BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SIMULIZI ZA TIDO:KISANGA CHA KUKAMATWA.

Kwa ufupi

Inavyoelekea, Serikali ya Rais Daniel Arap Moi haikuwa imefurahishwa na jinsi nilivyoripoti mkasa ule. Kumbuka kwamba, kwa sababu ya hali ya wasiwasi iliyokuwapo nyakati zile, hata magazeti ya Kenya yenyewe mwanzoni yalikuwa yanapandia kwenye mgongo wa taarifa zangu nilizokuwa nikizitangaza BBC, Voice of America na Deutche Welle.  
http://www.mwananchi.co.tz 
Tido Mhando
NI hivi majuzi tu mdau mmoja wa habari, akizungumza kwenye kikao cha wanahabari alisema: “Mwandishi wa habari ambaye hajawahi kukabiliwa na kashkashi zozote kwenye kazi yake hiyo, basi ajue bado hajakomaa.”.

Kauli hiyo ilinikumbusha kasheshe binafsi iliyonikuta wakati nikiwa bado nchini Kenya, hususan mwaka ule wa 1990 baada ya kuuawa kinyama kwa aliyekuwa waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Dk Robert John Ouko. 

Kisa ambacho nilikuwa mwandishi wa kwanza wa habari kukitangaza duniani, kama nilivyohadithia kwenye makala zangu tatu zilizopita.

Basi kimbelembele changu kile, kidogo kinitokee puani, kwani wakati nikijibaraguza kwa hili na lile, kumbe wakubwa walikuwa wananipigia mahesabu ya nguvu.

Inavyoelekea, Serikali ya Rais Daniel Arap Moi haikuwa imefurahishwa na jinsi nilivyoripoti mkasa ule. Kumbuka kwamba, kwa sababu ya hali ya wasiwasi iliyokuwapo nyakati zile, hata magazeti ya Kenya yenyewe mwanzoni yalikuwa yanapandia kwenye mgongo wa taarifa zangu nilizokuwa nikizitangaza BBC, Voice of America na Deutche Welle.
   

Kwa kweli hata huko nyuma tayari nilikuwa nimekwisha tahadharishwa na baadhi ya marafiki zangu (kumbuka nami nilikuwa nimejijenga vilivyo), kwamba nisipoangalia siku moja nitajikuta Nyati House, jumba lililopo katikati ya jiji hili na ambalo maafisa wa usalama walikuwa wanawababazua wapinzani wa serikali, wanaharakati na hata waandishi wa habari kwa“mateso ya kufa mtu”, ili kujua mambo wanayoyafanya.

Kwa ujumla, wakati ule wa kilele cha kutaka mageuzi nchini Kenya, watu wengi nchini humo  walikuwa wakiitegemea zaidi BBC kwa kupata habari za ukweli na uhakika.

Sasa hilo ndilo likawa kosa langu miye niliyekuwa ripota pekee wa idhaa hiyo nchini Kenya na Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla. Nakumbuka wakati mmoja Rais Moi alipandisha munkari, akawaambia watu aliokuwa akiwahutubia katika hadhara moja huko Mombasa: “BBC, BBC – kwani BBC mama yenu ?”.

Sasa mara baada ya kutulia kiasi kwa sekeseke lile la Dr Ouko, nami nikaanza kupanga ni nini cha kufanya. Kwakweli nilikuwa nimechoka sana maana kwa kipindi cha zaidi ya miaka mine hivi, sikuwa nimechukua likizo hata kidogo.
  

Kama ilivyo kawaida, ukiwa mwandishi wa habari wa kujitegemea, kula kwako kunatokana na kile unachokikamilisha kila siku, hivyo muda wa likizo haupo kabisa.

Kwa bahati, Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC ziku zile, Neville Harms, alikuwa amenialika kwa muda niende London kwa kipindi cha miezi mitatu ili niweze kuwafahamu vyema wenzangu ninaofanya nao kazi pamoja na kuyafahamu  mazingira yenyewe kwa karibu zaidi. 

Akanitumia tiketi, lakini nikawa nimeikalia tu kwani sikuwa na muda huo kwasababu ya kutingwa na kazi nyingi.

Lakini sasa baada ya kuutua mzigo wa stori ya Dr Ouko, nikaona heri niitumie ile ofa  ya Harms nijiendee London kwa miezi hiyo mitatu, kiasi iwe kama nimejipumzikia hivi, maana ningekuwa nafanya kazi ya saa maalum na huku pia nikijipatia muda wa kumpumzika na kubarizi.  

Nikaona huo ni uamuzi wa busara, lakini ilinibidi nijipange na kujitayarisha.

Wakati nikiwa nakamilisha baadhi ya mambo ambayo niliwajibika kuyawacha vizuri wakati nikiwa sipo kwa muda wote huo wa miezi mitatu, ikiwa ni pamoja na kurekodi vipindi mbalimbali vya radio nilivyokuwa nikivitangaza kwa kupitia Sauti ya Kenya (VoK), niliamua kuchukua siku chache na kwenda Dar es Salaam kuwaaga wazee, maana kama tujuavyo, unapokwenda dunia ya mbali tena ugenini baraka za wazazi ni muhimu.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: