BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

BUNGE HALIKALI.

http://www.mtanzania.co.tz

VURUGU kubwa zilitokea bungeni mjini Dodoma jana usiku. Dalili za vurugu hizo zilianza kujitokeza wakati Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka wa fedha 2013/14.

Akichangia hoja hiyo, Mwigulu alikishutumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwamba kinaeneza udini ingawa viongozi wa chama hicho hawataki kukubali.

“Kwanza nataka kusema kwamba suala la udini ni jambo geni kwa Watanzania. Wote hapa tunajua kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania alikuwa Mkristo alitoka CCM, wa pili alikuwa Muislamu, alitoka CCM, wa tatu alikuwa Mkristo alitoka CCM na wa nne ni Muislamu ametoka CCM, na wote hawa walikuwa wenyeviti wa CCM.


“Sasa bado hamjaelewa tu nani kaja na udini? Rais wetu amekuwa wa kwanza kukemea udini, lakini Dk. Slaa (Dk. Wilbrod Slaa, Katibu Mkuu wa Chadema) akifanya mikutano yake badala ya kukusanya wanachama amekuwa akifanya mikutano na viongozi wa dini fulani,” alisema.


SUSAN KIWANGA AINGILIA.
Wakati Mwigulu akitaka kuendelea, Mbunge wa Viti Maalum, Susan Kiwanga (Chadema) aliomba kutoa taarifa baada ya kutoridhishwa na kauli za Mwigulu.

Alipoanza kuzungumza alisema Chadema siyo chama cha udini kwa kuwa yeye ndiye alikuwa mratibu wa kampeni za mgombea wa urais wa chama hicho mwaka 2010 na yote aliyoyasema Mwigulu ni ya uongo.

Kiwanga alisema yeye ndiye aliyeandaa mkutano uliofanyika mkoani Singida na haukuwa wa viongozi wa dini bali ulikuwa wa wanachama wa Chadema na viongozi wa chama hicho.


MWIGULU AKATAA TAARIFA
Kiwanga alipomaliza kuzungumza, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alimuuliza Mwigulu kama anaikubali taarifa hiyo au anaikataa ambako Mwigulu alisema haikubali.

“Viongozi wa dini ndiyo waliokataa mkutano huo na ndiyo maana hawakwenda kuhudhuria kwa sababu waliona ni upuuzi,” alisema Mwigulu.


LISSU AOMBA UTARATIBU.
Wakati Mwigulu akijiandaa kuendelea kuchangia, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) alisimama na kuwasha kipaza sauti kuomba kuhusu utaratibu.

Hata hivyo nafasi hiyo hakuipata baada ya Naibu Spika kumgomea kwa kile alichosema kuwa amezungumza sana na kwamba anatakiwa akae ili Mwigulu aendelee kuchangia.

“Lazima uwe mvumilivu, wewe wakati unachangia wenzako walikuwa wanakusikiliza, haya ndiyo matatizo ya ugeni wa kuingia katika Bunge kwa mara ya kwanza,” alisema Ndugai.


VURUGU ZAANZA
Naibu Spika aliposema hayo, wabunge wa Chadema walianza kuguna na kumzomea kama ishara ya kutokubaliana na maneno yake na hapo ndipo vurugu zilipoanza.

Vurugu zilipozidi, Naibu Spika aliamuru Lissu atolewe nje ya Ukumbi a wa Bunge na askari wa Bunge.

Hali hiyo ilizua tafrani bungeni kwa kuwa baadhi ya wabunge wa Chadema walimzingira Lissu na kugoma asiguswe na askari yeyote.

Waliomzingira walikuwa ni Highness Kiwia (Ilemela), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Hezekiah Wenje (Nyamgana), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Suzan Kiwanga (Viti Maalum).

Kutokana na tukio hilo, askari wa Bunge wapatao wanne waliofika sehemu alipokaa Lissu, walishindwa kumtoa na hawakufanikiwa kumfikia kwa sababu alikuwa amezingirwa na wabunge wenzake.

Pamoja na kumzingira, wabunge hao walikuwa wakisema, “hatoki mtu hapa.

“Huo ni ubabe, tumesema hatoki mtu hapa, mnatuonea kwani kuomba utaratibu ni kosa?” zilisikika sauti za wabunge hao.

Baada ya askari hao kushindwa kumtoa Lissu, polisi waliokuwa nje ya Bunge ambao kwa mujibu wa kanuni hawaruhusiwi kuingia bungeni, walilazimika kuvunja kanuni na kuingia bungeni.

Wakati huo Mbilinyi (Sugu) alionekana kushikana shati na mmoja wa askari wa Bunge baada ya askari huyo kumshika shingoni akitaka kumsogeza pembeni ili amchukue Lissu.

Wakati vurugu hizo zikiendelea, askari anayehusika kuondoa fimbo ya Bunge (siwa), alikwenda kuiondoa lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na sababu ambazo hazikueleweka.

Baada ya purukushani hizo, baadaye wabunge hao wa Chadema walikubali Lissu atoke kwa hiari yake bila kuguswa na askari yeyote.

Wakati Lissu akitoka nje akiongozana na wabunge waliokuwa wakimlinda, Ndugai alitangaza kuwafungia vikao vitano vya Bunge, Lissu, Lema, Kiwia, Wenje na Msigwa.

Baada ya kutoa adhabu hiyo Ndugai aliahirisha Bunge.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: