Mwandishi wa habari wa kujitegemea mkoani Arusha anayeandikia vyombo mbalimbali ikiwemo Zanzibar leo, Dira, Redio Sunrise pamoja na magazeti ya udaku Joseph Ngilisho maarufu kama “”Jb’”amefikishwa mahakamani kwa makosa matatu ya kuomba, kushawishi na kupokea Sh. 500,000 ikiwa ni sehemu ya rushwa ya Sh. Milioni 2 alizoomba.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Arusha, Hawa Mguruta, Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Rehema Mteta, alidai kuwa Ngilisho alifanya makosa hayo kwa siku na nyakati tofauti jijini Arusha.
Katika shitaka la kwanza, Rehema alidai kuwa mnamo Januari 12, mwaka huu, mtuhumiwa aliomba rushwa ya Sh. Milioni 2 kutoka kwa Phil Makini Kleruu ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa  Jumuiya ya Afrika Mashariki, ili asimwandike vibaya kwenye gazeti la Dira.
Alidai katika shitaka la pili, Januari 25 mwaka huu, Ngilisho aliomba hongo kutoka kwa Kleruu ili amsafishe kwenye gazeti hilo baada ya kumwandika.
Alitaja shtaka la tatu kuwa Januari 28, mwaka huu, Ngilisho alikamatwa akiwa amepokea Sh. 500,000 ikiwa ni sehemu ya Sh. Milioni 2 alizokuwa ameomba.
Hata hivyo, Ngilisho ambaye anatetewa na wakili Edmund Ngelemi, alikataa kufanya makosa hayo mbele ya mahakama hiyo.
Hakimu Mguruta aliaahirisha kesi hiyo hadi  Februari 12, mwaka huu itakapotajwa tena na kumruhusu Ngilisho kudhaminiwa na watu watatu, mmoja wao akiwa ni mtumishi wa umma.
Wakati wadhamini hao wakiwasilisha nyaraka zao za kumdhamini, Hakimu Mguruta alizikataa baada ya kuona zilikuwa zina hitilafu na aliwataka warudi  na kupata barua zingine zilizokuwa zimekamilika na hali hiyo ilimfanya Ngilisho kwenda mahabusu hadi pale dhamana yake itakaposhughulikiwa.
Nje ya mahakama hiyo baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wakiwemo waandishi wa habari mkoani Arusha walishikwa na butwaa mara baada ya mwandishi huyo kutinga mahakamani hapo huku akificha sura yake kwa kuhofia kupigwa picha.