Rais Jakaya Kikwete
---
Na Ikulu-Dar es Salaam
Rais Kikwete anawapa pole nyingi wafiwa, anawapa pole nyingi walioumia na wanaoendelea kupatiwa matibabu baada ya kubanwa katika kifusi, wakiwamo watoto wadogo ambao walikuwa wanacheza chini ya jengo hilo la ghorofa 16 wakati lilipoporomoka asubuhi ya jana huku likiendelea kujengwa.
Rais Kikwete amewapongeza na kuwashukuru wananchi wote walioshiriki na wanaendelea kushiriki katika zoezi la uokoaji pamoja na vyombo na taasisi za umma na Serikali zinazoshiriki katika zoezi na kazi hiyo ya uokoaji.
Amewataka waendelee na jitihada hizo ili kama kuna watu ambao bado wamebanwa kwenye kifusi waweze kuokolewa ili wapatiwe matibabu, na kama watakuwa wamepoteza maisha basi miili yao ipatikane na iweze kupewa mazishi ya heshima yanayostahili mwanadamu.
Wakati alipotembelea eneo la tukio hilo, Rais Kikwete ametoa maelekezo mahsusi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Mheshimiwa Saidi Mecky Sadik pamoja na Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi ya Dar es Salaam, Kamanda Suleiman Kova.
Rais amewataka kuhakikisha kuwa Mjenzi wa jengo hilo ambaye ndiye anakuwa anajenga jengo hilo, Mhandisi Mshauri aliyekuwa anasimamia ujenzi wa jengo hilo, Mhandisi wa Jiji la Dar es Salaam ambaye alitoa kibali cha ujenzi na ndiye Mkaguzi wa ujenzi pamoja na mwenye Jengo wanapatikana haraka na kuwajibishwa ipasavyo.
0 comments:
Post a Comment