MBOWE AMBANA SPIKA AELEZE KANUNI ILIYOTUMIKA.
http://www.freemedia.co.tzKiongozi
wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe.
Utata huo ulibainika jana wakati Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe, alipoomba mwongozo wa Spika Anna Makinda, kutaka kujua kanuni aliyotumia Ndugai wakati hakuna kanuni iliyomruhusu kutoa adhabu hiyo.
Baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili jana pia walihoji kifungu kilichotumika hata kama wabunge hao walikosea.
Miongoni mwa waliohoji adhabu hiyo, wapo baadhi ya wabunge wa CCM ambao hawakupenda kutaja majina yao, wakisema kuwa uamuzi wa Naibu Spika ulitawaliwa na jazba za kibinadamu badala ya kufuata kanuni zinazoliongoza Bunge.
Katika mwongozo wake jana kwa Spika Makinda, kiongozi huyo wa kambi ya upinzani alihoji kifungu kilichotumika kuwaadhibu wabunge wake.
Mbowe alisema juzi wakati Bunge lilipokuwa katika kipindi chake cha jioni, wabunge sita wa CHADEMA waliotolewa nje kwa maelekezo ya Naibu Spika, Job Ndugai.
Aliwataja wabunge waliotolewa kuwa ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Haghness Kiwia (Ilemela), Ezekia Wenje (Nyamagana), Godbless Lema (Arusha Mjini), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) na Pete Msingwa (Iringa Mjini).
“Na wabunge hawa walipotolewa, walipewa vile vile adhabu ya kutohudhuria vikao vitano vya Bunge, adhabu iliyotolewa papo kwa papo na Naibu Spika.
“Kwa mujibu wa kanuni zetu, kanuni inayompa Naibu Spika au Spika mamlaka ya kumtoa mbunge kwa siku tano ni kanuni ya 73 ya kanuni ndogo ya tatu ambayo inahusu mbunge ambaye atashindwa kutoa vielelezo vya aidha kusema uongo ambayo inasema hivi:
“Endapo mbunge yeyote atatakiwa kuthibitisha maneno aliyoyasema na hadi kufikia mwisho wa muda aliopewa, ameshindwa kutoa uthibitisho huo, Spika anaweza kumsimamisha mbunge huyo asihudhurie vikao vya Bunge visivyozidi vitano,” alinukuu.
Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti wa CHADEMA, alisema yaliyotokea bungeni juzi ni sintofahamu kati ya wabunge na kiti cha Spika ambapo katika mambo ya msingi CHADEMA ilitegemea kifungu cha nne cha kanuni za Bunge, kifungu kidogo cha kwanza kingetumika.
Kifungu kinasema: “Spika anaweza kutaja jina la mbunge kwamba amedharau mamlaka ya Spika na kisha kupeleka jina hilo kwenye Kamati ya Haki na Maadili ya Bunge.
“Ikiwa kwa maneno au vitendo, mbunge huyo anaonyesha dharau kwa Spika au atafanya kitendo chochote cha makusudi cha kudharau shughuli ya Bunge au mbunge yeyote anayeongoza shughuli hiyo.”
Kutokana na kanuni hiyo, Mbowe aliomba mwongozo wa Spika kutaka kujua wabunge hao walitolewa kwa kanuni gani na ni lini wataweza kurejeshewa haki yao ya kurejea ndani ya Bunge.
Vituko vya juzi
Baadhi ya askari walioamriwa kuingia ndani ya Bunge, walisema hawakuwa tayari kumtoa Lissu kwa nguvu ndio maana walitumia muda mrefu kutimiza agizo hilo.
Askari hao walisema hofu yao ilikuwa ni usalama wa Waziri Mkuu kwani endapo vurugu zingeibuka, angekuwa katika wakati mgumu kiusalama.
Baada ya Lissu na wabunge wenzake kutoka nje ya ukumbi chini ya ulinzi, askari hao walipata wakati mgumu kuwatoa nje ya eneo la Bunge.
“Tulipanda juu hadi kwenye ofisi ya Lissu, alipofika alikaa chini, akafungua kompyuta yake, baadaye akaizima wala hakuwa na haraka na sisi wakati huo tulibaki tumesimama tu.
“Baadaye aliizima, akachomoa waya na kuziingiza kwenye begi lake, kisha alisimama taratibu na kuondoka kama vile hakuna jambo lililotokea,” alisema askari huyo.
Wenyewe wanena
Lema alisema:
“Nimepokea kwa furaha adhabu hii kwa sababu imetokana na kupigania haki na ukweli ndani ya Bunge. Kwa hiyo adhabu hii kwangu ni baraka.”
Alisema uonevu wa wazi uliofanywa na Naibu Spika, Job Ndugai, baada ya muda kidogo Tanzania itashangilia ushindi mkubwa. Kwamba Watanzania watafurahia vijana wao na watoto wao walioshinda hofu.
“Ushahidi nilioombwa kuhusu mwenyekiti wa CCM kuwa mwasisi wa udini ninao, tena wa uhakika wa nguvu na imara na niko tayari kuutoa mbele ya Bunge kwa kuwa nilitoa maneno hayo mbele ya Bunge.
“Sitapeleka tena ushahidi wangu vichochoroni kwa kuwa nilipeleka ushahidi wangu kwa Spika kuhusu uongo wa Waziri Mkuu, walipiga chenga hadi wakanivua ubunge,” alisema.
Lema alidai kuwa ametumiwa meseji za vitisho kwamba wangelimuonyesha tena mahakamani, lakini akasema wafanye wafanyavyo ila moyo wake una furaha kuwa amesema yale ambayo wengine wameogopa kuyasema.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, alisema: “Bunge letu lina matatizo, halina mwelekeo. Job Ndugai anajidai yeye ndiye kiongozi wa serikali.”
Alisema kama Ndugai ana sifa hizo na anajiandaa kuwa Spika wa Bunge lijalo, anamwomba Mungu asiwe mbunge katika Bunge hilo.
“Tusi lililotolewa na Peter Serukamba wa CCM, lilikuwa kubwa kuliko matusi yote yaliyowahi kutolewa ndani ya Bunge katika mabunge ya Jumuiya ya Madola.
“Hili lilihitaji adhabu, lakini kitendo cha Naibu Spika kumtimua Lissu ambaye alikuwa anafuata kanuni ni cha kusikitisha sana,” alisema.
Mbilinyi alisema wananchi wa Mbeya Mjini hawakumtuma kushangilia bungeni.
Kwa upande wake Mchungaji Msigwa alisema: “Adhabu hii ni ya hovyo kwa sababu haikufuata taratibu; wamegeuza Bunge kama sehemu ya serikali.”
Alifafanua kuwa kama angepata adhabu iliyofuata kanuni asingekuwa na shida, angeipokea kwa furaha.
“Naibu Spika ana jazba, anapaswa apate mafunzo ya jazba zake. Viongozi wa Bunge wamejaa u-CCM zaidi kuliko utaifa. Binafsi sitajali kufukuzwa, ninachotaka haki itendeke,” alisema.
Mbunge wa Ilemela, Kiwia, alisema adhabu waliyopewa ni kinyume cha kanuni.
“Adhabu hiyo anapaswa apewe mtu aliyesema uongo na kushindwa kuthibitishwa, pamoja na hayo kanuni zifanye kazi kwa wabunge kwa usawa,” alisema.
Kiwia aliongeza kuwa kanuni hazipaswi kuwaona wabunge wengine wana haki na wengine hawana; kwamba hoja za msingi zijibiwe, maamuzi bungeni yasifanyike kwa mabavu.
Naye Lissu ambaye ni mwanasheria kitaaaluma, alisema hajui ni kanuni gani iliyotumika na kumwadhibu na kwa kosa gani.
0 comments:
Post a Comment