni wabovu, la hasha, kuna wengi ambao wanafanya kazi nzuri na tunawapongeza.
Matukio haya ya baadhi ya askari polisi kuhusika katika vitendo vya uhalifu ikiwamo kukamatwa na vipande vya meno ya ndovu, yanatoa picha kuwa kuongezeka kwa ujambazi nchini kunachangiwa na askari kujihusisha katika uhalifu.
Kitendo cha askari waliouawa kutoka katika eneo la kazi na kwenda kukamata mhalifu tena wakiwa wanatumia gari lao binfasi, ni wazi waliamua kwenda kutafuta ulaji kinyume na taratibu za kazi ambazo zinataka weledi na uadilifu wa hali ya juu.
Kutokana na mambo mengine ambayo yamekuwa yakiwahusisha polisi na vitendo viovu vya ujambazi, tunadhani ni wakati mwafaka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema kulifanyia mabadiliko makubwa jeshi hilo ikiwamo kuwaondoa kazini askari wote ambao wanalipaka matope ili kurudisha heshima yake mbele ya jamii.
Tunatambua uwezo mkubwa na uadifu wa hali ya juu wa IGP Mwema na tunaamini anaweza kubadilisha taswira ya jeshi hilo mbele ya jamii.
Haiwezekani Jeshi hilo liendelee kufanya kazi na askari wanaofanya kazi za polisi mchana, usiku wanabeba bunduki kwenda kufanya ujambazi dhidi ya wananchi ambao wameapa kuwalinda.
Ni kweli askari wetu wana changamoto za maisha ambazo zinawakabili, lakini kamwe hatua hii ya baadhi ya askari wachache kuamua kujihusisha na ujambazi haikubaliki.
Ni maoni yetu kwamba sasa IGP na vyombo vingine vya dola vitafuatilia mwenendo mzima wa baadhi ya askari ambao wanakiuka miiko ya kazi na kuwachukulia hatua za kisheria na nidhamu.
Ni maoni yetu kwamba sasa IGP na vyombo vingine vya dola vitafuatilia mwenendo mzima wa baadhi ya askari ambao wanakiuka miiko ya kazi na kuwachukulia hatua za kisheria na nidhamu.
0 comments:
Post a Comment