Kadiri
siku zinavyokwenda mbele, idadi ya watoto wa mitaani inaongezeka katika
Jiji la Dar es Salaam na miji mingine mikubwa kama Arusha, Dodoma,
Mwanza, Mbeya na kwingineko.
Ni suala la kawaida kuona watoto wamejipanga kando ya barabara
wakiomba wasamaria wema. Wapo ambao wako peke yao wakifanya kazi hizo,
wengine wanafanya kazi hiyo wakiwa na wazazi wao; wazazi hukaa kando
kusubiri kuwanyang’anya kile ambacho watoto wanaomba kutoka kwa
wasamaria wema.
“Nimetoka Dodoma, huu ni mwaka wa tatu, niko na mama na bibi, wao
mara nyingi huwa wanakaa pembeni ya barabara, sisi watoto ambao ni wanne
ndio tunaoingia katikati ya barabara kuomba hasa wakati magari
yanaposimama,”anasema, John Francis (sio jina lake halisi) mwenye umri
wa miaka 12 akiwa maeneo ya Faya, Kariakoo jijini Dar es Salaam. Watoto
wengi wa mitaani wanaonekana kuteswa mno hasa usiku kwa kubakwa na
kulawitiwa na hata kupigwa pale wanapokataa kile ambacho walio wakubwa
kwao wanataka ikiwemo kufanyishwa vitendo vya ngono au kutoa fedha
walizoomba au walizopata kutokana na kazi mbalimbali zikiwemo kuosha
magari.
Huenda ndiyo ‘majambazi’ wa kesho
Hata hivyo kinachoonekana ni kwamba baadhi ya watoto hawa huenda
wakawa ni majambazi,kwani kwa mujibu wa Mwanasaikolojia, Modesta Kimonga
kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, kitaalamu mtu ambaye anaishi katika hali
fulani ngumu ikiwamo kiuchumi, ni rahisi kwake kushawishiwa kufanya
lolote.
Wasio na jamaa wako hatarini zaidi
“Kuna kijana aliwahi kutaka kunilawiti, nilikataa, nilimwambia mama
alimtukana na kutaka kumpiga.Wanaobakwa na kulawitiwa sana ni wale ambao
hawana watu wa kuwasaidia, unakuta wengine wametoka mikoani, wapo hapa
Dar es Salaam, hawana ndugu wala jamaa,” anasema Francis.
Usiku ni jehanamu
Katika utafiti ambao mwandishi amefanya katika maeneo mbalimbali ya
Jiji la Dar es Salaam, yakiwamo Ubungo katika makutano ya barabara ya
Mandela, Morogoro na Sam Nujoma, Kariakoo, Posta, Kinondoni, Magomeni,
Buguruni, Kawe na Mwenge ambako kunaonekana kuwa na watoto wengi wa
mitaani hasa kutokana na kuwa na shughuli nyingi za mbalimbali za
kijamii, usiku ni wakati wa hatari zaidi kwa watoto, kwani ndipo huwa
wanafanyiwa kila aina ya ukatili, huku wakiwa hawana wa kuwasaidia.
Katika eneo la Magomeni, makutano ya barabara itokayo Kinondoni
kwenda Jangwani, jijini Dar es Salaam, kuna watoto ambao wanaosha
magari, utafiti unaonyesha baadhi yao wamekuwa wakiingiliwa usiku na
baadhi ya watoto wa mitaani walio wakubwa au watu wengine ambao sio
ombaomba kwa ahadi za kuwasaidia waondokane na maisha duni
yanayowasumbua.
“Ni kweli nimewahi kuingiliwa, siyo kwamba nilipenda, nakumbuka siku
hiyo mvua ilinyesha sikuwa na pa kulala, kwani mimi na watoto wenzangu
huwa tunalala nje. Kuna jamaa mmoja mtu mzima ambaye naye huwa
tunasafisha naye magari na shughuli zingine za mitaani, ana chumba
aliniingilia kwa nguvu, alianza polepole, hatimaye alifanikiwa
kuniingilia, nililia sana, sikuwa na la kufanya. Baada ya hapo akawa
karibu nami kunisaidia mambo mengi yakiwemo kuninunulia chakula
ninapokuwa sina fedha,” anasema mtoto mmoja katika eneo la makutano hayo
(jina limehifadhiwa).
Katika eneo hilo la makutano ya barabara ya kutoka Kinondoni kwenda
Jangwani, kuna mtoto mwingine ambaye muda mwingi huwa anasinzia
kumaanisha kwamba huwa amekuwa amelewa, ana umri wa miaka 14,
anasisitiza “Ni kweli kuna watoto wengi wanaingiliwa kinyume na maumbile
hasa kama mtoto mwenyewe anapenda kula vizuri,” anasema mtoto huyo,
aliyeingia jijini akitokea Mwanza kwa kumhonga fedha kidogo kondakta wa
basi moja linalotoka Mwanza kuja Dar es Salaam ili kuja kujaribu maisha
jijini, kwani kule Mwanza anasema japo wazazi wake wako hai, hawana
uwezo.
Katika eneo la Kawe, kwenye bonde ambalo ni mpaka wa Kawe na Mbezi,
kuna kundi la watoto linaloitwa Mbwakoko, kwa maana kuwa kwa haraka
unaweza kufikiri ni watoto wazembe hivi, lakini ukikaribiana nao usiku
utakiona cha moto.
Wana umaarufu katika eneo hilo, kwa matendo yao, kuna wakati wenyeji
wanasema huwalazimisha wanaopita eneo hilo kutoa fedha, wanapokataa
huwadhuru au hata kuwatishia kwa maneno makali.
“Maisha ni magumu kuliko unavyoweza kufikiri, wakubwa wanatubaka
kadri wanavyotaka hasa inapofika usiku, hata ukilia haisaidii kwa sababu
hakuna wa kukusaidia,” anasema mtoto mmoja , huku watoto wa kike
wakionekana kuingiliwa na wanaume wengi kwa staili na nyakati tofauti na
wanapokataa hupigwa.
“Ni kweli wapo watoto ambao wanatumika katika wizi, wanakuwa kama
chambo, wengine wanatumika kuuza dawa za kulevya kwa maana ya kutumwa
kupeleka dawa hizo sehemu fulani au kwa mtu fulani au hata kuuza,”
anasema mtoto mwingine na kuongeza kuwa yeye hayafurahii maisha haya
lakini hana la kufanya kwa sababu wazazi wake wameshakufa na alikuja
jijini toka mwaka 2005 akitokea Mwanza, hana mawasiliano na wazazi wake
tangu wakati huo wala hajui chochote kwani alikuja akiwa na umri wa
miaka 11 baada ya wazazi wake kutalakiana.
Polisi wanajua nini?
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova,
alipohojiwa kuhusiana na taarifa hizo aliomba apelekewe maswali ndipo
ajibu.
Baadaye mwandishi aliwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi
wa Kinondoni, Charles Kenyela ambaye alitoa ushirikiano mzuri kwa kusema
kuwa anasikitishwa na taarifa hizo na kwamba anaangalia namna ya
kushirikiana na viongozi wengine ili kuona nini wanaweza kufanya.
“Tatizo la watoto wa mitaani ni kubwa, polisi pekee hatuwezi ni lazima
Watanzania kwa ujumla tushirikiane kuona namna ya kukomesha tatizo hili
la watoto wa mitaani nchini,” anasema Kenyela.
Serikali na mikakati
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto Ummy
Mwalimu katika mahojiano na mwandishi wa makala haya anakiri kuwepo kwa
tatizo kubwa la watoto wa mitaani na kusema Serikali imeandaa mkakati
maalumu kuwasaidia watoto hawa.
Idadi ya watoto wa mitaani Dar
“Ni kweli tatizo ni kubwa, watoto wa mitaani wanaongezeka, miaka
kadhaa iliyopita walikuwa 3000 hivi, sasa wako zaidi ya 6000. Kama
Serikali tumeunda mkakati dhabiti wa kupambana na hali hii, sasa
tumeuwasilisha kwa wataalamu ili kupata ushauri zaidi na kwamba naamini
suala la watoto wa mitaani huenda likawa historia,” anasema Ummy.
Hata hivyo baadhi ya wananchi wanaona hiyo ni kauli tu ambayo haina
utekelezaji kwani suala la watoto wa mitaani limekuwapo kwa miaka mingi
huku viongozi wakiendelea kutoa ahadi zisizo na utekelezaji.
Kuna
taasisi nyingi zisizo za kiserikali ambazo nazo ni kama zilizo nyingi
zinaonekana kutofanya jitihada kubwa kupambana na tatizo hili. Hata
hivyo Waziri anasisitiza kuwa watoto hawa wa mitaani watasaidiwa kwa
vitendo.
0 comments:
Post a Comment