UPELELEZI
WA SAKATA LAKE WATIA HOFU.
http://www.freemedia.co.tz
JUHUDI
za Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuwanasa watuhumiwa
waliomtesa na kumuumiza vibaya Mwenyekiti wa Jukwa la Wahariri Nchini (TEF),
Absalom Kibanda, huenda zikagonga mwamba kutokana na utata uliopo, Tanzania
Daima limedokezwa.
Taarifa
za ndani ya jeshi hilo zinadai kuwa suala hilo limeanza kuumiza vichwa huku
baadhi ya askari wa chini wakikerwa na tabia ya wakubwa wao kusuasua
kulimaliza.
Kibanda
ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New habari (2006) Ltd,
wachapishaji wa magazeti ya Rai, The African, Mtanzania, Bingwa na Dimba,
alivamiwa Machi 3, mwaka huu, nyumbani kwake kisha kupigwa nondo kichwani,
kutobolewa jicho, kunyofolewa ukucha, kung’olewa meno mawili na kukatwa kidole.
Wakati
Kibanda akiendelea kupata matibabu nchini Afrika Kusini, mwenendo wa uchunguzi
wa sakata lake umezua mashaka kutokana na mlolongo wa matukio yanayoibuliwa ili
kujaribu kuzima mjadala huo.
Vyanzo
vyetu kutoka ndani ya jeshi la polisi ambalo linaendelea kupeleleza tukio hilo,
vilisema kuwa baadhi ya askari hawaridhishwi na kasi ndogo inayoonyeshwa katika
kulipatia ufumbuzi badala yake jamii imekuwa ikidhani linahusika.
“Suala
hili kwa sasa limekuwa gumu, tangu Kibanda atekwe hadi sasa, makachero
tunaumiza vichwa, ingawa hatuwezi kusema wazi kuwa tumeshindwa kuwabaini watu
hao.
“Lakini
ukweli unajidhihirisha kuwa hicho kikundi kilichomtesa Kibanda kina wataalamu
wa kazi hiyo na wala si majambazi au vibaka wa kawaida.
“Haya
ni mateso ya watu maalumu wanaojua kutesa na hayo hufunzwa kwa watu maalumu
kwenye vyuo maalumu,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo
hicho kiliongeza: “Inasikitisha kiasi fulani watu wanataka kujaribu kuanza
kuhusisha suala la Kibanda na suala la watuhumiwa waliokamatwa kwa masuala
mengine kabisa ya kisiasa.
“Hata
sasa huyu ambaye tumemshikilia hapa, zote hizi ni siasa tu, watu wangependa
mabega yao yapendeze, hali kama hii ikiendelea kukua ndani ya jeshi
itasababisha tudharaulike.”
Baadhi
ya vyombo vya habari navyo vinadaiwa kutumiwa kulififisha suala la Kibanda kwa
kuibua mijadala ya kushambuliana vyenyewe kwa vyenyewe hatua inayoonekana
kuwepo kwa ajenda ya siri ndani yake.
“Ni
kama vile haiwezekani, kusema kuwa tangu Kibanda ateswe eti hakuna hata
mtuhumiwa mmoja aliyetiwa mbaroni, hata na viongozi wetu wa jeshi la polisi
ukiwauliza, wanaanza kusema timu iliyoundwa kupeleleza suala la Lwakatare
(Wilfred) na Ludovick (Joseph) litashughulikia pia suala la Kibanda.
“Haya
mambo mawili ya Kibanda na Dk. Stephen Ulimboka kweli yanatufedhehesha sana,
tunaonekana tunafanya siasa badala ya taaluma ya ukachero, hapa kuna baadhi ya
wakubwa wanalindwa; sisi tunapelekeshwa tu,” kilisisitiza chanzo chetu.
Zikiwa
zimetimia siku 26 tangu kuteswa kwa Kibanda, tume ya polisi ya wataalamu
iliyoundwa na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Suleiman Kova,
haijamkamata mtuhumiwa hata mmoja huku kamanda huyo akikataa kuzungumzia
maendeleo ya uchunguzi.
Tukio
la Kibanda limekuwa likifananishwa na lile la Dk. Ulimboka kutokana na
utaaalamu uliotumika kuwatesa kufafana ingawa yalitendeka maeneo tofauti.
Dk.
Ulimboka ambaye alitekwa na watu wasiojulikana usiku wa Juni 26, mwaka jana,
hadi leo ni mtu mmoja amefunguliwa mashtaka baada ya kujisalimisha kanisani
akidai kuhusika na tukio hilo.
Mshtakiwa
huyo, Joshua Mulundi, awali ilidaiwa na uongozi wa kanisa alikojisalimisha kuwa
alikuwa na matatizo ya akili lakini jeshi la polisi limekuwa likisema upelezi
wa tukio zima pamoja na uchunguzi wa afya yake unaendelea.
0 comments:
Post a Comment