Shambulizi la bomu Mogadishu.
Takriban watu wanane waliuawa na wengine kadha kujeruhiwa katika shambulizi la bomu katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu Jumapili.
Shambulizi hilo limefanywa siku mbili kabla ya kongamano kuu mjini London linalolenga kutafuta uungaji mkono kwa Somalia kutoka kwa jamii ya Kimataifa.
Shambulizi hilo la bomu lililenga eneo la K4 Kitongoji chenye shughuli nyingi katika mji huo m
kuu na kulenga msafara wa magari ya wajumbe waliokuwa ziarani kutoka Qatar.
Polisi wanasema wajumbe hao waliepuka bila majeraha lakini wapita njia waliokuwa karibu waliuawa na wengine kujeruhiwa. Daktari aliyekuwa katika eneo la tukio hilo Mohamoud Yarow alisema uharibifu uliotokea ulikuwa mkubwa.
Kundi la wanamgambo wa al-Shabab lenye ushirika na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida limekiri kufanya shambulio hilo. Na licha ya kudhoofishwa na vikosi vya ukanda huo, wanamgambo hao wameendelea kufanya mashambulizi ya hapa na pale.
Mwezi jana zaidi ya watu 30 waliuawa wakati wanamgambo wa al-Shabab walipovamia jengo la mahakama ya juu mjini Mogadishu. Wiki jana serikali ilifunga baadhi ya barabara na kuweka vizuizi kufuatia vitisho katika mji huo mkuu.
Kamanda wa wilaya Abdi Mohamoud Warsame alisema shambulizi la Jumapili lingekuwa na maafa zaidi kama serikali isingeweka ulinzi mkali.
Maafisa wa Somalia wanakutana London kwa kongamano kuu Jumanne linaloleta pamoja washirika wa kimataifa kusaidia katika ujenzi mpya wa Somalia.
0 comments:
Post a Comment