KIKONGWE Somoe
Issa, anayekadiriwa kuwa na umri zaidi ya miaka 90, ambaye aliwahi kutishia
kuigeuza gesi kuwa maji iwapo serikali itaendelea kulazimisha kusafirisha
kwenda Dar es Salaam, sasa hajulikani alipo.
Taarifa zilizoifikia
MTANZANIA Jumapili ambayo ipo mkoani Mtwara, zilidai kuwa bibi huyo baada ya
kutoa tishio hilo sasa amefichwa, ili asiweze kutekeleza lengo lake
hilo.
Bibi Somoe, anayeaminika kama Mkuu wa Kaya ya Msimbati, kijiji
ambacho gesi asilia iligundulika, sasa hajulik
ani alipo, huku ndani ya kijiji
hicho ulinzi mkali ukiwa umeendelea kutawala.
Ulinzi
umeimarishwa katika kijiji hicho, lengo likiwa ni kuhakikisha hakuna mtu
anayefika karibu na nyumba aliyokuwa akiishi bibi huyo.
MTANZANIA Jumapili, lilifika katika kijiji hicho juzi, ambako liliweza
kuzungumza na Mwenyekiti wa Kijiji cha Msimbati, Salum Athuman Tostao, ambaye
alikiri kuwa bibi huyo hayupo na wala haifahamiki alikopelekwa.
“Ni
kweli bibi huyu hajaonekana tangu palipotokea vurugu na watu wa usalama
waliokuwa wakitaka kumuiba, kama unavyofahamu kulikuwa na mtu aliyejifanya
mwandishi wa habari alitaka kumuiba bibi huyu, lakini wanakijiji wakamshtukia
na kuchoma gari lake moto.
“Kutokana
na hali hiyo, mpaka sasa hatufahamu alipo na hatujui kama ni serikali au
wanafamilia wamemficha, kwa sababu kwanza hawaturuhusu hata sisi ambao ni
viongozi kufika maeneo ya nyumba aliyokuwa akiishi kwa sababu wanadhani
tutaleta watu wengine wasiokuwa waaminifu kwa familia hiyo,” alisema Tostao.
Gazeti
hili lilipomtafuta mtoto wa bibi huyo, Manzi Faki, alikataa kuzungumza chochote
kuhusu mama yake, lakini aliitaka serikali kutekeleza ahadi zake kwa
Wanamtwara.
“Hilo
suala la mama sitaki kulizungumzia kabisa… jambo la muhimu serikali inapaswa kufahamu
kuwa sisi wana Mtwara tunataka itekeleze ahadi ilizotuahidi ndipo waje kuchukua
hicho kidogo wanachokitaka, zaidi ya hapo kijumla gesi haitoki,” alisema Faki.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Mtandi, Salum Waziri, alieleza kuwa bibi huyo anaaminiwa na wanakijiji
wenzake kutokana na uwezo wake wa kuzuia mambo yasiyotakiwa ndani ya jamii,
sambamba na kuleta riziki pale wanapokwenda kumuomba.
“Kwa
kweli sasa ulinzi mkali umeimarishwa na wanakijiji, hakuna mtu anayefika
nyumbani kwake, hata sisi wenyewe hatuthubutu, ndiyo maana hatufahamu
alikopelekwa.
“Nakumbuka
bibi aliwahi kutumiwa na kampuni ya Artumas kukwamua mashine iliyokuwa imenasa
katika mchakato wa uchimbaji wa gesi hiyo baharini, ambapo wazungu hao
walihangaika kuita wahandishi nje ya nchi, lakini wote wakashindwa, ndipo
waliponong’onezwa kuhusu bibi huyo wakamwendea na akaja kunasua.
“Wakampa
zawadi ya kumjengea nyumba, haya ni mambo ambayo yalitokea mwaka 1994, kiujumla
yapo mengi ambayo yametufanya tumwamini sana,” alisema Waziri.
Januari
mwaka huu, Afisa usalama mmoja anayedaiwa kufahamika kwa jina la babu alijikuta
katika wakati mgumu kiasi cha gari lake kuchomwa moto huku yeye mwenyewe
akikimbilia kusikojulikana baada ya kuzuka vurugu kubwa wakati akimshawishi
bibi huyo asizuie gesi kwenda Dar es salaam.
Inadaiwa
kuwa mwanausalama huyo alitumwa na viongozi wa juu wa serikali baada ya bibi
huyo kutamka wazi kuwa gesi haitoki Mtwara kauli ambayo iliwafanya viongozi
kupata wasiwasi na hivyo kumtuma mtu huyo ili amshawishi bibi huyo.
Wakati
bibi huyo akizungumza na mwanausalama huyo inadaiwa kuwa aliwaita wajukuu zake
wamsikilize ndipo vurugu kubwa zilipoibuka na kusababisha mwanausalama huyo
atimue mbio huku akilitelekeza gari lake.
Juzi
na jana baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wakizungumza na gazeti hili walisema
wao hawazuii gesi kutumiwa na Watanzania, ila wanataka gesi hiyo ichakatwe
hapohapo mkoani Mtwara na ndipo isafirishwe kuelekea sehemu nyingine.
Vurugu
kuhusu gesi hii ya Mtwara zilianza kuibuka Novemba mwaka jana, wananchi wa mkoa
huo walikuwa wakipinga ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam.
Pamoja
na vurugu hizo kuzimwa mara kadhaa na Jeshi la Polisi, ambao sasa
wanashirikiana na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), lakini bado MTANZANIA
Jumapili imeshuhudia hali ya amani haijaweza kurejea mkoani humo.
Baadhi
ya watu mkoani hapa, bado wanaendeleza visasi kwa kuchoma nyumba za wenzao,
huku JWTZ wakidaiwa kuwapiga raia kila mara hata inapotokea kuwa wamezomewa.
About mtanda blog
Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
0 comments:
Post a Comment