BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MWANDISHI WA MWANANCHI AFA AJALINI TANGA

Kwa ufupi
“Semdoe alifanya kazi bila kuchoka, alikuwa anafanya kazi nyingi kwa wakati mmoja, bila manung’uniko, aliweza kufanya habari lakini wakati huohuo alikuwa akiandika ripoti maalumu,” alisisitiza Mfalila. 
http://www.mwananchi.co.tz

HANDENI:  
MWANDISHI wa Habari wa Magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga, Hussein Semdoe, (37) pamoja na mwenzake wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Khamis Bwanga, (53) wamefariki katika ajali ya gari iliyotokea jana katika Kijiji cha Misima, Handeni.

 Marehemu Hussein Semdoe akiwa kazini. Picha hii ilipigwa mwishoni mwa wiki Kwamsisi wilayani Handeni mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo iliyothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe, mwingine aliyefariki katika ajali hiyo ni Kamishna Mwandamizi wa Uhamiaji Wilaya ya Handeni, Mariam Hassan.
Kamanda Massawe alisema ajali hiyo ilitokea saa 3:00 asubuhi wakati wakitoka Handeni kwenda Misima kuhudhuria siku ya upandaji miti.
Katika ajali hiyo, watu watatu walijeruhiwa akiwemo dereva wa gari hilo, Mtawala Makasi, Sajent Athanas Paul (Mshauri wa Mgambo Wilaya) na Natolini Mlowe ambaye ni Ofisa Misitu wa Wilaya ya Handeni. Majeruhi hao wamelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo.
Kamanda Massawe alisema chanzo cha ajali ni kupasuka kwa tairi la kushoto la gari ambalo liliruka umbali mrefu na kupindukia porini. Bwanga alirushwa kichakani na kufariki papo hapo wakati Mariam alifia ndani ya gari. Semdoe alifia Hospitali ya Wilaya Handeni alikopelekwa kwa matibabu.
Akizungumza jana jioni, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu alisema ofisi yake imepokea kwa masikitiko vifo hivyo na kuongeza kuwa maziko ya Semdoe ambaye ameacha mjane na watoto wanne, yatafanyika leo saa nane mchana. Bwanga atapelekwa Muheza.

Kaimu Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Bakari Machumu alisema: “Tumesikitishwa sana na kifo cha ghafla cha mwandishi mwenzetu ukizingatia alikuwa katika jitihada za kikazi.”

Machumu alitoa pole kwa familia ya marehemu na kuiomba iwe na subira hasa katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, huku akiwapa pole waandishi wote wa Mwananchi Mkoa wa Tanga, pamoja na wafanyakazi wote wa MCL.
Kwa upande wake, Mhariri wa Habari wa Gazeti la Mwananchi, Samson Mfalila, alisema Semdoe ameacha pengo kubwa katika chumba cha habari kwani alikuwa mwepesi na mtu aliyejituma katika kazi.
“Semdoe alifanya kazi bila kuchoka, alikuwa anafanya kazi nyingi kwa wakati mmoja, bila manung’uniko, aliweza kufanya habari lakini wakati huohuo alikuwa akiandika ripoti maalumu,” alisisitiza Mfalila.
Mhariri Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd, Dennis Msacky alisema: “Nimepokea kwa mshituko kifo cha Semdoe kwani alikuwa kiungo kikuu katika kuhabarisha umma kinachoendelea wilayani Handeni hasa kwa wananchi wa kawaida.
“Hivi karibuni aliandika ripoti maalumu kuhusu njaa Handeni na tuliipa nafasi yake,ni pigo kubwa si kwa Mwananchi tu bali tasnia nzima ya habari.”

Mhariri wa Habari za Mikoani, Tausi Mbowe, alisema Semdoe alikuwa msaada mkubwa katika Mkoa wa Tanga hasa Wilaya ya Handeni.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: