WABUNGE wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamezuiwa kuchangia
hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliyowasilishwa
bungeni jana.
Walioathirika na zuio hilo ni Mbunge wa Ludewa, Deo
Filikunjombe na mwenzake wa Mwibara, Kangi Lugola.
Taarifa zinasema
wabunge walinyimwa nafasi kuchangia hotuba hiyo iliyowasilishwa na
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emanuel Nchimbi.
Wabunge hao machachari ambao wamekuwa wakiikosoa wazi wazi Serikali
ya chama chao, jana walikutana na kuzuizi hicho licha ya kufanya
jitihada za kutaka waruhusiwe kuchangia hotuba hiyo.
Juhudi za
wabunge hao zilionekana walipomfuata Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Uratibu na Bunge), Wiliam Lukuvi kuomba waruhusiwe lakini
walikataliwa.
Baada ya juhudi zao kugonga mwamba hawakuweza
kuendelea kukaa bungeni, badala yake waliondoka huku wakiacha mjadala wa
bajeti hiyo ukiendelea.
Hata hivyo haikuweza kufahamika mara
moja sababu za wabunge hao kuzuiliwa, ingawa inaweza kueleweka kuwa
wabunge hao wanaponzwa na misimamo yao mikali dhidi ya Serikali.
Wakingumza
na MTANZANIA kwa nyakati tofauti nje ya ukumbi wa Bunge, wabunge hao
walionyesha kusikitishwa na kitendo kilichofanyika cha kuwanyima fursa
ya kutoa mchango wao.
Lugola alisikitishwa na kitendo hicho
alichosema kuwa hakina maana nyingine zaidi ya kutaka kuwapunguza nguvu
na kuwaziba midomo.
“Utaratibu huu wa kupitia katika vyama
haufai, sisi wengine tuliupinga mapema tukasema mkiruhusu huu utaratibu
wabunge wengine hatutapata fursa ya kusema majina yatachakachuliwa, hiki
ndicho kinachotokea sasa,” alisema.
Naye Filikunjombe,
alishangazwa na kitendo hicho na kusema kuwa sababu zilizotolewa na
Lukuvi hazikujitosheleza kwani wapo wabunge waliochangia na majina yao
hayakuwamo katika orodha.
Alisema wabunge ‘waliuziwa mbuzi kwenye
gunia’ wakati wa kupitisha mabadiliko ya kanuni zitakazoongoza mjadala
wa Bunge la bajeti.
0 comments:
Post a Comment