BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SPIKA ANNE MAKINDA AMBEBA NDUGAI

AUNGA MKONO WABUNGE CHADEMA KUFUKUZWA,
FREEMAN MBOWE ANG'AKA, ASEMA SPIKA NI DIKTETA
 
http://www.mtanzania.co.tzhttp://70.85.226.211/~tbcgo/images/Makinda.JPG
 SPIKA WA BUNGE ANNE MAKINDA.
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, jana alipigilia msumari katika sakata la adhabu inayowakabili wabunge sita wa Chama cha Demokrasia na Maendelea (CHADEMA).

Juzi Makinda aliahidi kutoa mwongozo wake kuhusu adhabu iliyotolewa na Naibu Spika, Job Ndugai ya kuwasimamisha wabunge hao kuhudhuria vikao vitano vya Bunge.

Mwongozo huo ambao ulitarajiwa kuwanusuru wabunge hao wa upinzani, ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu, kutokana na kile kilichodaiwa kuwa adhabu hiyo ilitolewa kienyeji bila kuzingatia matakwa ya kanuni.

Hata hivyo, mapema jana akitoa mwongozo wake, Spika Makinda alimuunga mkono naibu wake na kusema kuwa adhabu iliyotolewa kwa wabunge hao ilikuwa sahihi.

Kwa mujibu wa Makinda, kanuni ya pili sehemu ya pili inampa mamlaka kufanya uamuzi kwa mambo ambayo kanuni za Bunge zipo kimya juu ya jambo hilo.

Akizungumzia uamuzi huo, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, aliushangaa mwongozo wa kiongozi huyo wa Bunge na kusema kuwa Spika Makinda ni dikteta.

Mbowe alisema wabunge wa Chadema hawatishiki na udikteta huo na kwamba hawataacha kusema ukweli ndani na nje ya Bunge, kwa kuwa hiyo ndiyo kazi waliyotumwa na wananchi.

Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari jana mjini hapa, Mbowe alisema. “Sisi hatuna tatizo kabisa na hatufurahii hizi vurugu zinazotokea bungeni kila mara.



Hatuna tatizo kabisa na wabunge wenzetu wa CCM na ndiyo maana tunapokuwa nje ya Bunge tunakuwa kitu kimoja, tunacheka na kutaniana wakati wote.

“Tatizo letu ni kile kiti cha spika. Spika ni dikteta, kiti chake hakitutendei haki na kwa bahati mbaya hakitaki kutambua kuwa tuko katika mfumo wa vyama vingi.

“Nawaambia kama tatizo ni Lissu (Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki), wajue ataendelea kusimama mara 100 kama mambo hayaendi sawa na hatasimama kama mambo yatakwenda vizuri.

“Lissu ni mwanasheria wetu na ndiye Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, hawezi kusimama kwa sababu tu anapenda kusimama. Anasimama kwa sababu kuna haja ya kusimama iwapo kuna upendeleo wa wazi,” alisema Mbowe.

Kuhusu uamuzi watakaochukua dhidi ya uamuzi huo wa spika, alisema wakati wowote kuanzia sasa, Kamati ya Uongozi ya Upinzani itaketi ili kuangalia namna ya kukata rufaa.

“Tutakaa kama kamati ili kuangalia namna ya kuwasilisha ‘official protest’ kwa mujibu wa kanuni na rufaa hiyo tutaiwasilisha katika Kamati ya Kanuni ya Bunge.

“Tunajua hata tukikata rufaa hatutafanikiwa, lakini tunachotaka kufanya ni kuweka kumbukumbu sawa kwa vizazi vijavyo.

“Kanuni ya pili, sehemu ya pili aliyotumia Spika, kwamba inampa mamlaka kufanya uamuzi kwa mambo ambayo hayako kwenye kanuni, alikosea kuitumia.

“Kanuni hiyo inazungumzia mambo yasiyo ya kawaida, kwa mfano, wewe ni mwandishi wa habari na unatakiwa kuwa katika eneo maalum walilotengewa waandishi wa habari.

“Sasa, kwa kutumia ujanja wako, ukafanikiwa kuingia bungeni na kunipiga ngumi, sasa katika mazingira hayo ambayo kwenye kanuni hayakuzungumzwa, ndipo unapoweza kutumia kanuni hiyo.

“Lakini, wakati wabunge wetu wanadaiwa kufanya vurugu, naibu spika aliruhusu askari wengine waingie bungeni kumtoa Lissu, jambo ambalo ni ukiukwaji wa kanuni za Bunge.

“Nasema kanuni zilivunjwa kwa sababu watu wanaotakiwa kuingia bungeni, wa kwanza ni wabunge wenyewe na wengine ni viongozi wa Bunge na watumishi wa Bunge.

“Yaani kwa mujibu wa kanuni zetu, hata Rais wa Zanzibar na makamu wake na hata Rais wa Kenya au wa nchi yoyote, haruhusiwi kuingia bungeni mpaka Bunge litengue kanuni.

“Kwa mujibu wa kanuni zetu, anayeruhusiwa kuingia bungeni bila kanuni kutenguliwa ni Rais wetu tu kwa sababu yeye ni sehemu ya Bunge.

“Lakini, pamoja na naibu spika kujua kanuni hizo, alipoona askari wa Bunge wameshindwa kumkamata Lissu, aliagiza askari wengine wasioruhusiwa, waingie bungeni wakati akijua kanuni zinazuia.

“Kwa maana hiyo, msimamo wetu ni kwamba, kama kiti cha spika kitaendelea na upendeleo huo, watarajie matukio mengine zaidi.

“Nawaambia kabisa, kwamba hatuwezi kunyamazishwa kwa kutolewa nje au kwa kufungiwa kuhudhuria vikao. Watufungie hata kama ni vikao 100, lakini tutaendelea kusimamia haki na ukweli.

“Nasema hivyo kwa sababu mimi ni kiongozi wa upinzani bungeni, ninaposimama kutaka kusema kitu, hata kama kuna wabunge wengine wa upande wangu wamesimama, lazima mimi ndiye nitakayeruhusiwa.

“Hali kadhalika kwa Lissu, yule ndiye mnadhimu wa kambi ya upinzani, anaposimama hata kama kuna wabunge wengine wamesimama, lazima kiti cha spika kimruhusu yeye kwanza.

“Lakini, kilichofanyika siku ile ni kwamba, Lissu aliposimama, Mnyika na Kiwanga nao walisimama.

“Lakini kwa sababu binafsi, naibu spika akamruhusu Kiwanga badala ya Lissu. Nadhani alijua Kiwanga hatakuwa na hoja juu ya kilichokuwa kikizungumzwa kwani hakujua kama huyo Kiwanga ndiye aliyekuwa mratibu wa kampeni zetu za urais mwaka 2010.

“Kikanuni, hapo alitakiwa Lissu ndiye aruhusiwe kwanza, lakini mtaona wenyewe, kwamba alikataliwa eti kwa sababu ameshazungumza sana wakati kanuni zetu hazitoi ukomo wa mbunge kuzungumza.

“Lakini kikanuni, kanuni ya 74 (1) ndiyo ingetumika ambayo inataka mbunge anapokiuka utaratibu apelekwe mbele ya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, badala yake mambo yakafanywa kienyeji tu,” alisema.

Waliosimamishwa na majimbo yao katika mabano ni Godbless Lema (Arusha Mjini), Highness Kiwia (Ilemela) na Hezekiah Wenje (Nyamagana).

Wengine ni Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

SPIKA ATOA MWONGOZO
Awali, Spika Makinda alitoa ufafanuzi wa mwongozo ulioombwa na Mbowe juzi, kuhusu kusimamishwa kwa wabunge hao sita wa Chadema.

Akitoa ufafanuzi huo, Spika Makinda alisema uamuzi uliofanywa na naibu spika ulikuwa sahihi, kwa kuwa ulifuata kanuni za Bunge.

Alisema kwamba adhabu aliyopewa Lissu ilitokana na kukaidi agizo la kiti wakati alipotakiwa kukaa baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Kiwanga (Chadema), kuruhusiwa kuzungumza.

Kuhusu wabunge wengine watano wa chama hicho, alisema walipewa adhabu hiyo kwa kosa la kuwazuia askari wa Bunge kutekeleza agizo la naibu spika la kutolewa nje kwa Tundu Lissu na hivyo kusababisha fujo.

“Waheshimiwa wabunge, kanuni zetu na hasa ya 2 (2) na kanuni ya 5 (1) ya kanuni za Bunge, imempa mamlaka Spika kufanya uamuzi pale ambapo hakuna utaratibu wa kanuni.

“Aidha, uamuzi uliofanywa na spika unaoruhusu uendeshaji bora wa shughuli za Bunge ambao unaleta amani na utulivu bungeni, unaingizwa kwenye kitabu cha maamuzi ili kuongoza mwenendo wa baadaye wa uendeshaji wa Bunge.

“Kwa kitendo kilichotokea Aprili 17 bungeni, hakiwezi kupuuzwa kwa kuwa ni kitendo dhahiri cha kudhalilisha mamlaka ya spika na kilikuwa kitendo cha utovu wa nidhamu wa hali ya juu.

“Kwa maana hiyo, ninatumia kanuni ya 5 (1) na kanuni ya 2 (2) ya Bunge inayompa mamlaka Spika kufanya uamuzi ambapo jambo ama shughuli yoyote haikuwekewa masharti katika kanuni hizi.

“Uamuzi uliofanywa na Mheshimiwa Job Ndugai, Naibu Spika wa kuwatoa nje wabunge na kuwataka wasihudhurie vikao vitano vya Bunge ni halali,” alisema na kuongeza:

“Kwa maana hiyo, uamuzi huo utaingizwa katika kitabu cha uamuzi wa spika na mbunge yeyote atakayefanya vitendo hivi, apewe adhabu hii,” alisema.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: