NI KUTOKANA NA DENI KUBWA LA TAIFA
http://www.freemedia.co.tz
RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE, ALIYEPO MADARAKANI.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, madeni hayo ni pamoja na yale ya nje na ndani ya nchi, na mengine ambayo hayamo kwenye orodha ya madeni ya taifa.
Duru za siasa zinaeleza kuwa kasi ya ulipaji madeni hayo haiwezi kukamilika ndani ya kipindi cha Rais Kikwete, hivyo mrithi wake atakuwa na wakati mgumu wa kulipa madeni hayo.
Kinachotisha zaidi ni kwamba badala ya kuwapo mikakati ya kurejesha, kuna kila dalili ya kuendelea kukopa, hivyo kuondoa uwezekano wa Rais Kikwete kumaliza deni hilo.
“Wakati serikali inasisitiza kwamba deni letu linastahimilika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anaonesha mashaka makubwa sana kutokana na kasi ya kukua kwake.
“Taarifa ya CAG inaonesha kuwa deni la taifa linazidi kuongezeka kwa asilimia 38% kutoka sh trilioni 10.5 mwaka 2009/2010 hadi sh trilioni 14.4 mwaka 2010/2011,” alisema Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya Juni 30 2012, deni la serikali limefikia sh trilioni 16.9, ukilinganisha na mwaka 2011 ambapo lilikuwa sh trilioni 14.4.
Katika deni la sh trilioni 16, kiasi cha sh trilioni 12, sawa na asilimia 73 ni deni la nje na deni la ndani ni sh trilioni 4.5, sawa na asilimia 27.
Taarifa hiyo ilisema kuwa kuongezeka kwa deni hilo kumetokana na ukopaji mpya, malimbikizo, malimbikizo ya riba na kushuka kwa thamani ya shilingi, ukizilinganisha na fedha za nje.
“Sehemu kubwa ya deni ilitumika katika urari wa malipo na kusaidia bajeti, ustawi wa jamii na elimu, usafiri na mawasiliano,” ilisema taarifa hiyo ya CAG.
Kwa upande wa deni la ndani, liliongezeka kutoka sh trilioni 83.6 kutoka sh trilioni 3.7 mwaka 2011 hadi sh trilioni 4.5 hadi kufikia Juni 2012.
Taarifa ya CAG iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni ilisema kuwa mbali ya madeni hayo ya taifa, serikali ina madeni mengine ambayo hayajajumuishwa kwenye deni la taifa.
Madeni ambayo hayakujumuishwa kwenye deni la taifa ni pamoja na sh bilioni 716.6 kati ya madai ya jumla ya sh trilioni 3.2, ikiwa ni kwa ajili ya michango ya pensheni kwa wafanyakazi wa serikali, ambapo serikali imekubali kulipa kwa awamu kumi kwa kiasi cha sh bilioni 71.6 kila mwaka wa fedha.
Madeni mengine ambayo hayajajumuishwa kwenye deni la taifa ni pamoja na madai ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini na City Bank kiasi cha dola za Marekani 4,129,298.38 na dola za Marekani 1,460,000, sawa na sh bilioni 6.5 na sh bilioni 2.3, sawia dhidi ya Kampuni ya Ndege ya Tanzania. Madeni haya yatalipwa na serikali kupitia Hazina.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, serikali pia ilitoa dhamana kwa wizara, idara, Serikali za Mitaa na mashirika ya umma kwa ajili ya mikopo iliyotolewa kutoka mifuko ya pensheni ambayo serikali inalipa kupitia kwenye bajeti.
Madeni hayo yanafikia sh trilioni 1.3, ambapo fedha hizo zilitumika katika miradi ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Ofisi ya TAKUKURU na nyumba za polisi.
Hata hivyo CAG wakati akitoa taarifa yake kwa vyombo vya habari, hakutaka kuzungumzia ukuaji wa deni hilo na hata alipoulizwa kauli yake, alisema kwa kifupi kwamba hayuko tayari kuzungumzia ukuaji wa deni hilo.
Wadadisi wa mambo ya siasa wanabainisha kuwa kuna kashfa kubwa sana katika Akaunti ya Deni la Taifa.
“Uhakiki wa mchanganuo wa madeni ya taifa kama ulivyokuwa tarehe 30, Juni, 2012, ulibaini kuwepo kwa marekebisho ya deni ya sh 619,803,554,183.91 ambayo uongozi haukuweza kutoa maelezo ya kuridhisha,” alisema mmoja wa wabunge akinukuu taarifa ya CAG.
Hali hiyo imetokana na kukosekana kwa maelezo ya kutosha kuhusu zaidi ya nusu trilioni za deni la taifa.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari wiki iliyopita, Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), alisema ongezeko la deni hilo linapaswa kutiliwa mashaka makubwa.
Alisema tafiti mbalimbali duniani zinaonesha kuwa kuna mahusiano makubwa sana kati ya deni la taifa na utoroshaji wa fedha kwenda kwenye mabenki ya nje.
“Mabilioni haya kwenye Akaunti ya Deni la Taifa yanashtusha sana. Kambi ya Upinzani Bungeni kwa miaka miwili mfululizo imekuwa ikitaka ukaguzi maalumu kwenye Akaunti za Deni la Taifa lakini serikali imeshindwa kufanya hivyo,” alisema.
Kwamba, akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya PAC pia ametaka CAG afanye ukaguzi huo maalumu.
0 comments:
Post a Comment