KAULI YAKE BUNGENI YAZUA BALAA
http://www.freemedia.co.tz
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu),
Stephen Wassira.
KAULI ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu),
Stephen Wassira kudai kuwa Idara ya Usalama wa Taifa haiwezi kumtesa
Kibanda kwa kuwa hana umaarufu kisiasa nchini, imeibua mjadala mkali,
Tanzania Daima Jumapili limebaini.Juzi wakati akihitimisha hoja ya hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/ 2014, Wassira aliitetea Idara ya Usalama wa Taifa dhidi ya tuhuma zinazowahusu baadhi ya watendaji wake kuhusika katika matukio kadhaa ya utekeji na utesaji wa raia.
Wassira alisema haiwezekani kwa watumishi wa idara hiyo kujihusisha na matukio hayo na kueleza mafanikio mbalimbali ambayo imeliletea taifa.
Alihoji sababu za kulihusisha tukio la kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Absalom Kibanda na idara hiyo na kuhoji; ‘kwani yeye ni nani ?.’
Katika kuali hiyo ambayo imeibua mjadala, Wassira alisema haiwezekani idara hiyo ikahusika kwa kuwa Kibanda hana umaarufu katika siasa za Tanzania, na kwamba labda wangekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa angeelewa.
Kibanda alivamiwa akiingia nyumbani kwake Mbezi Juu jijini Dar es Salaam usiku wa Machi 6 mwaka huu na watu wasiojulikana, na kushambuliwa vibaya kwa kupigwa nondo kichwani, kutobolewa jicho la kushoto, kung’olewa ukucha, meno mawili na kukatwa kidole.
Kauli ya Wassira imepokelewa kwa mtazamo hasi na watu mbalimbali katika jamii, huku wengi wakisema kuwa hiyo ni ishara kwamba chombo hicho kinahusika na vitendo hivyo, lakini kwa kundi fulani la watu.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, mwanasheria maarufu nchini, Mabere Marando alisema mjadala huo unatokana na hoja aliyoanzisha yeye ya kuwataja watu wa Usalama wa Taifa kuwa wanahusishwa na utekaji na utesaji.
Marando ambaye pia ni ofisa wa zamani wa idara hiyo, alifafanua kuwa ni vema Wassira ashauri sera za Idara ya Usalama zifanyiwe mabadiliko, waache kulinda heshima ya chama badala yake walinde taifa.
“Kazi za usalama ni kugundua mapema na kutoa taarifa habari zinazohusu serikali kupinduliwa, kusaidia serikali katika ujasusi wa uchumi ili nchi iendelee na mwisho kabisa ni kushauri serikali kuhusu hali ya kisiasa nchini.
Wala sio kupambana na wanasiasa au waandishi wa habari,” alisema.
Marando aliongeza kuwa Usalama wa Taifa sasa unafanya kazi za usalama wa raia ambazo ni za polisi kimsingi.
Kwamba Usalama wa Taifa huwa hawakamati, lakini siku hizi wanakamata.
“Sasa kama hawa wakifanya hivi polisi watafanya kazi gani? Tunashindwa kutofautisha kazi za usalama wa taifa na usalama wa raia,” alisema.
Katibu wa TEF, Neville Meena alisema kuwa Wassira ni kielelezo cha ulevi wa madaraka.
Anaona kuwa wanasiasa ndio watu zaidi kuliko wengine.
Alisema kwa kauli ile pengine ndiyo maana uchunguzi wa suala la Kibanda haufanyiki wala hakuna taarifa rasmi ya polisi iliyotolewa tangu atekwe na kuteswa.
“Tunafurahi kwa kuwa tumepata mawazo ya watawala na kauli ya Waziri huyu wa Nchi, Ofisi ya Rais pengine ndiyo msimamo wa serikali maana alisema bungeni.
“Huyu anatoka Ofisi ya Rais, tena anashughulikia mahusiano.
Anapotoa kauli hii zikiwa zimefika siku 45 tangu Kibanda atekwe na kuteswa, mauaji au mateso kama hayo hayataisha katika nchi kwa kuwa sisi wengine sio watu kwa mujibu wa Wassira. Kauli hii ni mbaya na haina afya,” alisema Meena.
Mwandishi nguli wa habari nchini na mshauri wa masuala ya habari, Ndimara Tegambwage alisema; “Kwanza tunafurahi kwa kuwa Wassira amethibitisha kuwa wana usalama wanawaandama watu na mara zingine kuwadhuru viongozi wakubwa hasa wasiofuata au kukubaliana na sera zao.
“Pili, kwa mujibu wa Wassira kwa sasa Watanzania tunajua kuwa baya lolote likimpata Dk. Slaa au Mbowe litakuwa limetekelezwa na watu wa usalama.”
Ndimara aliongeza kuwa kwa kauli ya Wassira kusema kuwa Idara ya Usalama inashughulikia wanasiasa maarufu, ameivua nguo idara hiyo na wangetarajia idara hiyo imwajibishe kwa kutoa siri za Usalama wa Taifa.
“Linapokuja suala la haki za binadamu hakuna mdogo au mkubwa, hakuna rais au mama ntilie.
Hakuna aliye mdogo asiyehusiana na mkubwa, ikifikia hatua ya dharau ya aina hii tunashindwa kumwelewa waziri huyu,” alisema.
Mkurugenzi wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotetea haki za binadamu, Onesmo Olengurumwa alisema Wassira amethibitisha kuwa kumbe Usalama wa Taifa kuna watu wanawateka na kuna wengine hawatekwi.
“Tunashukuru kwa kusema kuwa kuna kundi fulani linawindwa, ni dharau sana kwa kauli ile kwa kuwa Kibanda ni Mtanzania, awe na cheo asiwe na cheo, awe mwanasiasa au sio mwanasiasa serikali inapaswa kumlinda.
“Kauli ya Wassira inaleta matabaka, inaonesha wengine wana thamani zaidi, wengine hawana thamani,” aliema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana alizungumza kwa kifupi akisema; “hiyo kauli haikupimwa, sio kauli iliyotarajiwa kutoka kwa kiongozi wa CCM.
Kweli hakutumia busara katika kutamka kauli hii tena bungeni.”
0 comments:
Post a Comment