BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

FAMILIA: HAITARUHUSU KUSITISHA MATIBABU KWA MZEE NELSON MANDELA.

JOHANNESBURG
FAMILIA ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela imesema haitaruhusu kusitishwa kwa matibabu anayoendelea kuyapata na kwamba itaendelea kufanya juhudi za kurefusha uhai wake hadi Mungu atakapoamua kumchukua.
Kauli hiyo ilitolewa jana na mwanawe mkubwa, Makaziwe Mandela huku kukiwa na taarifa kwamba kiongozi huyo hajitambui na anasaidiwa kuendelea kuishi kwa mashine tangu alipofikishwa hospitalini huko Pretoria wiki mbili zilizopita.
Alisema kwamba familia haiwezi kuacha kumhudumia kwa shinikizo la watu wa pembeni wanaodai kwamba inatakiwa imruhusu akapum
zike kwa amani na kwamba kwa mujibu wa mila za Wathembu, watafanya hivyo endapo tu mhusika mwenyewe (Madiba), atakapotamka.
Juzi, kwa mara ya kwanza, Rais Jacob Zuma alikiri hadharani kwamba hali ya shujaa huyo wa Afrika Kusini ni mbaya na anahitaji maombezi. Alisema hayo baada ya kumtembelea na kuzungumza na mkewe, Graca Machel-Mandela.
Hata hivyo, taarifa zilieleza kwamba hajaweza kuzungumza tangu alipofikishwa hospitali, bali alifungua macho kwa shida mara kadhaa.
Mandela anayesumbuliwa na maradhi ya homa ya mapafu alifikishwa katika Hospitali ya Magonjwa ya Moyo ya Medi-Clinic, Pretoria Juni 8 na tangu wakati huo, taarifa zimeeleza kwamba hajaweza kuzungumza lolote.
Taarifa zikieleza kwamba hali yake ilizidi kuwa mbaya Jumapili iliyopita na baadhi ya wanafamilia tayari wameshatangulia kijijini kwake, Qunu.
Gazeti la Mail&Guardian la Afrika Kusini lilieleza jana kwamba wanafamilia hao walifanya kikao maalumu nyumbani kwa Mandela, kisha kutembelea na kufanya ukaguzi katika eneo la makaburi ya familia, sehemu ambayo kiongozi huyo pia anaweza kuzikwa.
Makaburi hayo yako jirani na nyumba ya mdogo wake, Morris na haikuwekwa wazi kuhusu uamuzi wa wanafamilia hao kufika eneo hilo la makaburi, lakini kwa mujibu wa mila na desturi za watu wa Kabila la Xosa, familia hutembelea eneo hilo wanapobaini kwamba mmoja wa wanafamilia yuko mbioni kuungana na waliotangulia mbele za haki, au kuomba sala maalumu kwa ajili ya kupata ridhaa ya kurefusha maisha ya mhusika.
Pamoja na mkutano huo, wanafamilia hao walifanya mazungumzo na machifu wa eneo hilo, wakiongozwa na Chifu Bhovulengwe wa Baraza la Kifalme la Abathembu.
Wanafamilia waliofika na kuhudhuria kikao hicho cha jana ni pamoja na mkewe wa zamani, Winnie Madikizela-Mandela na Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala, Lindiwe Sisulu pamoja na Kiongozi wa Chama cha United Democratic Movement, Bantu Holomisa.
Iliarifiwa kwamba kikao hicho kilifanyika kutokana na simu ya dharura iliyopigwa kwa wanandugu na wanawe, Mandela, Thanduxolo, Ndaba na Ndileka Mandela ambao tayari walishawasili kijijini hapo tangu Jumapili na kujumuika na wanafamilia wengine.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: