BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAZIRI MUHONGO AWAKEJELI WANANCHI WA LINDI NA MTWARA, ASEMA HAWANA SAABABU YA GESI ASILIA IWANUFAISHE.

 ZITTO KWABWE, MURJI WAMJIBU KUWA WANAPINGA UFISADI.
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amewakejeli wakazi wa mikoa ya Mtwara na Lindi akisema kuwa hawana sababu ya kuandamana kutaka gesi asilia iwanufaishe kwa kuwa mikoa hiyo haina uchumi utakaoweza kutumia gesi hiyo.

Prof. Muhongo pia aliwakeji wanasiasa waliounga mkono maandamano ya wakazi hao, akiwemo mbunge wao wa Mtwara Mjini, akisema kuwa wanapaswa wajue kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara haina gesi inayomiliki.

Akizungumza na waandishi jana jijini Dar es Salaam, Prof. Muhongo, alisema Mtwara inazalisha asilimia 14 ya gesi yote inayozalishwa nchini, huku Lindi ikizalisha asilimia moja na kwamba hakukuwa na sababu ya kufanya maandamano kwa ajili ya suala hilo.

“Hiyo gesi inayowafanya wanasiasa wawashawishi wakazi wa Mtwara kuandamana haipo Mtwara wala Lindi, bali ipo katika mipaka ya Tanzania ndani ya kina kirefu cha bahari na kwa hilo kila Mtanzania ana haki ya kutumia,” alisema.

Aliongeza kuwa, kabla na baada ya uhuru, Tanzania ilikuwa ikitegemea mazao kwa ajili ya uchumi wa nchi na kwamba mikoa iliyokuwa inalima mazao ya biashara haikuwahi kuandamana kupinga pato linalopatikana kutumika kwa ajili ya mikoa mingine ikiwemo Lindi na Mtwara.

Alisisitiza kuwa, ni lazima Watanzania waelewe kuwa gesi asilia inatafutwa na kuchimbwa na wawekezaji wenye mitaji mikubwa na wataalamu wa teknolojia ya utafutaji na uchimbaji, hivyo ni lazima watu hao warejeshe mitaji yao.

Kuhusu madai ya wanasiasa kuunga mkono maandamano hayo, Waziri Muhongo, alisema wamekuwa vigeugeu kwa kuwa wengi wao walishirikishwa wakiwemo wabunge wa Lindi na Mtwara.

Alisema kuwa wabunge hao walipelekwa katika nchi za Trinidad, Malaysia na China kwa ajili ya kujifunza masuala ya gesi asilia na walilipwa posho na nauli.

Waziri Muhongo alibainisha kuwa, ni jambo la kusikitisha kuona wakazi wa Mtwara wakiandamana kwa ajili ya gesi wakati walipa kodi wa Tanzania hawajaandamana kwa ajili ya rasilimali zinazotoka maeneo mengine kwenda kutumika Mtwara.

Alitolea mfamo umeme wa Kidatu aliosema upo katika gridi ya taifa na kwamba unanufaisha mpaka mikoa ya Mtwara na Lindi.
Hata hivyo, katika hatua ya kushangaza, waziri huyo aligeuka mbogo pale waandishi walipotaka ufafanuzi wa mambo kadhaa ambapo alijibu kwa kifupi na kwa kuwashushua.

Alipoulizwa kama kulikuwa na ushirikishwaji wa kutosha wa wananchi, na kwanini ufafanuzi anatolea kupitia vyombo vya habari badala ya wananchi wenyewe wa Mtwara kabla ya kuandamana, Waziri Muhongo alijibu kuwa mwandishi yuko nyuma ya wakati katika kujua mambo yanayoihusu serikali.
ZITTO KABWE.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) ambaye alikuwa mmoja wa wanasiasa waliounga mkono maandamano hayo, alimjibu Waziri Muhongo akisema kuwa anashindwa kuelewa kuwa wananchi wa Mtwara wana haki ya kufanya hivyo na kuona matumizi bora ya matumizi ya gesi.

“Huyo anasema kuna siri kwa wanasiasa wanaounga mkono, ni kweli tuna siri, nayo ni kupinga uporaji wa rasilimali za nchi, siri iliyopo ni kupinga ufisadi, na watu wa Mtwara wana madai ya msingi na lazima wasikilizwe,” alisema.
 Nape akizungumza na mbunge wa Mtwara mjini, Hasnain Mohammed Murji.
 
Naye Mbunge wa Mtwara Mjini, Husnain Mohamedi Murji (CCM), alisema anashukuru kwa ziara hiyo ya mafunzo aliyoitaja waziri kwa kuwa imemfumbua macho na ndiyo maana yupo pamoja na madai ya wananchi.

“Kwanza namshukuru waziri kwa kunipeleka kujifunza Trinidad na Tobago, nilichojifunza ni kwamba wenzetu wa huko wana uzoefu wa miaka 100, na wanawajali watu wa eneo husika ambako rasilimali inatoka tofauti na sisi tunavyotaka kuwafanyia wakazi wa Mtwara,” alisema.

Aliongeza kuwa, wananchi wa Mtwara ni lazima wajue watanufaika vipi na rasilimali ya gesi kwa kile alichoeleza kuwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia alipofika mkoani humo katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliwaambia hawana chao katika mrabaha mzima wa gesi.

Murji aliongeza kuwa, kazi ya mbunge ni kusikiliza mawazo ya wananchi na alichoeleza ndio msimamo wa wananchi, huku akisisitiza kuwa Waziri Muhongo amedanganya kwani wakazi wa Mtwara hawajawahi kunufaika na umeme wa kutoka nje ya Mtwara.

Alihoji ulazima wa serikali kujenga mtambo wa gesi Kinyerezi jijini Dar es Salaam na kuacha kuzalisha umeme huo mjini Mtwara na kisha uunganishwe katika gridi ya taifa.
CHANZO:www.freemedia.co.tz
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: