BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HAYA NI MAJANGA KWA WANASANII ?.

Albert Kenneth Mangweha ‘Ngwea’.

HUKU mwanamuziki wa Hip Hop Bongo, Langa Mangisen Kileo akitarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya Kinondoni, Dar, Ijumaa Wikienda limebaini kuwa vifo mfululizo vya mastaa huku wengine wakiwa wagonjwa sasa ni majanga, ingia ndani usome ripoti kamili ya kusikitisha.KIFO CHA LANGA ?.
 
Siku chache baada ya Mwana Hip Hop Albert Kenneth Mangweha ‘Ngwea’ kutangulia mbele ya haki, Langa naye alifariki dunia Alhamisi iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar baada ya kulazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), akisumbuliwa na malaria, hiyo ni kwa mujibu wa Afisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Eligaesha.

Langa Mangisen Kileo.
Akizungumza na Ijumaa Wikienda juu ya kifo cha mwanaye, baba mzazi wa Langa, Mengisen Kileo alisema kuwa alizidiwa Jumapili ya Juni 9, mwaka huu na kukimbizwa katika Hospitali ya Kinondoni ‘Kwa Dokta Mvungi’, Dar lakini Jumatano hali ilikuwa mbaya hivyo ikabidi akimbizwe Muhimbili.
 
Kwa mujibu wa baba huyo, Langa alikuwa na malaria kali iliyopanda kichwani lakini pia alikuwa na homa ya uti wa mgongo ambayo haikugundulika mapema ndipo akakutwa na umauti.
Jaji Khamis 'Kashi'.
UCHAMBUZI KILICHOMUUA LANGA NDICHO KILIMUUA NGWEA!
Katika mahojiano na gazeti hili miezi kadhaa iliyopita, Langa alikiri kuwa aliingia kwenye matumizi ya madawa ya kulevya ‘unga’ kutokana na msongo wa mawazo ‘stress’ baada ya kudhulumiwa na kukataliwa kusambazwa kwa kazi zake za sanaa.
 
Maswali yaliyosababisha Langa akaeleza hayo ni pale alipoulizwa kwa nini alijiingiza kwenye unga na mbona hasikiki ?.
 
Langa: Kwanza nilikuwa na frustration (kuchanganyikiwa) sana, stress zilikuwa haziishi kwa sababu nilikuwa nafanyiwa hujuma.
 
Nilitetengeneza albamu kali iliyokwenda kwa jina la Langa. Nadhani hakuna ngoma ya Hip hop Kibongobongo iliyowahi kukalisha kama Matawi ya Juu. Ilikuwa moja ya ngoma kali kwenye ile albamu. Nilipoipeleka kwa msambazaji akakataa makusudi kuisambaza. Sikuishia hapo, niliwapelekea wadau wengine wengi lakini walichomoa kuisambaza, basi nikajua kuna hujuma.
 
Si unajua tena mambo ya kusizi kitaa? Ndiyo nikaingia kwenye mambo ya wida (bangi) na unga kupunguza stress lakini sasa hivi nimeacha.
 
Mwandishi: Vipi kuhusu kukaa kimya muda mrefu bila kusikika ?.
 
Langa: Nina ngoma nyingi sana sema tu huwa hazisikiki kutokana na kubaniana kwenye gemu. Kama vipi uje home (nyumbani) nikusikilizishe, huwa nazisikiliza mwenyewe.
LANGA KAMA NGWEA
Ukipitia maelezo hayo hayana tofauti na yale aliyoyatoa marehemu Ngwea kuwa alikuwa akidhulumiwa, kubaniwa, kukataliwa kusambazwa kwa kazi zake na wakati mwingine kutishiwa maisha hivyo akajikuta akijiingiza kwenye bangi, unga na pombe kali ili kuondoa msongo wa mawazo kama ilivyokuwa kwa Langa.

Waombolezaji wakimlilia mwigizaji Hassan Ahmad ‘Mzee wa Zeze’.
MSANII MWINGINE WA FILAMU AFA KIMYAKIMYA !.
 
Saa mbili kabla ya Langa kukata roho, tasnia ya filamu za Kibongo nayo ilipata simanzi baada ya mwigizaji Hassan Ahmad ‘Mzee wa Zeze’ kufariki dunia kimyakimya akiwa ameugua kwa muda mfupi.
 
Mzee wa Zeze alifariki dunia mishale ya saa 9:00 alasiri katika Hospitali ya Temeke, Dar akisumbuliwa na maradhi ya ini na figo.
 
Mzee wa Zeze ambaye alizaliwa Novemba 4, 1975, Dar aliaga dunia akiwa hana mke wala mtoto.
 
Akizungumza msanii mwenzake ambaye alikuwa rafiki yake wa karibu, ambaye pia alikuwa akimchezesha katika filamu zake, Deogratius Shija alisema ameumizwa na msiba huo kwani alikuwa ni msanii wake ambaye alikuwa akimtegemea na pengo lake halizibiki.
 
Mzee wa Zeze ambaye alifanya vizuri kwenye filamu kama Chanzo ni Mama, Where is God na My Book alizikwa Ijumaa iliyopita katika Makaburi ya Mwinyimkuu yaliyopo Magomeni, Dar ambapo mazishi yake yalihudhuriwa na wasanii wachache.
Mtangazaji wa Kituo cha Radio Times FM, Khadija Shaibu ‘Dida’.
DIDA NAYE MGONJWA
Huku wasanii hao wakiwa wameaga dunia, naye Mtangazaji wa Kituo cha Radio Times FM, Khadija Shaibu ‘Dida’ ni mgonjwa akiwa hoi kitandani.
 
Dida alilazwa katika Hospitali ya Amana, Dar akisumbuliwa na malaria kali ambayo ilimsababisha ashindwe kuinuka kitandani hadi ainuliwe na kulishwa chakula na mtu ambaye alikuwa akimsaidia.
 
Ijumaa iliyopita, Ijumaa Wikienda lilifanikiwa kuingia kwenye wodi namba nne aliyokuwa amelazwa Dida na kuzungumza naye kwa taabu kuwa anasumbuliwa na malaria kali huku ndugu wakihaha ili apone.
Crispine Masele ‘Chapombe’.
MASELE CHUPUCHUPU KUUAWA.
Wakati hao yakiendelea, ripota wetu kutoka Tanga anaeleza kuwa staa wa vichekesho Bongo, Crispine Masele ‘Chapombe’ alinusurika chupuchupu kuuawa na raia wenye hasira kali baada ya kuwagonga watu wawili kwa gari.
 
Masele alikutwa na mkasa huo maeneo ya Barabara ya 14 jijini hapa ambapo wasanii wenzake wa Kundi la Vituko Show walipatwa na mshtuko mkubwa na kutia timu kwa kuwa walikuwa kwenye ziara ya kikazi.
Gari la Masele likiwa limevunjwa vioo.
Maelezo yaliyopatikana polisi yalieleza kuwa Masele alimgonga mtu na kumvunja mguu, wakati anasogeza gari mbele ili apaki aongee na raia, ghafla mawe yakaanza kurushwa na watu asiowatambua.
 
Ili kuokoa uhai, Masele alijaribu kukimbia na gari ndipo akamgonga mtu mwingine ambaye kwa bahati nzuri hakuumia, raia wakamvamia na kulipiga gari mawe na kumpora kila kitu.
 
Ilidaiwa kuwa raia hao walitaka kumuua, ndipo wasamaria wema wakaita polisi kutoka Kituo cha Mabawa ambao walimchukua msanii huyo kwa ajili ya mahojiano zaidi.
NA GLOBAL PUBLISHER.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: