MSIMAMO WAKE KATIKA KATIBA MPYA WATIKISA, DR SLAA ASEMA ATAHUKUMIWA KAMATI KUU.
http://www.mtanzania.co.tz
MSIMAMO wa mwakilishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesigwa Baregu, kugomea agizo la chama chake lililomtaka ajiengue katika Tume hiyo ifikapo Aprili 30, umeonekana kukivuruga chama hicho, MTANZANIA Jumapili linaripoti.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, zinaeleza kugoma huko kwa Profesa Baregu kumeilazimisha Chadema kufanya maamuzi ya kuitisha Mkutano wa dharura wa Kamati Kuu kwa ajili ya kulijadili suala hilo, ikiwa ni pamoja na kufikia maamuzi ya kichama na hatua za kuchukua.
Hivi karibuni Chadema kilisema kuwa hakiridhishwi na mchakato mzima wa kutunga Katiba mpya, baada ya masharti kiliyotoa kwa serikali kikitaka kifanye mabadiliko kutotimizwa, na hivyo kumuagiza mwakilishi wao, Prof. Baregu ajitoe ndani ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba baada ya kujitoa kitaanzisha kampeni ya nchi nzima kuwahamasisha wananchi wasusie mchakato huo.
Hata hivyo, uamuzi huo wa Chadema ulipingwa na Prof. Baregu mwenyewe, ambaye alikataa kujitoa kwa hoja kwamba haoni kama kuna mambo yanapindishwa na serikali ndani ya Tume hiyo kama ambavyo chama chake kinadai.
Zikiwa zimepita siku tano (jana) tangu muda aliopewa Prof. Baregu na Chadema kujitoa katika Tume kuisha na yeye kugoma, kimesema kuwa suala hilo majibu yake yatapatik
ana kupitia kikao cha dharura cha Kamati Kuu kitakachoketi muda wowote kuanzia sasa.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema: “Suala hili alilitoa Mwenyekiti wangu na sina cha kuongea, nimekuwa najibu swali hili kwa waandishi mbalimbali wa habari, kwa ufupi jambo hili litazungumzwa kwenye kikao cha Kamati Kuu ya Chama. Sijui muda wala siku kwa sababu bado hakijapangwa.”
Wakati Dk. Slaa akiweka msimamo huo wa chama, baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa wanamshutumu Prof. Baregu kuwa amekataa kufuata maagizo ya chama chake kwa sababu ya malipo makubwa wanayopatiwa viongozi na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Taarifa ambazo hazijathibitishwa kutokana na wahusika kugoma kuzungumza zinaeleza kuwa, viongozi na wajumbe wa Tume hiyo kwa siku wanalipwa kiasi cha shilingi laki tano, ambapo kwa mwezi ni karibu na shilingi milioni 12-16.
Pamoja na hilo, juzi wakati Msemaji wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alipokuwa akiwasilisha hotuba yake kuhusu mpango wa makadirio ya mapato ya fedha ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014, alihoji matumizi makubwa ya mabilioni ya fedha za wananchi ndani ya Tume hiyo, akidai kuwa yanaashiria harufu mbaya ya ufisadi.
Alisema matumuzi hayo hayaelezeki wala kukubalika kwa misingi ya kisheria na kwa rekodi ya utendaji kazi wa Tume hiyo.
Lissu alihoji Bunge kuombwa tena kuidhinisha shilingi bilioni 33.944, kiasi kile kile kilichoidhinishwa mwaka jana kwa ajili ya matumizi ya Tume kwa mwaka huu wa fedha wa 2013/14.
Katika mwaka wa fedha 2012/2013, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 33.944 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya Sheria za Tanzania.
Hata hivyo matumizi yake yamezua mashaka na kwa mujibu wa Lissu, kuna ulaji zaidi kwa wajumbe wa Tume hiyo.
Alipoulizwa Prof. Baregu kwamba dhamira ya kugoma kutekeleza maagizo ya chama chake imesukumwa na fedha nyingi anazozipata kutoka katika Tume ya Katiba na si utaifa kama anavyodai, alisema anachokifikiria kuhusu tume hiyo ni kwamba inapewa fungu dogo sana la fedha kuliko tume nyingine zilizopata kuundwa.
“Unajua kuna habari nyingi za uzushi ambazo zimekuwa zikiinyoshea kidole Tume hii, hasa wanasiasa wako mstari wa mbele katika hili, mara utawasikia, Tume tunalipana posho kubwa hadi wengine wanadiriki kusema tunachukua posho ya Sh. 500,000 kwa siku.
Wengine utawasikia wanadai tunalipwa mamilioni ya fedha kwa mwezi, laiti kama wangeufahamu ukweli wasingeweza kutamka maneno hayo,” alisema Prof. Baregu.
Kuhusu kukaidi kwake agizo la chama chake kilichomtaka ajiengue kwenye Tume ya Katiba, Prof. Baregu, alisema hajui kitu chochote kuhusu hilo kwa sababu hana taarifa zaidi kutoka katika chama chake inayomuelekeza afanye hivyo.
Aliwataka wanasiasa wasiingilie Tume hiyo, kwa sababu inafanya kazi muhimu kwa muktadha wa maisha ya Watanzania.
“Si vizuri tukiwa bado kwenye mchakato kuanza kutoka relini, suala la Katiba ni jambo nyeti na linahitaji mshikamano wa pamoja na si kutishia kujiondoa katika njia ya kuelekea kupata Katiba Mpya.
“Mimi kuwa Chadema kunatokana na dhamira yangu, lakini kikubwa ninachokiona ni kuwasaidia wananchi, hivyo hatuna budi kuungana kwa pamoja ili kuzaa Katiba yenye kumsaidia kila Mtanzania,” alisema Baregu.
Alisema yeye katika Tume hiyo ni mtaalamu pekee wa masuala ya Sayansi ya siasa, hivyo ana ufahamu umuhimu wake ndani ya mchakato wa kutengeneza Katiba mpya.
0 comments:
Post a Comment