MATUKIO YA KISIASA.
KESI dhidi ya mwanachama aliyebakia wa kikundi cha magaidi wa Kinazi
hapa Ujerumani (NSU) kinachoshukiwa kuwauwa wageni kumi kwa misingi ya
ubaguzi imeanza mjini Munich, ikichukuliwa kama moja ya kesi kubwa
kabisa.
Wanane kati ya watu waliouawa walikuwa wahamiaji wa Kituruki, mmoja alikuwa Mgiriki na wa mwisho alikuwa askari polisi wa kike wa Kijerumani.
Zaidi ya polisi 500 wametawanywa mjini Munich katika siku hii ya mwanzo wa kesi hiyo, ambapo mitaa kuelekea na karibu na mahakama ya mkoa imefungwa, huku waandamanaji wakikusanyika nje ya jengo hilo la mahakama.
Picha zinazorushwa moja kwa moja kwa njia ya televisheni zinaonesha kiwango fulani cha makabiliano kati ya polisi na waandamanaji, kabla ya kesi hiyo kuanza.
Familia nyingi za wahanga wa matukio hayo ya kigaidi watamshuhudia kwa mara ya kwanza Zschäpe, mshukiwa pekee aliyebakia.
"Lakini maamuzi haya, vyovyote yatakavyokuwa, hayataweza kupunguza maumivu yetu.
Aidha afungwe maisha au la, hakuna anayeweza kumrudisha Halit Yozgat."
Amesema Kamil Saygin, mfanyakazi wa Idara ya Uhamiaji ya Mji wa Kassel na rafiki wa familia ya kijana wa Kituruki, Halit Yozgat, aliyeuawa tarehe 6 Aprili 2006.
Mauaji ya NSU
Msichana wa Kituruki akiwa amezuiliwa na polisi nje ya Mahakama ya Munich, akiwa sehemu ya waandamanaji.
Zschäpe anaaminika kuwa mmoja wa waasisi wa kundi la NSU,
ambalo lilifanya kazi zake kwa zaidi ya muongo mmoja bila kugunduliwa
nchini Ujerumani. Kundi hilo liligundulika mwezi Novemba 2011 kutokana na kujiua kwa washirika wawili wa Zschäupe na kuchomwa moto kwa nyumba ambayo inaaminika kutumiwa na wanachama wote watatu wa kundi hilo.
Siku chache baada ya moto huo, Zschäpe alijisalimisha mwenyewe polisi kwenye mji wa mashariki wa Jena.
Watu wengine wanne, wanaotuhumiwa kulisaidia kundi la NSU, pia wanashitakiwa. Kesi hii inatarajiwa kuchukua miaka miwili kabla ya kukamilika.
Kesi hii inachukuliwa kama muhimu kabisa nchini Ujerumani katika kipindi cha miongo kadhaa.
Kufichuka kwa matukio haya ya kigaidi kumebainisha namna ambavyo makundi ya siasa kali kama NSU yanavyoweza kufanya mauaji makubwa na kwa muda mrefu.
Pia yamedhihirisha uwezo mdogo wa jeshi la polisi kwani kundi hilo liliweza kuendesha shughuli zake kwa muda wa zaidi ya miaka kumi bila kugundulika.
Hans-Christian Ströbele, mbunge kutoka Chama cha Kijani, amekiambia kituo cha televisheni cha ARD hivi leo kwamba, NSU ni dalili ya kufeli kwa mfumo wa usalama nchini Ujerumani.
0 comments:
Post a Comment