ASILIMIA 20 ya bajeti ya serikali 'hutafunwa' kwa njia ya rushwa na kukwamisha shughuli za maendeleo nchini kutofikia malengo.
Mbunge wa Magu Mjini (CCM), Dk. Festus
Limbu, alisema hayo wakati akiwasilisha mada ya majukumu ya kamati za
kudumu za Bunge katika mapambano dhidi ya Rushwa nchini na nini
kifanyike.
“Inakadiriwa kuwa asilimia 20 ya bajeti ya
Serikali huliwa na rushwa kila mwaka,”alisema Dk. Limbu na kuongeza
kuwa taarifa za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na
mapendekezo ya Kamati za Bunge hayafanyiwi kazi ipasavyo na serikali.
Semina hiyo ya kuwajengea uwezo wabunge
iliyoandaliwa na Bunge kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la
Maendeleo (UNDP) iliwahusisha wabun
ge wanachama wa Chama cha Wabunge
walio katika mapambano dhidi ya rushwa (APNAC).
Naye Mkuu wa shule ya Sayansi za jamii
Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa David Mwamfupe, akitoa mada kuhusu
"Changamoto zinazoliokabili Bunge na serikali katika mapambano ya rushwa
nchini na suluhisho lake" alisema mwingiliano wa kisiasa ni miongoni
mwa changamoto zinazokabili mapambano hayo.
“Vita hii inatishia nafasi zetu za kisiasa
na maslahi binafsi na baada ya kuona tishio lazima mtu ajihami hata kwa
kutumia rushwa yenyewe,”alisema.
Wakichangia katika semina hiyo, wabunge
walitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Bunge
kuwaelimisha wapiga kura juu ya wajibu wa mbunge ili kuondoa vitendo vya
kuomba rushwa kwa njia ya kudai huduma ambazo sio wajibu wao.
Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vicent
Nyerere aliwataka wananchi kutowashinikiza kutoa rushwa kwa kushinikiza
kupewa huduma ambazo si wajibu wa wabunge.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally
Keisy alisema kugundua kuwa kiongozi yoyote anapokea rushwa ni rahisi
kwa kuwa wanaweza kupiga mahesabu ya idadi ya thamani ya mali zake kama
inalingana na mapato yake.
Pia alisema vyombo vya dola viache kuwakamata watumishi wanaotoa ama kupokea rushwa ndogo ndogo kwa sababu hizo ni zawadi tu.
Mbunge wa Manyovu (CCM), Albert
Ntabalile, alisema Serikali ni chanzo cha rushwa kwa kuwa huduma
zinazotolewa hazikidhi mahitaji ya wananchi.
Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Moza alitaka Takukuru kujisafisha yenyewe kwasababu huwa havina siri vinavyopewa taarifa za rushwa.
Akijibu Waziri wa Nchi Utawala Bora,
George Mkuchika, alisema kuwa maandalizi ya kubadilisha Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi kuwa Tume ya Maadili ya Viongozi yameshakamilika na
mapendekezo yapo serikalini.
Alisema lengo ni kukiongezea nguvu chombo
hicho, kiweze kuwa na meno ya kutoa adhabu kwa wale watakaokutana na
makosa ya kukiuka maadili.
Aidha, alisema bado suala la Takukuru
kuwakamata watu na kupeleka faili kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa
Serikali (DPP), kwa ajili ya kutoa kibali cha kushtakiwa limekuwa katika
mjadala wa kubadilisha utaratibu huo.
Alisema kutokana na Takukuru kutokuwa na
mamlaka ya kumshtaki mtu moja kwa moja ndio maana vyombo hivyo vimekuwa
vikilalamikiwa kuwa vinatupiana danadana vinapolizwa kuhusu kesi
mbalimbali za rushwa.
SOURCE:
NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment