NELSON MANDELA.
MZEE MANDELA AKIFUR
AHIA JAMBO NA WATOTO.
MZEE MANDELA AKIWA NA MICHAEL JACKSON
PROTORIA.
IKULU ya Afrika Kusini imetoa taarifa kuwa hali ya
Rais wake wa zamani, Nelson Mandela imezidi kuwa mbaya katika siku mbili
zilizopita.
Taarifa hiyo ilithibitishwa na Rais Jacob Zuma
ambaye kwa mara ya kwanza alikiri hadharani kwamba hali ya afya ya
Mandela ni mbaya na madaktari wanaendelea na juhudi za kuokoa maisha
yake.
Zuma ambaye pia ni Rais wa Chama cha African
National Congress (ANC), alikiri kufadhaishwa na hali ya kiongozi huyo
wa zamani, alipomtembelea katika Hospitali ya Magonjwa ya Moyo ya
Medi-Clinic mjini Pretoria na kuzungumza na mkewe, Graca Machel kuhusu
hali yake.
Kumekuwa na taarifa kwamba tangu alipofikishwa hospitali, Mandela amekuwa hajitambui na amekuwa akipumua kwa msaada wa mashine.
Pia, kumekuwa na ulinzi mkali katika hospitali
hiyo alikolazwa huku waandishi wa habari na watu wasiokuwa wanafamilia
wakizuiwa kwenda kumwona.
Ilielezwa pia kwamba ulinzi ulizidi kuimarishwa jana katika maeneo yanayozunguka hospitali hiyo.
ANC ambacho ndicho chama kinachotawala Afrika
Kusini, pia kilitoa taarifa yake jana asubuhi kikielezea wasiwasi kuhusu
afya ya kiongozi wake huyo wa zamani maarufu kwa jina la Madiba kuzidi
kuwa mbaya.
Msemaji wa chama hicho, Jackson Mthembu aliwataka
wananchi wa Afrika Kusini na dunia kwa jumla kuwaombea Mandela, ndugu
zake na madaktari.
Hatua hiyo imesababisha simanzi na majonzi kwa
wananchi wa Afrika Kusini ambao wamekuwa wakimwombea na kutoa salamu za
kumtakia afya njema.
Mandela alilazwa katika Hospitali ya Moyo ya
Medi-Clinic, Juni 8, mwaka huu kutokana na maradhi ya homa ya mapafu
yanayomsumbua na iliripotiwa kwamba tangu wakati huo hajitambui.
Hatua ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais Zuma
kutangaza kwamba hali ya Mandela ni mbaya, imeongeza wasiwasi kwa
wananchi na wengi wameitikia wito wa kuendelea kufanya maombezi maalumu
kwa Mandela.
Hata hivyo, ofisa mmoja mwandamizi wa Serikali
ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema kwa sasa hali ya Madiba si
nzuri na kwamba wananchi wa Afrika Kusini wasiwe na matumaini kupita
kiasi kuhusu kuimarika kwa hali ya afya yake.
CHANZO MWANANCHI.
CHANZO MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment