BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

GODBLESS LEMA KIZIMBANI LEO.

POLISI WAHAHA KUIMARISHA ULINZIMJINI ARUSHA, LENGO KUUHAMI MKUTANI WA MARAIS WA JUMUITA EAC.
http://www.mtanzania.co.tz

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbles Lema (CHADEMA), leo anatarajiwa kufikishwa mahakamani, kutokana na tuhuma za uchochezi. Mbunge huyo alikamatwa siku ya Ijumaa na kuwekwa rumande kwa amri ya Mkuu wa Mkoa wa wa Arusha, Magesa Mulongo, huku wadau mbalimbali wa masuala ya sheria wakikosoa ukamatwaji wake.

Kwa mujibu wa Mulongo, vurugu zilizotokea wiki iliyopita katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), zilisababishwa na Lema aliyewachochea wanafunzi wa chuo hicho waliokuwa wakipinga kuuawa kwa mwenz
ao, Henry Kago (22) aliyekuwa nje ya chuo.

Kukamatwa kwa Lema kumekuja siku moja baada ya mbunge huyo kudai kutumiwa ujumbe wa vitisho kutoka kwa mkuu huyo wa mkoa.


Lema aliwaonesha waandishi wa habari ujumbe huo mfupi wa simu ya kiganjani aliotumiwa na Mulongo, akimtishia kuwa atamfungulia kesi yoyote anayotaka.

Ujumbe huo ulisomeka; “Umeruka kihunzi cha kwanza, nitakuonesha kuwa mimi ni Serikali, ulikojificha nitakupata na nitakupa kesi ninayotaka mimi,” ulisema ujumbe huo.

Mulongo amekanusha kutuma ujumbe huo, akieleza masikitiko yake kwamba, wanafunzi wa chuo hicho walimzomea katika vurugu hizo na kulipiga gari lake kwa mawe.

Hata hivyo wakati wafuasi wa Chadema wakitarajiwa kujitokeza kwa wingi mahakamani, Jeshi la Polisi limeonekana kuhaha kupanga mbinu za kuimarisha ulinzi katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo.

Hatua hiyo, inatokana na mji wa Arusha tangu juzi jioni, kupokea marais watano wa nchi wa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanaokutana katika vikao vya kawaida.

Kutokana na wingi wa viongozi hao, polisi wamelazimika kugawanywa katika makundi mawili, huku wengine wakitolewa mkoani Kilimanjaro kwenda kuongeza nguvu.

Taarifa kutoka mkoani humo, zinasema wafuasi wa CHADEMA leo wamepanga kujitokeza kwa wingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, kwa ajili ya kusikia mbunge wao anasomewa mashitaka gani.

Wafuasi hao, ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini, walisema kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya mahakama, ni ujumbe tosha kwa Serikali ya CCM na viongozi wa nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambao wanakutana mjini humo tangu juzi.

Baadhi ya wabunge wa chama hicho na uongozi wa Chadema mkoani humo, wamezungumzia kukamatwa kwa Lema wakisema hizo ni hila na chuki za kisiasa dhidi ya viongozi wa chama chao.

Ulinzi kuimarishwa kila kona

Taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, zinasema jeshi hilo, limejipanga kuimarisha ulinzi katika mji wa Arusha na vitongoji vyake, kama njia ya kuzuia vurugu za aina yoyote zinazoweza kujitokeza.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya jeshi hilo, kililiambia MTANZANIA kuwa muda wa mapumziko ya mwisho wa wiki, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alikuwa na vikao vizito na askari ikiwa ni njia ya kuimairisha usalama dhidi ya viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na tukio la Lema kupelekwa mahakamani.

“Tangu Jumamosi, Kamanda Sabas alikuwa anajipanga na vijana wake namna ya kuweza kudhibiti kila aina ya vurugu ambayo inaweza kutokea kesho (leo), wamejipanga vizuri wapo askari wa kikosi cha mbwa, farasi na askari wa kawaida,” kilisema chanzo chetu.

“Wana mkutano mkubwa ambao unafanyika katika hoteli ya Ngurdoto, ambapo marais wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na watendaji wa ngazi za juu wanakutana, itakuwa aibu kubwa kama kutatokea vurugu kubwa mkoani Arusha,” kilisema chanzo hicho.

Mdee, Nassari kukutana na RC leo

Pamoja na kuwepo kwa mvutano huo unaoonekana wa kisiasa, wabunge wawili wa CHADEMA, Joshua Nassari (Arumeru Mashariki) na Halima Mdee (Kawe), leo wamepanga kuonana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo.

Wabunge hao, wamesema kuwa lengo la kufanya mazungumzo na RC Mulongo, ni kuhusiana na kilichotokea IAA, hali iliyosababisha kukamatwa kwa Lema.

“Leo tunatarajia kukutana na kufanya mazungumzo ya kina na Mkuu wa Mkoa Mulongo na tayari nimeshafanya mawasiliano, ambapo tutazungumza kuhusiana na hali ya kisiasa kwa sasa katika mkoa wetu wa Arusha,” alisema Nassari.

Chadema yatangaza mgogoro na RC

Wakati hayo yakiendelea, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza mgogoro na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, huku kikisema kitaendesha kazi ya kumzoa kila atakapokuwa anafanya shughuli za kiserikali.

Kauli hiyo, imetolewa na Katibu wa CHADEMA, Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, ambapo alisema kuwa wafuasi wa chama hicho wataendelea kumzomea Mulongo kila watakapomwona, hadi pale atakapobadilika kifikra dhidi ya viongozi wa chama hicho.

“Tutaendelea kumzomea kila kona ya Arusha hadi pale atakapobadilika kimwenendo, maneno na vitendo kuhusiana na uhalali wa CHADEMA na viongozi wake katika uongozi wa umma waliokabidhiwa kisheria,” alisema Golugwa.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: