BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WABUNGE WAPINGA ONGEZEKO LA NAULI ILIYOTANGWZA NA SUMATRA



MAISHA YA WATANZANIA NI MAGUMU.
http://www.mtanzania.co.tz
WABUNGE mbalimbali wamepinga uamuzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), kuongeza nauli mpya za daladala na mabasi yaendayo mikoani.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam jana, wabunge hao walisema kitendo cha SUMATRA kupandisha nauli hakiwezi kukubalika kwa sababu kinaonyesha jinsi asilimia 90 ya wananchi ambao ni walalahoi wanavyonyanyaswa.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) alisema SUMATRA wamepandisha nauli katika muda usiotarajiwa kwa kuwa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa 2013/2014 haijapitishwa.

“Kitendo cha kupandisha nauli za mikoani na daladala kitasababisha mfumuko wa bei za bidhaa bila kuwapo sababu za msingi.

“Kwanza gharama za usafirishaji mizingo zitaongezeka ambapo anayeumia ni mwananchi wa kawaida tofauti na wale wenye uwezo kifedha.

“Binafsi sina imani kabisa na SUMATRA, siamini kama mchakato ulifuatwa kwa kuwahusisha wadau wote, nafikiri waliolengwa kunyanyaswa ni wananchi wanyonge.

“Ninavyojua vitu ambavyo vinaweza kusababisha mfumuko wa bei ni chakula, usafiri na elimu, sasa kwa kuwa wamepandisha nauli subirini hali hiyo itatokea muda si mrefu.

“Kwanza, nawashangaa hao SUMATRA, kwa nini wanapandisha nauli wakati mafuta hayajapanda bei, nafikiri kuna haja suala hili Serikali kupitia viongozi kuliangalia, vinginevyo ni kuwaumiza masikini bila sababu za msingi,” alisema Zitto.

 
Naye Mbunge wa Tunduru Kusini, Abdallah Mtutura (CCM), alisema hakukuwa na sababu za msingi mamlaka hiyo kupandisha nauli kipindi hiki.

“Mimi sioni picha halisi ya SUMATRA kupandisha nauli wakati thamani ya dola ipo pale pale, mafuta hayakupanda na barabara nchini zimeboreshwa.

“Najua kuna kitu watasingizia, ikiwamo kupanda kwa vipuri, lakini hiyo si sababu ya msingi ya kuwafanya wananchi waumizwe kiasi hicho,” alisema Mturura.

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Peter Serukamba, aliwaambia waandishi wa habari, kwamba hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa halijui vizuri.

“Jamani naweza kusema leo nauli hizo zibaki kama zilivyokuwa wakati sijui namna walivyoendesha mchakato wenyewe, binafsi jambo hili limekuja kwangu ghafla.

“Mimi ni kiongozi, sitaki kuanzisha malumbano na idara au viongozi wenzangu, lakini natarajia kukutana na Wizara ya Uchukuzi na SUMATRA wenyewe ili kupata taarifa kwa undani juu ya uamuzi huo,” alisema Serukamba.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kisarawe, Seleman Jafo (CCM), alisema nauli hizo zimepandishwa bila kufanya utafiti wa maisha ya wananchi.

“Hapa wamepandisha nauli bila kufanya utafiti wa maisha ya Watanzania ambao ni walengwa, hii ni kuwataka sasa waendelee kuteseka, licha ya kuwapo Serikali iliyokamilika.

“Kwanza, nauli zinapandishwa wakati abiria wanasafiri kwa shida, wangeanza kuboresha vyombo vya usafiri kwanza ili hata kama unaongeza nauli abiria anakubaliana na jinsi anavyosafiri.

“Leo Dar es Salaam wanasafirishwa kama magunia ya mkaa, ukiliona basi la Mbagala au Gongolamboto jinsi abiria wanavyoning’inia, hutaamini kama watafika salama, lakini SUMATRA na askari wa barabarani wanaangalia tu.

“Ni vema hatua zingechukuliwa kwanza, yaani usafiri ungeboreshwa kwanza ndipo masuala mengine yafuate, kwa hili naombeni wadau na viongozi wa Serikali kulingalia ili wananchi wasiendelee kuminywa bila sababu za msingi,” alisema Jafo.

Naye Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (CHADEMA), alisema nauli zimepandishwa kwa amri ya viongozi wa Serikali wanaomiliki magari ya abiri na mizigo pamoja na meli ili wapate fedha nyingi.

Kwa mujibu wa Vincent, kitendo cha SUMATRA kupandisha nauli kinadhihirisha ni kwa jinsi gani Serikali ya CCM isivyojali Watanzania walioiweka madarakani.

Wakati wabunge wakisema hayo, baadhi ya wananchi jijini Dar es Salaam, nao wamepinga ongezeko la nauli hizo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Kambangwa, Amosi Mpinga, alisema ongezeko hilo linalenga kuwadhoofisha wananchi wa kawaida, kwa sababu wanaishi maisha ya shida.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: