BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WADAU: WAZIRI KAWAMBWA AKAMATWE-MWANAFUNZI

Uamuzi wa serikali hauwezi kufuta doa lililowekwa duniani kote kwamba wanafunzi wa Tanzania ni mbumbumbu. http://www.mtanzania.co.tzLICHA ya serikali kufanya uamuzi mgumu wa kufuta matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 na kuamua yaandaliwe upya, hatua hiyo imepingwa na wasomi pamoja na wanasiasa, kwa madai kuwa siyo suluhu ya tatizo lililojitokeza. Wakizungumzia uamuzi huo, wadau hao walisema kuwa hautasahihisha mfumo mbovu uliopo.

Pamoja na hilo, walisema serikali haipaswi kuachia jambo hili lipite hivi hivi bila Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na Katibu wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Joyce Ndalichako, kuachia ngazi, kwani kuna wanafunzi wanne waliopoteza maisha kutokana na matokeo hayo.

Juzi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, akitangaza hatua ya serikali kufuta matokeo hayo, alisema serikali imechukua uamuzi mgumu wa kuamua kuwafariji wanafunzi waliofeli mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012 ambapo alisema yataandaliwa upya kwa kutumia mfumo uliotumika mwaka 2011.

Lukuvi alisema uamuzi huo umetokana na kwamba asilimia kubwa ya wanafunzi waliofanya mtihani huo walipata alama sifuri.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliunda tume ya kuchunguza chanzo cha matokeo hayo kuwa mabaya, ambapo ripoti ya tume hiyo ilibaini pamoja na mambo mengine mfumo uliotumika kusahihisha ndiyo chanzo kikubwa cha anguko hilo kwa wanafunzi.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Profesa Nderakilo Kessy, amesema kitendo cha serikali kufuta matokeo ya kida

to cha nne ni usanii ambao hauwezi hutoa suluhu katika sekta ya elimu.

Aliwataka wote ambao wamehusika katika kutoa matokeo hayo wawajibishwe kutokana na matatizo yaliyowapata wanafunzi, ikiwemo baadhi kupoteza maisha.

“Hivi unasemaje tu unafuta matokeo wakati kuna watoto walipoteza maisha baada ya matokeo kutoka, kuna watoto wamepata msongo wa mawazo hadi leo hii, serikali inawasaidia vipi? Niseme tu kwangu huu ni usanii mkubwa, kwani hatua hii ilitakiwa kuchukuliwa mapema kabla hata matokeo hayajatangazwa.

“Huwezi kula chakula muda huo huo tumbo likakusumbua halafu ukasema utafute daktari wakati unafahamu kabisa umekula nini hadi ukapata tatizo la tumbo, mfumo huo ulikuwa unajulikana kwamba ndiyo umesababisha yote hayo, sasa kwa nini NECTA kwa kushirikiana na Waziri wa Elimu wasingechukua hatua mapema kabla ya kutangazwa kwa matokeo?, alihoji Profesa Kessy.

Alisema kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani, Joyce Ndalichako na Waziri wa Elimu, Dk. Shukuru Kawambwa wanapaswa kuwajibishwa, ikiwemo kuachia ngazi.

“Hakuna haja ya kuendelea kuwa na hawa watu katika hii sekta ya Elimu, naamini kabisa yote yaliyotokea Waziri alikuwa anafahamu na kama si yeye, basi Katibu Mkuu wake alikuwa anafahamu, kwa hiyo waamue wenyewe kujiuzulu na kama hawataki kufanya hivyo basi wawajibishwe,” alisema Profesa Kessy.


KAULI YA MSOMI
Mmoja wa wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema kuwa hata uamuzi huo wa serikali hauwezi kufuta doa lililowekwa duniani kote kwamba wanafunzi wa Tanzania mbumbumbu.

“Matokeo haya yameshatangazwa na kuwekwa kwenye mitandao, kwa hiyo hata yakifutwa haitafuta kwamba wanafunzi wa Tanzania ni kapa..lakini pia naona hii kama siyo suluhisho la kudumu, kwani serikali inapaswa kuangalia pia mfumo mzima wa elimu.”

Alisema kufutwa huko kwa matokeo hayo hakuwezi kufunika matatizo makubwa yaliyopo kwenye sekta ya elimu, ambayo imesahaulika kwa muda mrefu.

“Sekta hii ina matatizo mengi, ikiwemo nyenzo za kufundishia, walimu na maslahi yao, mitaala na mambo mengine mengi. Hata leo hii wakisema wamesahihisha na kusema wanafunzi wengi wamefaulu haitatoa jibu katika mfumo uliopo,” alisema.


MBATIA: KAWAMBWA AKAMATWA.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), amesema Waziri Kawambwa, ni kati ya wanaostahili kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria, kwa kuwa ndiye aliyesababisha matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Mbatia alisema hata kama tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, imesema wanafunzi hao walifeli kutokana na mfumo mpya wa usahihishaji, Dk. Kawambwa anatakiwa kuchukuliwa hatua kwa vile ndiye aliyeidhinisha mfumo huo utumike.

“Mimi ukiniambia anayetakiwa kuchukuliwa hatua siwezi kukubali kwamba awe ni Dk. Ndalichako (Katibu Mtendaji, Baraza la Mitihani la Taifa).

“Hapa anayehusika ni waziri, huyu ndiye aliyeruhusu mfumo huu utumike, yaani huyu waziri alitakiwa awe amejiuzulu tena angekuwa anajificha kwa aibu kwa sababu matokeo hayo yamekuwa mabaya kwa makusudi.

“Yaani mtu anafanya jambo makusudi, huku akijua matokeo yake, hapa ni sawa na jengo la ghorofa lililoanguka pale Dar es Salaam, hili halikuanguka kwa bahati mbaya, bali watu walikuwa wakijua kitakachotokea,” alisema Mbatia.

Pamoja na hayo, Mbatia aliwataka wanasiasa kutoingilia masuala ya kitaalam kwa sababu wanaweza kusababisha madhara bila kutarajia.

“Mambo mengine huwa yanaharibika kutokana na tabia yetu wanasiasa, hasa hasa sisi wabunge.

Wabunge tunatakiwa kuacha ushabiki wa vyama pale tunapokuwa tunajadili masuala ya kitaifa.

“Nasema hivyo kwa sababu jukumu la kwanza la mbunge ni kwa ajili ya taifa lake, jukumu lake la pili ni kwa jimbo lake la uchaguzi, jukumu la tatu ni kwa chama chake na jukumu lake la nne ni kufanya mambo kwa dhamira yake binafsi.

“Pamoja na wajibu huo, inavyoonekana wabunge wengi hatujui wajibu wetu na ndiyo maana wakati mwingine tunaingilia masuala ya kitaalam kwa kuangalia vyama vyetu.

“Kwa mfano, nilipowasilisha hoja yangu bungeni nikisema hapa nchini hatuna mitaala ya elimu, baadhi ya wabunge walinibeza kwa itikadi za vyama, kisha Serikali ikaleta bungeni mitaala ya kuokoteza.

“Lakini, kuhusu Bunge, ripoti hiyo ya waziri mkuu, inaliamsha Bunge letu tukufu kutoka kwenye usingizi wa kutumia itikadi za vyama katika kufanya uamuzi wa mambo ya kitaifa.

Alisema kuhusu serikali, imepiga hatua kwa kukiri udhaifu kwenye usahihishaji wa mitihani hiyo, japokuwa bado hajaridhika kuhusu hilo.

Kuhusu wanafunzi waliojiua baada ya kutoridhishwa na matokeo hayo mabaya, alisema kuna haja Serikali ifidie familia za marehemu kwa kuwa walipoteza maisha kutokana na uzembe uliosababishwa na baadhi ya watendaji serikalini.


CWT WATAKA KAWAMBWA ANG'ATUKE.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekia Oluoch, alisema kutokana na serikali kuamua kufuta matokeo hayo, ipo haja Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa pamoja na watendaji wake wakaona umuhimu wa kujing’atua.

Alisema kitendo cha kufutwa kwa matokeo hayo kinaonesha jinsi ambavyo hawakutekeleza majukumu yao ipasavyo tangu waingie madarakani, kwani kwa kipindi chao ndipo kumekuwa na matokeo mabaya ya mitihani.

Pamoja na hilo, alisema Wizara ya Elimu haina ushirikiano mzuri na walimu pamoja na CWT na ndiyo maana kila kukicha matokeo yanazidi kudidimia na kuwasababishia wanafunzi misukosuko ya kimaisha.

Alisema yapo mambo ya wazi ambayo yanaonesha jinsi ambavyo serikali haipo makini kupitia wizara zake ambapo mgomo wa walimu ulisitishwa, lakini hadi leo hakuna kinachoendelea, hali ambayo ni mbaya kielimu.


WAZAZI
Nao, baadhi ya wazazi waliozungumza na MTANZANIA Jumapili kwa nyakati tofauti, walisema tatizo la matokeo hayo lilianza kwa wasahihishaji kuwa na makundi miongoni mwao.

Mzazi Hassan Rashid alisema usahihishaji ulionekana bayana ni fitna hivyo ni vyema timu nzima ya wasahihishaji ikachukuliwa hatua, kwani wamewapa wazazi gharama kubwa za kuwatafutia watoto wao shule nyingine.


WANAFUNZI
Mmoja wa wanafunzi aliyezungumza na MTANZANIA Jumapili, Joseph Kessy, alisema wanaomba haki itendeke, kwani tayari wamewapotezea mwelekeo wa maisha yao.

Alisema ni wakati mwafaka sasa kwa serikali kuweka watu makini ili kuondoa dosari zinazojitokeza mara kwa mara na kuharibu misingi ya wanafunzi ambao ndiyo tegemeo la taifa la kesho.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari ya Green Acres, Julian Bujugo, ameitaka Serikali kutowatumia walimu katika kazi ya upangaji wa viwango vipya vya alama za mitihani, bali kazi hiyo ifanywe na wataalamu wa elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amesema hatua ya kuwatumia walimu kwa kushirikiana na Baraza la Mtihani (NECTA), inaweza isifanyike kwa ufanisi, kwani kundi kundi kubwa bado lina kinyongo na Serikali, hasa kutokana na madai yao ya malimbikizo ya fedha zao.

Akingumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, jana Bujugo, alisema kuwa hatua ya serikali kufanyia kazi mapendekezo ya tume iliyoundwa na Waziri Mkuu ni ya kupongezwa na kila Mtanzania ambaye alikuwa anatafakari namna ya kulisaidia kundi kubwa la wanafunzi ambalo limeathirika kisaikolojia.

Habari hii imeandaliwa na Elizabeth Mjatta, Christina Gauluhanga, Hadia Khamis, Bakari Kimwanga, Dar es Salaam na Maregesi Paul Dodoma.

Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: