BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NCHI YA JAMHURI YA AFRIKA YA KATI KUJADILIANA NA KUNDI LA MSETO LA WAASI.


Wanajeshi wa nchi za Afrika ya Kati (FOMAC) wakiwasili katika uwanja wa ndege mjini 

Bangui, December 31, 2012.

SERIKALI ya jamhuri ya Afrika ya Kati na kundi mseto la waasi nchini humo Seleka yaripotiwa wanakaribia kufanya mazungumzo ya amani  wiki ijayo kufuatia juhudi za upatanishi kutoka  kwa viongozi wa kikanda. Kundi la  wanajeshi wa nchi za Afrika ya Kati  liliweka udhibiti  nje ya mji mkuu Bangui  Jumatano,  na kuonya wote , serikali na waasi kuwa uhasama zaidi baina yao hutavumiliwa.

Takriban  wanajeshi mia tano wa nchi za Afrika ya Kati waliendelea kufanya doria nje ya mji wa Damara na kuweka  eneo lisiloruhusiwa wanajeshi wa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati wala wapiganaji wa kundi mseto la waasi linalojiita Seleka, na ambalo limedhibiti thuluthi moja ya nchi katika muda wa wiki tatu zilizopita. 

Mkuu wa jeshi hilo la kikanda linalojulikana kama FOMAC  jenerali  Jean Felix Akaga alisema majeshi yake hayataachia mji wa Damara  ulioko  kilomita 75 tu kutoka mji mkuu Bangui.

Anasema  ikiwa waaasi watashambulia mji wa Damara, itakuwa na maana wametangaza vita na kwamba wapo tayari kupigana   kundi la majeshi  ya kikanda kutoka nchi za Afrika ya Kati- FOMAC. 

Aidha Jenerali Akaga   alisema majeshi ya FOMAC yanazuia majeshi ya serikali  kuelekea kaskazini kupigana na wapiganaji wa kundi la Seleka. Alisema mji wa Damara  ni tulivu na thabiti.

Hatua hiyo imechukuliwa ili kuwaleta pamoja wawakilishi wa serikali na viongozi wa Seleka katika majadiliano ya amani  mjini Libreville, Gabon hapo Januari 10. Pande zote mbili zimesema zipo tayari kwa majadiliano.

Waasi wamekuwa mji wa Sibut, yapata kilomita 180 kutoka mji mkuu tangu Jumamosi. Na kwa mara nyingine wamesema wanasitisha hatua ya kuingia mji mkuu ili kutoa nafasi kwa majadiliano. Lakini katika siku za nyuma wamevunja ahadi zao wakisema kuwa wameshambuliwa na vikosi vya serikali.

Mji wa Damara Jumatano ulikuwa mtulivu, lakini kulikuwa na malori 32 yaliyojaa wanajeshi kutoka Chad wakiwa na silaha nzito. Wanajeshi hao ni sehemu ya wanajeshi wa kikanda FOMAC. Wengine wanatoka Jamhuri ya Congo na Gabon.

Watu wachache waliosalia huko Damara wanasema wana hofu kuu na kwamba  wamezificha familia zao  vichakani wakisubiri mzozo huo. Mkazi wa mji huo Andipassera Bertin anasema wamechoshwa na maasi. 

Anasema wake zao, watoto na jamaa zao wanataabika vichakani walipojificha. Anasema kuna baridi kali usiku na mbu wengi. Wakazi pia wanasema hospitali ya mji huo pamoja na soko zimefungwa na hawana namna ya kupata dawa wala chakula.

Kundi la Seleka ni mkusanyiko wa makundi manne ya waasi na yalianza mapigano dhidi ya serikali kati ya mwaka wa 2005 na 2006. Sasa wanadai serikali itekeleze kikamilifu mktaba iliyofikia pamoja nao mwaka wa 2007 na 2011 na wanamtaka rais Francois Bozize aondoke mamlakani. 

Waasi hao  wanasema walitakulipwa fedha kwa kusalimisha silaha zao na kushirikishwa  kwenye jeshi la kitaifa. Naye rais Bozize anasema yupo tayari kwa mazungumzo yasiyo na masharti kuunda serikali ya mseto.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: